SERIKALI ya Rais John Magufuli imeanza kuhujumiwa, wanaotajwa kuihujumu ni wafanyabiashara.
Wafanyabiashara wa sukari nchini wameanza kujenga utaratibu wa kuficha
sukari ili kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi lengo likiwa ni
kushinikiza vibabali vya kuingiza sukari kutoka nje vinatolewa.
Hatua hiyo imemwibua Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda na Biashara
ambaye anakiri kuwepo kwa hujuma hizo na kudai, serikali haitalala.
Amesema, kuna wafanyabiashara wanaficha sukari kwenye maghala yao ili
kuchochea mfumko wa bei na kisha waiuze kwa bei ya juu na hatimaye
kupata faida kubwa.
Hivi karibuni Rais Magufuli alizuia kutolewa vibali holela vya uingizaji
sukari nchini na kumwagiza Kasim Majaliwa, Waziri Mkuu kusimamia hilo.
Taarifa zilizopatikana zinaeleza kwamba, wafanyabiashara waliokuwa
wananufaika na uingizaji wa sukari nchini wameanza kuhujumu kwa
kushirikiana na wenye maghala ya sukari.
Mwijage amesema, wafanyabiashara hao wamekuwa wakificha sukari ghalani
ikiwa pamoja na kufungia maghala yao ili kuzuia mfumuko wa bei na
hatimaye kupata faida kubwa.
Amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es
Salaam ambapo amewataka wananchi kutoa taarifa sahihi za baadhi ya watu
wanaoendelea kuficha sukari kwa makusudi.
“Kama kuna taarifa sahihi za baadhi ya watu wanaoficha sukari ghalani
kwa makusudi ili kuiaminisha jamii kuwa sukari ya ndani haikidhi na
kupandisha bei holela ya sukari kwa masilahi yao binafsi muwataje,”
alisema Mwijage.
Mwijage alisema kuwa, kwa dhamana aliyokuwa nayo katika Sekta ya Viwanda
na Biashara anauwezo wa kufungia maghala yatakayobainika kuficha sukari
kwa makusudi.
“Niwahakikishieni kuwa hakuna mfumuko wa bei ya sukari, mambo ni mazuri
na utaratibu uko vizuri, niwasihi wawekezaji wa ndani wajitokeze
kuwekeza katika viwanda vya sukari ili kuiendeleza nchi yetu,” alisema.
Alisema, Serikali inampango wa kujenga viwanda vya sukari vidogo na
vikubwa ikiwemo ujenzi wa kiwanda kikubwa cha sukari kinachotarajiwa
kujengwa hivi karibuni katika mkoa wa Kigoma.
Post a Comment