HOTUBA
YA MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA PILI
WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TAREHE 5 FEBRUARI, 2016
I: UTANGULIZI
(a) Masuala ya Jumla
Mheshimiwa Naibu Spika,
1. Kwanza
nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutujalia afya njema na uwezo katika
kutenda yote yaliyo mema. Tumekuwepo hapa kwa takriban siku 11 katika
shughuli za Mkutano wa Pili wa Bunge lako Tukufu. Ni jambo la kumshukuru
Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya
leo.
2. Tumekutana
hapa tukiwa tumeshuhudia uundwaji wa Serikali unaoendelea ambapo
Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania amefanya uteuzi wa Baraza jipya la Mawaziri ambao ni
Waheshimiwa Wabunge wenzetu. Niruhusu nitumie nafasi hii ya awali
kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote ambao wameteuliwa kushika
nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Tano.
(b) Chaguzi Mbalimbali
Mheshimiwa Naibu Spika,
3. Katika
Mkutano huu, tumeweza kufanya Chaguzi za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti
wa Kamati za Kudumu za Bunge. Vilevile, tumefanya chaguzi za Wenyeviti
wa Bunge letu na Wajumbe wa kutuwakilisha katika Taasisi mbalimbali za
Kitaifa na Kimataifa. Kwa vile orodha ni ndefu, napenda nitumie nafasi
hii kuwapongeza kwa dhati kabisa na kwa ujumla wao wote waliogombea
nafasi hizo na kushinda. Ni matarajio yangu kwamba tutatumia nafasi hizo
vizuri katika kuleta ushirikiano, mshikamano na kufanya kazi pamoja
kama Wawakilishi wa Wananchi na kutekeleza majukumu yetu kama Wabunge
ndani ya Bunge hili.
(c) Maafa na Ajali
Mheshimiwa Naibu Spika,
4. Tarehe
27 Januari, 2016 wakati Bunge lako Tukufu likiendelea na Vikao,
Waheshimiwa Wabunge walipewa taarifa ya kusikitisha ya kuzama kwa Kivuko
cha Kilombero, ambapo katika tukio hilo watu walipoteza maisha na
wengine kujeruhiwa. Aidha, mali za abiria zimepotea. Wakati huo huo,
mvua zinazoendelea kunyesha nchini katika baadhi ya maeneo zimesababisha
mafuriko, vifo, uharibifu wa mali ikiwemo mazao na miundombinu. Katika
baadhi ya maeneo, mvua hizi zimesababisha njaa na athari nyingine kwa
jamii.
5. Pamoja
na maafa ya mvua na mafuriko, wapo wananchi waliofariki na wengine
kupata ulemavu katika ajali mbalimbali za vyombo vya usafiri. Nitumie
fursa hii kuwapa pole wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika
matukio yote hayo. Aidha, napenda kuwatakia afya njema wote waliopata
majeraha. Kwa wale wote waliopoteza maisha tunawaombea Roho zao zilale
mahali pema peponi - Amina.
6. Kuhusu
uharibifu wa miundombinu, tunazo taarifa za uharibifu mkubwa wa
Miundombinu katika maeneo kadhaa. Napenda kulihakikishia Bunge lako
Tukufu kwamba Serikali itafanya kila liwezekanalo kurekebisha miundo
mbinu ya barabara iliyoharibika. Tunatambua gharama kubwa inayohitajika,
lakini ni wajibu wetu kama Serikali kuhakikisha Wananchi wanapata
huduma muhimu hasa za mawasiliano kati ya eneo moja na jingine.
(d) Maswali
Mheshimiwa Naibu Spika,
7. Leo
tunahitimisha Mkutano wetu wa Pili wa Bunge tukiwa tumefanya shughuli
mbalimbali ndani ya Bunge letu. Katika Mkutano wetu, Waheshimiwa Wabunge
wamepata fursa ya kuuliza maswali ya kawaida na yale ya papo papo kwa
Mheshimiwa Waziri Mkuu. Jumla ya maswali115 ya msingi na 307 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.
(e) Mjadala wa Hotuba ya Rais
Mheshimiwa Naibu Spika,
8. Katika
Mkutano huu moja ya agenda iliyochukua nafasi kubwa ni Hoja ya Serikali
ya kujadili Hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Maufuli, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo tuliihitimisha vizuri na kwa
mafanikio makubwa. Kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kutekeleza yale
tuliyokusudia kama wajibu wetu. Napenda kuwapongeza tena Waheshimiwa
Wabunge wote kwa kushiriki katika mjadala wa Hotuba hiyo vizuri.
Nichukue tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba michango ya
Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa utekelezaji.
