Kikwete alisema hayo alipofungua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kwenye ukumbi wa White House, makao makuu ya CCM, mjini hapa jana. Kauli hiyo ya Kikwete inamaliza minong’ono ya muda kuwa hapangekuwa na kupokezana kijiti katika mkutano huo.
Pia kauli hiyo imezima madai kwamba kungekuwa na mchujo katika uchaguzi wa Mwenyekiti, ambapo majina hadi matano yangependekezwa na Kamati Kuu na kupelekwa katika Halmashauri Kuu ambayo ingekata mawili na kupeleka matatu kwenye Mkutano Mkuu Maalumu, ili yapigiwe kura kumchagua Mwenyekiti.
“Ajenda yetu kubwa leo (jana) ni moja tu; nayo ni kupendekeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili nayo Halmashauri Kuu ya Taifa ipendekeze kwa Mkutano Mkuu wa CCM ili achaguliwe kuwa Mwenyekiti wa CCM,” alisema Kikwete kwenye ufunguzi huo wa Kamati Kuu, akitumia dakika tano tu, kisha wajumbe wakaendelea na ajenda. Rais Magufuli alichaguliwa kuongoza Tanzania Oktoba mwaka jana.
Katika hotuba yake hiyo ya jana, Kikwete aliwajia juu ‘wafitini’ walioombea chama hicho kife katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Alisema “Wapo watu walidhani CCM ingekufa na walishajiandaa na salamu za rambirambi. Walidhani wataibuka. Hawakuibuka na hawataibuka kamwe.”
Kikwete aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa kilikuwa kikao chake cha mwisho cha Kamati Kuu, kauli iliyobainisha wazi kuwa anang’atuka kumwachia kijiti Rais Magufuli kuongoza chama.
Alisema amekuwa Mwenyekiti wa Chama kwa miaka 10, hivyo aliwashukuru wajumbe wa Kamati Kuu kwa kumsaidia katika kipindi chote hicho huku akisisitiza; “Bila msaada wenu CCM isingekuwa imara kama ilivyo hivi leo.”
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Rais Magufuli alikuwa akifahamika kama Tingatinga na kwenye mikutano kadhaa, Rais mstaafu Kikwete aliweza kumuita kwa jina hilo.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete jana alikagua ukumbi wa mikutano wa CCM na kuoneshwa sehemu mbalimbali ambapo alisema ameridhika na maandalizi ya mkutano kwamba yanaenda vyema.
Maeneo mengine aliyotembelea ni mabanda ya mama na baba lishe, sehemu za kutolea huduma za Benki na mabanda ya maonesho ya wajasiriamali.
Katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana, makamu Mwenyekiti Bara, Phillip Mangula, waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Nape Nnauye, msemaji wa CCM Christopher Ole sendeka, naibu katibu mkuu wa CCM Bara Rajab Luhwavi na wajumbe wa Kamati Kuu Pindi Chana na Mohamed Seif Khatib. Wajumbe wa mkutano Mkuu maalum wa CCm walianza kuwasili jana na wengine wengi wanatarajiwa leo.
Post a Comment