SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amempa siku tatu Mbunge wa Viti Maalumu,
Susan Lyimo (Chadema) awasilishe mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge,
maelezo ya utetezi dhidi ya madai aliyotoa bungeni kuhusu Serikali
kununua magari ya washawasha 777.
Ndugai alitoa amri hiyo kutokana na mwongozo ulioombwa na Naibu Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni juzi akitaka Lyimo
athibitishe au afute kauli yake juu ya madai hayo wakati serikali
imenunua magari 32.
“Hata kwa akili ya kawaida haiwezekani Serikali ikaagiza magari yote
hayo 777 ya washawasha. Ninachokumbuka mimi Waziri huyu aliwahi kusema
hapa bungeni kuwa magari hayo 777 ni idadi ya magari yote ya aina
mbalimbali yaliyonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya polisi,” alisisitiza
Ndugai.
“Sasa nakutaka uniandikie rasmi majibu vizuri kuhusu kauli yako hii,
nakupa siku tatu uwe umeniletea na baadaye nitaipeleka taarifa yako kwa
Kamati ya Maadili ya Bunge, ili kujadili suala hili kwa
mapana,”alisisitiza Ndugai.
Awali mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Ndugai
alimpatia mbunge huyo nafasi ya ama kufuta kauli yake hiyo au
aithibitishe kabla ya hatua za kikanuni za Bunge hazijachukuliwa dhidi
yake.
Lyimo alikataa kufuta kauli hiyo na kudai kuwa anao uthibitisho juu ya
idadi hiyo ya magari aliyoitamka na kusisitiza kuwa amenukuu taarifa za
idadi hiyo kupitia taarifa iliyotolewa na mtandao wa Jamii forum pamoja
na taarifa za Hansad za Bunge.
“Mheshimiwa Spika mimi ni mtu mzima siwezi kwenda kwa hisia za watu, ni
kweli jana niliombewa mwongozo bahati mbaya sikuwepo ndani ya Bunge.
Nathibitisha kauli yangu na wala siifuti kwa kuwa nina uhakika na idadi
ya magari niliyoisema,” alisisitiza mbunge huyo.
Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 63 (2) ya Bunge, mbunge hatasema uongo
endapo chochote atakachokisema ndani ya Bunge atakuwa amekirejea kwenye
chombo cha habari au taarifa za Bunge.
About Author
Journalist , Enterpreneur, Lecturer and Blogger. Email :ngoboleaa@gmail.com.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post a Comment