II: MPANGO WA TAIFA WA MAENDELEO
Mheshimiwa Naibu Spika,
9. Katika
Mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya kujadili na
kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na
Serikali katika mwaka wa Fedha 2016/2017. Vilevile, Bunge limejadili na
kutoa maoni na ushauri katika mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya
Serikali katika mwaka wa Fedha, 2016/2017. Kipekee, naomba nimshukuru
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango(Mb) na Naibu wake
Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa
Wizara za Kisekta kwa ufafanuzi mzuri walioutoa wakati wa kuhitimisha
hoja hii. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa
Wabunge wote kwa michango yao mizuri, maoni na ushauri ambao Serikali
itauzingatia katika kukamilisha maandalizi ya Mpango na Bajeti ya mwaka
2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika,
10. Naomba
nami uniruhusu nitoe maelezo mafupi ya msisitizo katika maeneo machache
yaliyopata michango mingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge waliochangia
hoja ya Serikali ya mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo.
Waheshimiwa Wabunge wengi wamesisitiza kuhusu umuhimu wa Serikali
kuongeza uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali na
kuimarisha udhibiti wa matumizi ya Serikali. Aidha, Waheshimiwa Wabunge
wameishauri pia Serikali kuweka kipaumbele cha ujenzi wa Reli mpya ya
Kati, kujenga uchumi wa Viwanda, kuanza na kusimamia ujenzi na Mitambo
ya kuchakata gesi asilia (LNG) na Kiwanda cha Mbolea Mkoani Lindi,
kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme Vijijini, ujenzi wa Bandari Mtwara,
kutatua changamoto zinazowakabili Wakulima na Wafugaji pamoja na
Wachimbaji Madini.
Vilevile,
kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji wa Miradi ya Sekta za Elimu,
Afya, Maji na huduma kwa wenye Ulemavu na pia kuzingatia utawala bora.
Serikali inatambua kuwa maeneo haya ni muhimu sana katika kujenga uchumi
imara na endelevu na pia kuondoa umasikini. Hivyo, itazingatia sana
ushauri huu mzuri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika,
11. Naomba
nitumie fursa hii kumpongoeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe
Magufuli kwa umahiri mkubwa na umakini aliouonesha ikiwa ni mwanzo mzuri
wa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano. Mheshimiwa Rais ameonesha kasi
kubwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia Watanzania katika kujenga
uchumi imara, unaokuwa na endelevu. Waheshimiwa Wabunge wengi
watakubaliana nami kwamba Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi chake
cha mwanzo cha siku 100, imeonesha dhahiri nia ya dhati ya kuhakikisha
kwamba makusanyo ya mapato yetu yanaongezeka. Jitihada hizo za kuongeza
makusanyo ya mapato ya Serikali zimefafanuliwa vizuri kwenye Hotuba ya
Waziri wa Fedha na Mipango. Serikali itaendelea na mikakati yake ya
kuongeza Mapato yake na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi. Ni matumaini
yangu kuwa Waheshimiwa Wabunge, Wafanyabiashara na Wananchi wote
wataunga mkono dhamira hiyo njema ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika,
12. Kuhusu
matumizi, tayari Serikali imeanza kuchukua hatua thabiti za kudhibiti
matumizi yasiyo na tija katika Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea
na Taasisi zote za Umma pamoja Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Lengo la hatua zinazochukuliwa ni kuhakikisha kwamba Serikali inasimamia
kwa umakini matumizi ya fedha za Umma ili zitumike ipasavyo kwa malengo
yaliyokusudiwa. Hatua hizi zitaimarishwa zaidi katika mwaka ujao wa
fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika,
13. Kama
nilivyoeleza awali hoja nyingi za msingi zilizotolewa na Waheshimiwa
Wabunge kuhusu Mpango wa Taifa, zimefafanuliwa vizuri na Waheshimiwa
Mawaziri wa Kisekta na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Naomba
niwaahidi kuwa tutazizingatia katika mchakato wa maandalizi ya Mpango na
Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, kwa kadri itakavyowezekana.
Waheshimiwa Wabunge watashirikishwa kikamilifu katika mchakato huo
kupitia Kamati mbalimbali za Bunge. Serikali itafarijika sana kupata
maoni na ushauri zaidi ili tuweze kuboresha mipango yetu ya muda mfupi
na muda mrefu.
III: SEKTA YA KILIMO
Uzalishaji wa Mazao ya Chakula 2014/2015 na Upatikaji wa Chakula 2015/2016
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Hali
ya chakula kwa mwaka 2015/2016 katika maeneo mengi ya nchi imeendelea
kuwa ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri yaliyopatikana msimu wa kilimo
wa 2014/2015. Takwimu za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi zinaonesha
kuwa albaki kutoka msimu uliopita nchi ilikuwa na ziada ya chakula licha
ya kuwepo kwa maeneo machache ambayo hayakuwa na chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
14. Kutokana
na uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2014/2015 kuwa Tani
milioni 15.5 na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2015/2016 kuwa Tani
milioni 12.9 hivyo nchi imejitosheleza kwa chakula kwa ziada ya Tani milioni 2.5 sawa na asilimia 120. Napenda kuwahakikishia Watanzania kuwa Serikali itaendelea kuhudumia maeneo yote yenye uhaba wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika,
15. Pamoja na Taifa kuwa na ziada ya asilimia 120 ya chakula, tathmini ya hali ya chakula nchini inaonesha kuwa kuna Halmashauri 69 katika mikoa 18 nchini yenye maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula. Maeneo hayo yapo katika Mikoa ya Dodoma,
Shinyanga, Lindi, Singida, Tabora, Arusha, Geita, Kilimanjaro, Manyara,
Mara, Tanga, Simiyu, Mwanza, Morogoro, Iringa, Njombe, Mtwara, na Pwani.
