Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya Arumeru Mashariki kimelaani vikali kitendo
cha Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Alexender Mnyiti kumuweka rumande Diwani wa Kata
ya Embaseny Gadieli Mwanda kwa saa 48 na
kudai kuwa kitendo hicho ni matumizi mabaya ya madaraka.
Katibu wa
CHADEMA Wilaya ya Arumeru Elisa Stephen
Mungure amesema kuwa kitendo hicho ni
udhalilishaji dhidi ya viongozi wa upinzani ambao wamekua wakikamatwa mara kwa
mara na kuwekwa rumande .
Mungure
alisema kuwa mbinu hiyo imekua ikitumika kwa hila ili kudhoofisha na kuua upinzani hivyo chama chake
kimejipanga kukabiliana na hila hizo za kisiasa.
“Diwani wa
Kata ya Embaseny alitakiwa kuripoti katika kituo cha polisi cha Usariver
septemba 20 mwaka huu ndipo alipokutana na Amri ya Mkuu wa Wilaya ya kuwekwa
ndani kwa masaa 48 bila kuhojiwa ,jana
alifikishwa mahakama ya Mwanzo ya Enaboishu na kutuhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya
udanganyifu kupitia mradi wa Kuku Kukua ambao Diwani huyo siyo muhusika ,tunamshukuru
Mungu amepata Dhamana” Alisema Mungure
Akizungumza
baada ya kupata Dhamana katika mahakama hiyo Diwani huyo Gadiel Mwanda ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Chadema jimbo la Arumeru Mashariki alisema kuwa Mkuu wa
Wilaya alifanya ziara katika kata yake na kuzungumza na Wananchi ,baadhi ya
watu ambao wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM walimshutumu kuwa anahusika na
mradi huo alipotaka kujitetea alinyimwa nafasi hiyo na kuamriwa kufika kituo
cha polisi asubuhi na mapema ndipo alipokutwa na masaibu hayo.
Mwanda
alisema kuwa misigano ya kisiasa inayotekea inalenga kuzorotesha juhudi za
maendeleo ambazo amekua akizifanya kwa kushirikiana na wananchi jambo ambalo
litawaathiri wananchi wengi hivyo amewataka wananchi kuendelea na juhudi hizo
ikiwemo ujenzi wa zahanati ya kisasa.
Kwa upande
wao wananchi wa kata hiyo Ester Swai na Agnes Elia wamesema kuwa kukamatwa kwa
viongozi kila mara kunazua hali ya taharuki miongoni mwa wananchi hivyo
wamezitaka mamlaka husika kutimiza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki
na usawa.
Post a Comment