PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Waziri wa Ardhi, William Lukuvi Akataa Rushwa ya Bilioni 5
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Waziri wa  Ardhi, William Lukuvi amesema rushwa imekithiri kwenye sekta ya ardhi kiasi kwamba wafanyabiashara wawili walimuahidi ru...



Waziri wa  Ardhi, William Lukuvi amesema rushwa imekithiri kwenye sekta ya ardhi kiasi kwamba wafanyabiashara wawili walimuahidi rushwa ya Sh5 bilioni afanikishe mpango wao wa kuiuzia Serikali ardhi kwenye eneo linalotakiwa kujengwa mji wa kisasa wa Kigamboni.


Mji huo kabambe wa Kigamboni unajumuisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada, Somangila na eneo lote lina ukubwa wa takribani ekari 6,000.



Awali mradi huo ulitarajiwa kugharimu Sh13 trilioni ambazo zingetolewa na Serikali, lakini ikaamua kushirikisha sekta binafsi ili zishiriki kuujenga na Serikali ishughulikie uwezeshaji wa awali.



Lukuvi, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa takriban miaka mitano kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka jana na kubakizwa wizara hiyo na Rais John Magufuli, alitoa siri hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita.



Mbunge huyo wa miaka mingi wa Isimani mkoani Iringa alisema amegundua kuna mtandao mkubwa wa rushwa unaoanzia ngazi ya halmashauri mpaka wizarani ambao unahusisha maofisa wa Serikali na viongozi wa wizara.



Waziri Lukuvi alisema mtandao huo ni hatari na unaweza kusababisha mtu ashindwe kufanya kazi ya wananchi iwapo ataendekeza rushwa.



“Hapa (Wizara ya Ardhi) fedha ipo,”alisema Lukuvi ambaye amekuwa mbunge wa Isimani tangu mwaka 1995.



“Kama ukiwa na tamaa huwezi fanya kazi uliyotumwa. Kuna wakati walikuja wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka wanipe Sh5 bilioni ili nikubali kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi na walitangaza kwa marafiki zangu kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi” alisema Lukuvi.



“Wakati naingia tu wizara hii, nilikuta harakati za kukamilisha mradi wa Kigamboni ukiwa katika hatua za mwisho na kila kitu kilikuwa kimekamilika. Lakini nilipopitia vizuri, nilikataa kuwalipa wafanyabiashara hao. Cha ajabu hazikupita siku mbili wafanyabiashara hao walipata taarifa wakaja mbio kutaka kuniona.”



Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, wafanyabiashara hao walitaka walipwe kiasi cha Sh141 milioni kwa kila ekari wakati wao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa Sh5 milioni kwa ekari, jambo ambalo alisema lilishapitishwa awali.



“Niligundua pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue kutoka kwa wananchi ekari moja kwa Sh5 milioni, kisha Serikali tumlipe Sh141 milioni kwa ekari kwa kuvuka pantoni tu. Ni wizi mkubwa. Kama kweli Serikali ina fedha hizo kwa nini tusimlipe mwananchi moja kwa moja?” alihoji.



Waziri Lukuvi alisema endapo njama hizo zingefanikiwa, Serikali ingetumia zaidi ya Sh84 bilioni kuwalipa wawekezaji hao hewa kwa kuwa mmoja anamiliki takribani ekari 200 na mwingine 400.



“Niliwaambia Serikali haiwezi kuwalipa fedha hizo na badala yake waende kuiendeleza ardhi wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kutajirika kwa ujanja ujanja,” alisema Lukuvi.



“Eti walidai wamekopa benki kwa ajili ya mradi huo. Haiingii akilini mtu utumie Sh5 milioni, halafu uje uvune mabilioni ya fedha kwa kuvuka pantoni tu.”



Hata hivyo, Lukuvi alikataa kutaja majina ya wafanyabiashara hao.



Akiongea na gazeti moja la kila wiki mwaka 2013, Profesa Anna Tibaijuka, waziri aliyemtangulia Lukuvi kwenye wizara hiyo, alisema tayari kampuni mbili za Miworld kutoka Dubai na China Hope (China) zilishasaini mkataba wa maridhiano na Serikali wa kujenga nyumba takriban 20,900 kwenye eneo hilo.



Miworld ilisaini mkataba wa kujenga nyumba 5,000 wakati China Hope ilitaka kujenga nyumba 15,900 kwenye eneo hilo la mradi wa mji mpya.



Profesa Tibaijuka aliliambia gazeti hilo wakati huo kuwa wananchi wangefidiwa kwa bei za soko kwa mujibu wa sheria, akisema ekari moja ingefidiwa Sh141 milioni kwa ajili ya kumuwezesha kulipia gharama ya nyumba mpya mbadala.



Akizungumzia migogoro ya ardhi, Waziri Lukuvi alisema amegundua mingi inasababishwa na maofisa na viongozi wa wizara hiyo wasio waaminifu, lakini pia wawekezaji wenye tamaa ya kumiliki kiasi kikubwa cha ardhi hata kama hawana shughuli nayo.



“Nimegundua kuna watu hapa wanataka kumiliki ardhi kila sehemu. (Mtu huyo) Atafanya kila njia ashirikiane na watumishi wasio waaminifu ili wampatie eneo hata kama limeshauzwa,” aliongeza.



Lukuvi alisema wengi wao ni wafanyabiashara wenye asili ya Kiarabu na Asia ambao kwa muda aliokaa wizarani hapo amegundua wamehodhi  mashamba katika miradi yote ya viwanja au mashamba iwe ya halmashauri au wizara.



“Wanasiasa na viongozi wa Serikali wanaohodhi maeneo wapo, lakini siyo wengi ukilinganisha na hawa wafanyabiashara wengi wenye tamaa ambao wakishapata ardhi wanatumia kukopa mabilioni ya fedha ndani na nje ya nchi kisha wanawekeza katika miradi yao mingine ikiwamo kujenga majumba katika nchi za Dubai na Ulaya na kuyatelekeza maeneo hayo kuwa mapori hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi wasio na maeneo."



Akizungumzia matarajio yake, Waziri Lukuvi alisema endapo Rais John Magufuli ataendelea kumuweka katika wizara hiyo anatamani amalize migogoro yote baina ya wananchi katika kipindi cha miaka mitano


Chanzo:  Mwananchi

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top