Mheshimiwa Naibu Spika,
16. Ili
kukabiliana na hali ya uhaba wa chakula katika maeneo hayo, Serikali
inaendelea kutoa chakula katika maeneo hayo ambapo jumla ya Tani 23,871.6 za chakula zilitengwa kwa ajili hiyo. Hadi kufikia tarehe 17 Januari, 2016, jumla ya Tani 11,860.8 zilikuwa
zimechukuliwa toka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenda
kwenye Halmashauri za Wilaya zenye upungufu wa chakula kwa ajili ya
usambazaji. Natoa wito kwa Halmashauri ambazo hazijachukua mgao wao
kufanya hivyo mara moja ili Wananchi katika maeneo hayo wasizidi
kuathirika.
Mheshimiwa Naibu Spika,
17. Sambamba
na utoaji wa chakula cha msaada, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kutoa mahindi katika maghala ya
Songea na Sumbawanga kwa ajili ya kuuzwa kwa wafanyabishara wa nafaka
walioidhinishwa na mikoa yenye uhaba wa Chakula. Lengo ni kuongeza
upatikanaji wa chakula na kukabiliana na kasi ya kupanda kwa bei ya
vyakula katika maeneo hayo. Chini ya utaratibu huo, vibali vimeshatolewa
kwa wafanyabiashara wa Mikoa 17, vya kununua jumla ya Tani 77,166. Hadi kufikia tarehe 18 Januari, 2016 jumla ya Tani 56,817.5 kati ya Tani 64,817.3 zilizokuwa zimelipiwa kutoka NFRA tayari zilikuwa zimechukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
18. Ili kuongeza na kuimarisha uhakika na usalama wa chakula hapa nchini, Serikali imelenga kujenga maghala 275kwa awamu katika sehemu zenye uzalishaji mkubwa wa zao la mahindi ambapo hadi sasa jumla ya maghala 125yanaendelea
kujengwa na kukarabatiwa katika maeneo hayo. Aidha, Serikali kwa
kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) inaendelea kujenga
maghala ya kimkakati kwa ajili ya kuhifadhi akiba ya Taifa. Kwa sasa
ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi Tani 5,000 limeshajengwa
Wilayani Mbozi Mkoani Mbeya. Aidha, Serikali imepata mkopo wenye
masharti nafuu kutoka Serikali ya Poland ambao utawezesha kujenga
vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 160,000 na maghala yenye uwezo wa kuhifadhi Tani 90,000.
Mheshimiwa Naibu Spika,
19. Pamoja
na hatua zinazochukuliwa na Serikali, ninawataka viongozi wa Mikoa,
Wilaya na atendaji katika Halmashauri zote Nchini kuwahamasisha Wananchi
kutumia vizuri mvua zinazonyesha nchini kote kulima kwa bidii ili
kuweza kuvuna na kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha kwa ajili ya
kaya zao wakati wote wa mwaka. Aidha, wawahamasishe wafanyabiashara na
wadau wengine kusaidia Serikali kuchukua chakula kutoka maeneo yenye
ziada na kupeleka katika maeneo yenye upungufu. Ni imani yangu kwamba
tukizingatia maelekezo haya pamoja na juhudi za Serikali zilizooneshwa,
tatizo la uhaba wa chakula nchini litapungua, kama siyo kumalizika
kabisa.
IV: MIFUGO:
Hatua zilizochukulwa na Serikali katika Kushughulikia Migogoro ya Wakulima na Wafugaji;
Mheshimiwa Naibu Spika,
20. Migogoro
ya ardhi hapa nchini ina sura nne; migogoro kati ya Wakulima na
Wafugaji, mgogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji; migogoro kati ya
Wananchi na Serikali na migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka
nyingine ndani ya Serikali. Migogoro hii imeenea nchi nzima kutokana na
sababu mbalimbali ikiwepo kuongezeka kwa matumizi ya rasilimali ya
ardhi.
21. Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kwa kutumia Sheria ya Ardhi ya Vijiji Na. 5 ya mwaka 1999 na Sheria ya matumizi ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, hadi kufikia mwezi Juni 2015 jumla ya Vijiji 620 katika Wilaya 81 kwenye Mikoa 22 zimeweza kutenga Hekta Milioni 1.9 kwa
ajili ya Wafugaji. Wito wangu kwa Wananchi na Wadau wa Kilimo na
Ufugaji nawaomba kutunza na kuendeleza maeneo haya ili yaweze kutumika
kwa mujibu wa malengo yaliyopangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
22. Nitumie
fursa hii pia kulijulisha Bunge lako Tukufu kuhusu hatua ambazo
Serikali imechukua kukabiliana na migogoro ya Wakulima na Wafugaji
iliyotokea katika Mikoa ya Morogoro (Wilaya za Mvomero na Kilombero) na
Manyara (Wilaya ya Kiteto). Katika kushughulikia tatizo hili, Jumla ya
Vijiji 53 vimeainisha maeneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali
ikiwemo Kilimo na Ufugaji. Aidha, jumla ya Mashamba Pori Manane (8)
yameanishwa na orodha yake imewasilishwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa hatua za kufutiwa hati miliki na hatimaye
kufanya utaratibu wa kuyatumia kwa ufugaji. Ni matarajio yangu kuwa
maeneo haya yatapunguza sana kwa kiasi kikubwa matatizo ya uhaba wa
malisho hapa Nchini. Wito wangu niwatake Viongozi wa Vijiji kusimamia
vizuri matumizi ya maeneo yatakayotolewa kwa ajili ya malisho ili tatizo
hili la kukosa maeneo ya malisho lisijirudie tena.
Mheshimiwa Naibu Spika,
23. Bado kuna mgogoro wa Wafugaji na Wakulima katika Bonde Oevu la Kilombero ambao umetafutiwa ufumbuzi kwa kuweka alama (branding) mifugo yote katika eneo hili ambapo jumla ya Mifugo 52,780 ilipata usajili wa Wilaya. Aidha, jumla ya Mifugo 24,586 imeondolewa
katika eneo la Bonde la Kilombero. Kwa kuzingatia hatua zilizochukuliwa
na Serikali Wananchi wanapaswa kufuata Sheria na kuhakikisha Mifugo
hairudi tena katika maeneo yaliyokatazwa na kwamba maeneo haya
yanahifadhiwa kwa mujibu wa Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika,
24. Mgogoro
wa Wafugaji na Wakulima katika maeneo ya Kiteto ni wa muda mrefu na kwa
bahati mbaya sana umeleta madhara makubwa kwa maisha ya Wanadamu na
uharibifu wa mali. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Tume
iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu (Mstaafu) Mheshimiwa Mizengo Peter
Pinda ikiongozwa na Askofu Amos Mhagachi imekamilisha hatua muhimu ya
kuleta maelewanao na maridhiano katika pande zilizoathirika na mgogoro
huo. Kwa sasa hali imeendelea kuimarika na tunaendelea kufuatilia
kuhakikisha inakuwa shwari kwa muda wote.
25. Vilevile
tarehe 29 Januari 2016 nimekutana na Viongozi wa Serikali, Halmashauri
ya Wilaya na Chama kutoka Wilaya ya Kiteto hapa Dodoma ambapo nilipata
fursa ya kupokea taarifa ya Tume niliyoitaja hivi punde. Nimeiagiza Tume
kuendelea na hatua iliyobakia ili kurejesha utulivu na amani kwa
wananchi wa Kiteto. Hata hivyo, nimepanga kufanya ziara Wilayani Kiteto
katika siku chanche zijazo ili niweze kukutana na Wananchi walioathirika
na mgogoro huu na ikiwa ni pamoja na kujionea hali halisi Wilayani
Kiteto ili tuweze kutatua migogoro yote. Wito wangu kwa ndugu zangu wa
Kiteto ni kuwaomba waendelee kuvumilia wakati jitihada za Serikali
katika kutatua migogoro hiyo inaendelea.
V: UTEKELEZAJI WA ELIMU MSINGI BILA MALIPO
Mheshimiwa Naibu Spika,
26. Tangu
Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli atoe maaelezo ya utekelezaji
wa elimu ya msingi bila malipo, kumekuwa na umuhimu wa kutoa elimu na
ufafanuzi zaidi juu ya utekelezaji wa agizo la elemu bila malipo kwa
Watanzania kuanzia darasa la awali hadi Kidato cha Nne katika Shule za
Umma. Hii ni hatua ya Serikali katika kuhakikisha uwepo wa fursa ya
elimu bora kwa wote kwa kuwapunguzia mzigo wazazi na walezi kugharamia
au kuchangia upatikanaji wa elimumsingi.
Katika
mpango huu, Serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa mwanafunzi atasoma
kuanzia darasa la awali hadi kidato cha Nne bila ya wazazi na walezi
kulipa ada ya shule, gharama za mitihani na michango mbalimbali. Hata
hivyo, yapo majukumu ambayo yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi
wote ambayo ni pamoja na kununua sare za shule na michezo, madaftari,
kalamu na chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa zilizojiwekea
utaratibu huo. Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na kurudi
shule, na mahitaji mengine kama kununua godoro, shuka na vifaa vya usafi
binafsi. Mzazi au mlezi anao wajibu wa kugharamia matibabu ya mtoto
wake.
