Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametaka magazeti ya
Serikali kumsaidia Rais John Magufuli, kutumbua majipu kwa kuibua uozo
serikalini.
Akizungumza
katika kikao cha wafanyakazi wa Kampuni ya Tanzania Standard
(Newspapers) Ltd Dar es Salaam jana, inayochapisha magazeti ya Daily
News, HabariLeo na Spotileo, Nape ametaka magazeti hayo yasimung’unye
maneno kwa kuandika ukweli; kwenye nyeusi yaandike nyeusi na kwenye
nyeupe, yaandike nyeupe.
Alisema
vyombo vya habari vya Serikali vina wajibu wa kumsaidia Rais kutumbua
majipu kwa kuandika habari bila woga, upendeleo wala kuomuonea mtu, ili
kama kuna dosari ziko mahali ziibuliwe kwa lengo la kupata suluhu.
“Unajua
vyombo vya habari vinaaminika na vinasomwa na wengi na hasa wananchi
wanapotaka ukweli wa jambo, wanaangalia kama limeandikwa, sasa kama
jambo litaandikwa kwa kufichwa fichwa haitaisaidia Serikali, kama ni
nyeusi sema nyeusi, kama ni nyeupe sema nyeupe na hiyo ndiyo suluhu,” alisisitiza Nape.
Alisema
majipu yanayoendelea kutumbuliwa na Rais, mengine yanaibuliwa na vyombo
vya habari na ili kumsaidia na kusaidia Taifa, vyombo vya habari vya
Serikali lazima viibue hayo, pia viaminiwe mpaka na watumishi wa
Serikali, wavitumie kuibua uozo.
Nape
alisisitiza kwamba kuficha ukweli kwenye jambo ovu, ni kuendelea
kuharibu hivyo kuibuliwa kwa maovu kutaisaidia Serikali na watendaji
wake kuchukua hatua madhubuti.
“Kuna
hili jambo la baadhi ya watendaji kusema mfumo hautaki hili, hakuna cha
mfumo ni maneno yao wanayatumia kama kichaka cha kufanya uchafu,” alisema Nape.
Nape
alitoa onyo kwa watendaji wa serikali kuacha tabia ya kuzuia habari
zisitoke kwa maslahi yao na kutaka wenye pingamizi ya kutoka kwa habari,
wawasiliane naye na si kuingilia chombo cha habari.
Post a Comment