PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Naibu Spika Achafua Hali ya Hewa Bungeni Baada ya Kumwita Mbunge BWEGE
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga she...


 

Naibu Spika Tulia Ackson, ambaye katika vikao vya Bunge anatakiwa kusimamia mijadala kwenye chombo hicho cha kutunga sheria, jana alizua kizaazaa baada ya kumuelezea mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Said Bungara kuwa ni bwege, akimtaka aache kuonyesha hali hiyo.


Kwa mujibu wa toleo la pili la Kamusi ya Kiswahili Sanifu (Oxford) la mwaka 2004, neno bwege linamaanisha “mtu mjinga, mpumbavu, bozi, fala gulagula”.


Kitendo cha kutumia neno bwege kumuelezea mbunge huyo kilisababisha wapinzani wacharuke, na kuibua bungeni kesi ya mtu aliyefunguliwa mashtaka mkoani Arusha kwa kosa la kumuelezea Rais John Magufuli kuwa ni bwege.


Bila ya kuruhusiwa, mmoja alifungua kipaza sauti na kusema: “Hatimaye msamiati wa bwege watua bungeni sasa kutumika rasmi. Futa lugha ya kuudhi; bwege bwege.”


Hata hivyo, wabunge hao wa upinzani hawakushinikiza Dk Tulia kufuta kauliz yake, lakini baadaye wakiwa nje ya ukumbi waliponda kitendo hicho cha kiongozi huyo wa Bunge ambaye aligombea uspika kwa tiketi ya CCM kabla ya kujitoa na muda mfupi baadaye kuteuliwa na Rais Magufuli kuwa mbunge na hivyo kupata sifa ya kugombea nafasi hiyo ya naibu spika.


Dk Ackson aliamsha tafrani hiyo saa 5:48 asubuhi baada ya Bungara, ambaye ni maarufu kwa jina la Bwege, kusimama bila kufuata kanuni za Bunge, kupinga maelezo ya Waziri wa Habari, Nape Nnauye juu ya uamuzi wa Serikali kusitisha shughuli za Bunge kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni nchini.


“Na wewe Mheshimiwa Bwege, hebu kaa chini. Usionyeshe ubwege wako hapa,”alisema Dk Ackson kumzuia mbunge huyo asiendelee kuzungumza wakati mjadala ukianza kuwa mkali.


Mjadala huo uliendelea bila ya wapinzani kuhamaki, lakini baada ya Nape kutoa taarifa akieleza kuwa uamuzi wa kuanzisha studio za Bunge ulifanywa na Bunge la Kumi ambalo yeye hakuwamo, ndipo wapinzani walipokumbusha kauli hiyo ya naibu spika.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top