Mheshimiwa Naibu Spika,
27. Napenda
nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane
katika juhudi za kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila
malipo. Aidha, nawaomba wote kwa ujumla wetu kushirikiana kuwaelimisha
Wananchi wetu kuhusu utaratibu huu na wajibu wa kila mmoja wetu kama
Mzazi/Mlezi, Serikali na jamii kuhusu utekelezaji wa zoezi hili. Nia
yetu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata fursa ya kupata elimu
bora kwa mtoto mwenye umri wa kwenda Shule na wote walioko katika Shule
za Msingi na Sekondari. Napenda pia kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba
kama tulivyokwisha sema suala la ada elekezi inafanyiwa kazi na
ikikamilika Wananchi watajulishwa kuhusu utaratibu huo. Vikao vya pamoja
baina ya Serikali na wadau vitaanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika;
28. Katika kutekeleza mpango huu, Serikali imetenga fedha shilingi Bilioni 131.4 kuanzia
mwezi Disemba 2015 hadi Juni, 2016, kuhudumia wanafunzi wa bweni kwa
chakula, kufidia gharama za ada za mitihani, ada ya shule na kutoa fedha
za uendeshaji wa shule (Capitation Grants). Aidha, kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015, Serikaliimefuta michango yote iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa idhini ya Kamati na Bodi za Shule.
Mheshimiwa Naibu Spika,
29. Tunatambua
katika utekelezaji wa zoezi hili zipo changamoto zilizojitokeza. Kwa
mfano, baadhi ya shule zenye wanafunzi wachache kupata fedha kidogo sana
kwa kuwa ugawaji wa fedha unazingatia idadi ya wanafunzi. Lakini pia
zipo changamoto katika kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa
na uendeshaji wa Hosteli ambazo wazazi na walezi au jamii walikuwa
wanachangia fedha za chakula. Serikali inaendelea kuzifanyia kazi
changamoto hizo zilizojitokeza katika utekelezaji wa mpango huu ikiwemo
uelewa wa jamii na wadau kuhusu mpango mzima kwa ujumla wake.
VI: HUDUMA YA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Mheshimiwa Naibu Spika,
30. Serikali
imeendelea kutoa huduma ya mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa
mwaka wa masomo 2015/2016 kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu Namba 9 ya mwaka 2004 (Kama ilivyorekebishwa),
Kanuni za Utoaji Mikopo za mwaka 2008, na Mwongozo wa utoaji Mikopo na
Ruzuku kwa mwaka wa masomo 2015/2016. Hadi kufikia mwishoni mwa Januari
2016, Serikali ilikuwa imetoa mikopo yenye thamani ya ShilingiBilioni 207.9 kwa wanafunzi 122,786 wa elimu ya juu, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa kwanza 53,850 ambao ni asilimia 98.9 ya wanafunzi 55,254 walioomba mikopo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
31. Ili
Taifa liendelee kuwa na wataalamu wa kutosha katika nyanja muhimu,
Serikali itaendelea kutoa kipaumbele cha kutoa mikopo kwa wanafunzi wa
elimu ya juu wanaodahiliwa katika programu za kipaumbele ikiwemo Sayansi
za Tiba, Ualimu wa Sayansi na Hesabu, Uhandisi wa Mafuta na Gesi,
Uhandisi Umwagiliaji, Sayansi za Kilimo, Wanyama na Ardhi. Aidha,
Serikali inaendelea kufanyia kazi mikakati ya kuimarisha urejeshaji wa
mikopo pamoja na kuwa na vyanzo endelevu vya kupata fedha za kumudu
ongezeko la wanafunzi wenye mahitaji ya mikopo.
VII: HALI YA USALAMA NCHINI
Mheshimiwa Naibu Spika,
32. Hali
ya usalama katika Nchi yetu kwa ujumla ni shwari. Hata hivyo,
katika kipindi hiki nchi yetu imekuwa ikikabiliana na changamoto ya
ongezeko kubwa la Wakimbizi hususan katika Mkoa wa Kigoma. Kambi zetu
zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi
wapatao 218,895 kutoka mataifa ya Burundi (wakimbizi 156,377), Congo-DRC (wakimbizi 62,176), Somalia (wakimbizi 150) na Mataifa Mchanganyiko (wakimbizi192) kutoka nchi za Rwanda, Uganda, Sudan ya Kusini na Ethiopia. Kwa ujumla, katika kipindi hiki wamepokelewa wakimbizi zaidi ya 122,267 kutoka Burundi. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2015 kambi mpya ya wakimbizi ya Nduta imepokea wakimbizi 38,994 wengi kati yao wamehamishiwa kutoka Kambi ya Nyarugusu na wachache wakiwa wameingia moja kwa moja kutokea Burundi.
Mheshimiwa Naibu Spika,
33. Kufuatia
ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi toka Burundi kumejitokeza matukio ya
uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya
Nyarugusu. Aidha, kutokana na upekuzi na ukaguzi kwa wakimbizi
unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na taarifa za
ki-intelijensia imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia pamoja na
raia wa kawaida ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili
kujiunga na vikundi vya waasi. Nitoe wito kwa wananchi na wakimbizi
kushirikiana na vyombo vyetu vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu,
hususan umiliki haramu wa silaha za moto kwenye makambi na katika maeneo
mbalimbali.
VIII: MPANGO ENDELEVU WA USAFI WA MAZINGIRA NCHNI
Mheshimiwa Naibu Spika,
34. Mtakumbuka
kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliamua maadhimisho ya
miaka 54 ya Uhuru ya terehe 9 Desemba, 2015 yafanyike kwa kufanya usafi
wa mazingira katika maeneo ya Umma na maeneo yanayowazunguka. Kwa ujumla
Wananchi, Taasisi za Umma na Binafsi ziliitikia agizo hilo na kushiriki
kikamilifu katika zoezi hilo. Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa dhati
wananchi, taasisi za umma na binafsi wote kwa kushiriki katika zoezi
hilo kikamilifu. Mlionesha moyo wa uzalendo na ari kwa nchi yenu. Nawapongeza sana!
Mheshimiwa Naibu Spika,
35. Usafi
ni dhana muhimu katika kulinda afya za binadamu na kudhibiti magonjwa
mbalimbali ya mlipuko ikiwemo kipindupindu. Ili kufanikisha lengo hili,
kunahitajika juhudi za makusudi na za pamoja katika usimamizi wa sheria,
kanuni na taratibu tulizojiwekea. Hivyo, Serikali imeamua kulifanya
zoezi la usafi wa mazingira kuwa endelevu. Kupitia Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Serikali imetoa Waraka unaoelekeza kuwa kila Jumamosi ya
mwisho wa mwezi iwe Siku Maalum ya kufanya Usafi wa Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika,
36. Napenda
kuendelea kusisitiza katika kila ngazi yaani Viongozi na Wananchi
kutimiza wajibu wao kwa kuhakikisha zoezi hili linakuwa endelevu. Aidha,
napenda kuwahimiza Viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kusimamia
usafi wa mazingira katika maeneo yao ya utawala zoezi ambalo litakuwa
linafanyika kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi. Kila Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya nchini awe na mikakati ya kudumu ya usafi ikiwa ni
pamoja kuhakikisha kuwa kuna sheria ndogo za usafi wa mazingira na
zinatekelezwa ipasavyo. Aidha, Halmashauri zote nchini zihakikishe kuwa
uchafu uliokusanywa katika maeneo mbalimbali unazolewa na kupelekwa
katika maeneo mahususi ya dampo. Simamieni kikamilifu wakandarasi
waliopewa zabuni hizo na kuona wanatimiza wajibu wao kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
37. Kama
tulivyoona Usafi wa mazingira ni jukumu la kila Mwananchi na linapaswa
kuwa endelevu. Rai yangu kwa Watanzania wote ni kujenga tabia ya
kuhakikisha kuwa mahali pa kazi na mazingira yanayowazunguka yanakuwa
safi wakati wote. Kufanya hivyo, kutasaidia kuimarisha usafi wa
mazingira na kuboresha afya. Hali kadhalika kupunguza mlipuko wa
magonjwa yakiwemo kipindupindu.
38. Wito
wangu kwa Wananchi ni kuona kuwa zoezi la usafi ni la kila mmoja wetu
na kuepuka kuchafua mazingira kwa makusudi ikiwemo kuepuka tabia za
kutupa taka hovyo wanapokuwa katika vyombo vya usafiri na pia kutofanya
biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa ili kuzuia kutupwa taka hovyo.
Wamiliki wa mabasi yanayofanya safari ndefu wanatakiwa waweke vifaa vya
takataka. Yeyote atakayebainika kutupa takataka dirishani, atachukuliwa
hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na mmiliki wa basi hilo.
Watendaji wa
Mitaa na Kata na Vijiji kutimiza wajibu wao wa kuhakikisha maeneo
wanayoyasimamia yanakuwa katika hali ya usafi. Nitumie fursa hii
kuwahimiza Wananchi, Taasisi na Jumuiya zote kuhakikisha wanaweka
mazingira katika hali ya usafi na pia kushiriki katika siku ya usafi
kama iliyopangwa na Serikali.
IX: UHUSIANO WA KIMATAIFA
Mheshimiwa Naibu Spika,
39. Nchi
yetu imeendelea kuwa kivutio kikubwa katika mahusiano baina ya Nchi na
Nchi, Jumuiya za Kikanda na Kimataifa. Hii inatokana na Viongozi wetu
ambao wamekuwa katika mstari wa mbele kudumisha mahusiano yetu katika
Medani za Kimataifa. Yapo mambo mengi yaliyofanyika na yanayo endelea
kufanyika kama mwendelezo wa kudumisha ushirikiano katika Jumuia hizi za
Kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika,
40. Kutokana na juhudi za Viongozi wetu kutangaza Nchi yetu Kimataifa, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Bwana Ban Ki-moon kuwa mmoja wa Wenyeviti wa jopo la ushauri la
ngazi ya juu kuhusu Afya ya Mama na Mtoto Duniani (Every Woman, Every Child).
Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu kwa kuwa itaiweka Tanzania kuwa
miongoni mwa mataifa yenye kuheshimika duniani. Aidha, uteuzi huu ni
chachu ambayo inaleta matumaini mapya katika kukabiliana na changamoto
za afya ya mama na mtoto, hususan katika nchi zinazoendelea kama
Tanzania. Nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete kwa uteuzi huo. Tunamuombea heri na baraka tele katika
kutekeleza jukumu hilo kubwa la Kimataifa kwa maendeleo ya watu wetu.
X: KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI NA MAADILI
Mheshimiwa Naibu Spika,
41. Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi imedhamiria
kurejesha nidhamu na maadili ya Watendaji wa Serikali na Watumishi wa
Umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi kwenye maeneo
mbalimbali. Katika kuhakikisha Watumishi wa Umma na Watanzania wote
wanafanya kazi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania amekuja na kauli mbiu ya “Hapa Kazi Tu”. Tafsiri
ya falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali
walizopo kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe,
urasimu na kutenda kazi kwa mazoea.
42. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 chini ya Ibara ya 22 inaainisha kuwa, kilaMtu anayo haki ya kufanya kazi. Vilevile, Ibara ya 25 inafafanua
kuwa kufanya kazi ndiyo njia pekee ya kumwezesha Mtanzania kupata
utajiri na ndilo chimbuko la ustawi wa wananchi na ni kipimo cha utu.
Wakati
akihutubia Mkutano wa kwanza wa Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Magufuli, kwa maneno yake alisema, napenda kunukuu:-
“Serikali
nitakayounda, nataka iwe inawahudumia Wananchi kwa haraka na sio
kuwasumbua sumbua na kuwazungusha. Natoa rai kwa Watumishi wa Serikali,
hasa ambao ni wazembe na wavivu, kujiandaa. Wamevumiliwa kwa muda mrefu
sasa basi. Kwa sababu Watumishi wa aina hiyo hawatavumiliwa katika
Serikali nitakayoiongoza. Lugha za “Hiyo ni changamoto tutaishughulikia” au “Mchakato unaendelea”hazitavumiliwa katika Serikali ya Awamu ya Tano. Mimi nataka watu wa Kazi tu.
Hatuwezi kulea watu ambao wanalipwa mishahara lakini hawafanyi kazi
wanazotakiwa kufanya, au wamegeuza Ofisi za Umma kuwa ni mahala pa
kuchuma bila kufanya kazi.”mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
43. Ili kutekeleza
maneno ya Mheshimiwa Rais na kuhimiza matakwa ya Kikatiba, kila
Mtanzania anapaswa kushiriki na kujituma kwa uaminifu katika kazi halali
za uzalishaji mali. Aidha, kila Mwananchi anapaswa kuwa na nidhamu ya
kazi na kuhakikisha anafikia malengo yaliyowekwa. Nitumie fursa hii pia
kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuwa wamepewa dhamana ya kuwahudumia
Wananchi kwa niaba ya Serikali. Hivyo wanawajibika kuhakikisha
wanawahudumia Wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao. Ni
lazima wahakikishe kuwa wanatatua kero za Wananchi. Sio sahihi wananchi
kuwasilisha kero zao kwa viongozi wa ngazi za kitaifa hasa wakati wa
ziara ilhali viongozi wa mikoa na wilaya wapo katika maeneo hayo kwa
wakati wote.
44. Tunatambua kuwa
wapo Watumishi wanaotekeleza vyema majukumu yao. Lakini pia wapo
Watumishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao na pia wanafanya kazi
kwa uzembe. Serikali haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi
wote wasiozingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi
wa Umma. Aidha, kwa
kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Viongozi na Watumishi wote wa
Umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na kujiamini. Kila mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa anaitendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika,
45. Huu
sasa ni wakati wa kufanya mabadiliko ya dhati katika utendaji na
uadilifu. Kwa maana hiyo napenda kusisitiza mambo yafuatayo kwamba:-
(i) Kila
Kiongozi na Mamlaka ya nidhamu ni lazima kuwajibika kusimamia Utendaji
na Maadili ya Kazi. Hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa wakati na kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi. TUSIONE HAYA HATA
MARA MOJA, CHUKUENI HATUA.
(ii) Wananchi
wahudumiwe ipasavyo na kwa weledi, haki, uadilifu na heshima. Mambo
haya yakizingatiwa hakuna mwananchi atakayesafiri kutoka kijijini,
wilayani au mkoani kutafuta huduma Makao Makuu ya Wizara, Ofisi ya
Waziri Mkuu au IKULU.
(iii) Madawati
ya malalamiko yawepo katika Ofisi za Umma. Aidha, tayari maelekezo
yametolewa ya Watumishi wa Umma wazingatie utaratibu wa kuvaa
vitambulisho vyenye majina yao kwa urahisi wa wananchi kuwatambua
wanapowahudumia. AGIZO HILI LITEKELEZWE.
Mheshimiwa Naibu Spika,
46. Ni kweli kwamba, Mheshimiwa Rais ametumia dhana ya “kutumbua jipu” kama
dawa ya kusimamia uwajibikaji hasa katika wale wenye dalili ya kukosa
maadili ya Utumishi wa Umma. Tafsiri ya dhana hii ya “Kutumbua jipu”inalenga
katika kuwarejesha Watumishi wa Umma na walioko Serikalini katika
mstari mzuri wa utendaji. Nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kama
tulivyo na kwa umoja wetu, tumuunge mkono Mheshimiwa Rais katika vita
hii kubwa ya “Kutumbua Majipu”. Tukiwa pamoja na kwa
kushirikiana tutaweza kuibadilisha nchi yetu kuwa nchi ya maadili na
yenye sifa ya juu katika utendaji wa Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika,
47. Aidha,
naomba nisisitize kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Magufuli inaongozwa na Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu za
Nchi. Vilevile inaheshimu na kuthamini haki za Watumishi wa Umma wa
ngazi zote na inatambua mchango mkubwa unaotolewa na Watumishi wa Umma
katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa. Kamwe, Serikali haitamwonea
mtumishi yeyote wala kumnyanyasa endapo tu atakuwa anatenda yale
yanayopasa. Lakini pia haitamvumilia mtumishi mzembe na asiyetimiza
wajibu wake. Serikali itaendelea kuchukua hatua za kurejesha nidhamu kwa
Watumishi wa Umma ili kuwezesha Nchi yetu kuwa na Utumishi wenye
kuzingatia uadilifu na uliotukuka.
XI: HITIMISHO.
Mheshimiwa Naibu Spika,
48. Uzoefu
nilioupata katika muda mfupi tuliokaa pamoja hapa Bungeni, nimegundua
kuwa tuna Waheshimiwa Wabunge mahiri waliobobea katika nyanja
mbalimbali. Wapo wasomi wa ngazi zote, wazee kwa vijana ambao wana
uzoefu na utaalam mkubwa. Ni imani yangu kuwa tutatumia utaalam na uwezo
mkubwa tulionao katika kuijenga nchi yetu na kuwasaidia Watanzania
kutoka hapa tulipo hadi hatua ya mbele katika kuleta maendeleo. Wananchi
waliotuchagua wanatutegemea. Nawaomba tutangulize uzalendo katika kila
jambo tufanyalo kwa manufaa ya Taifa letu na watu wake. Tufike mahali
ambapo kwa elimu, busara na hekima tulizonazo kuacha kabisa ushabiki wa
kisiasa badala yake tutizame mbele katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika,
49. Napenda
kuhitimisha Hotuba yangu kwa kurejea tena nilivyosema hapo awali
kwamba, baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu kwa mafanikio makubwa,
kazi kubwa iliyo mbele yetu ni kuijenga nchi yetu kwa umoja na
mshikamano. Nawaomba tuweke maslahi ya Watanzania na Taifa letu mbele.
Tudumishe amani na utulivu. Tupuuze sera zozote za kudhoofisha utaifa
wetu kama Watanzania na kutugawa kwa misingi yoyote ile, iwe ya
kikabila, imani za dini, rangi au kwa itikadi za kisiasa. Dhamira yetu
sote iwe ni kukuza uchumi wa nchi yetu na kuondoa umaskini ili kuwaletea
wananchi wetu maendeleo na maisha mazuri.
50. Ni
jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa Tanzania inapiga hatua
mbele. Tufanye kazi kwa bidii kuunga mkono kaulimbiu yetu ya “Hapa ni Kazi Tu”.
Aidha tutumie juhudi, maarifa na ubunifu zaidi katika kila jambo. Mimi
naamini kuwa kwa ushirikiano katika Bunge hili na wananchi kwa ujumla,
tutaweza kutimiza matarajio ya wananchi waliotuchagua na matarajio ya
Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika,
51. Naomba
nitumie nafasi hii tena kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha
mkutano huu. Nikushukuru wewe Naibu Spika, na Mheshimiwa Spika kwa
kutuongoza vizuri na kwa weledi mkubwa. Kipekee niwashukuru Wenyeviti wa
Bunge ambao wamekalia kiti kwa mara ya kwanza lakini kwa weledi
mkubwa, Hongereni sana!!.
Mheshimiwa Naibu Spika,
52. Nitumie
nafasi hii kumshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote kwa kazi
nzuri ya kuhakikisha mkutano huu unakamilisha shughuli zake kama
ilivyopangwa. Niwashukuru Wataalam wote wakiwemo Waandishi wa Habari kwa
kazi nzuri waliyofanya kufanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa Naibu Spika,
53. Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu.Ninaamini kwamba, Mwenyezi Mungu atatulinda na kutuweka salama sote kama tulivyo hadi kukutana tena katika Mkutano ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika,
54. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 19 Aprili, 2016 saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa Tatu kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika,
55. Naomba kutoa Hoja.
Post a Comment