Mkuu
wa Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Nishati na Madini, Badra Masoud,
akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, wakati alipokuwa
akitoa ufafanuzi kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi Awamu ya Pili,
akielezea kuhusu habari zilizoandikwa kimakosa katika moja ya magazeti
ya kila siku nchini jijini leo. Kulia ni Ofisa Habari Mwandamizi wa
Idara ya Habari-Maelezo, Magreth Kinabo. (Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot. com)
Na Nyakongo Manyama- MAELEZO
14/01/2016
WIZARA ya Nishati na Madini imekanusha habari iliyopotosha umma kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi II kuwa bado haujaanza na gharama zilizoandikwa si za kweli.
Wizara hiyo imekanusha habari hiyo, iliyoandikwa katika gazeti la Mtanzania la jana Januari 14, mwaka huu toleo namba8063, lenye kichwa cha habari “ Harufu ya Jibu Mradi wa Umeme.”
Habari hiyo ambayo ilieleza kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais Mstaafu wa Serikali
ya Awamu ya Nne, Mhe. Dkt.Jakaya Kikwete uligharimu Sh. trilioni 1.6 na
kwamba fedha za ujenzi wa mradi huo zimetokana ubia kati ya Serikali ya
Tanzania na Japan,ambapo Serikali ya Tanzania itakuwa na hisa ya
asilimia 40 na kampuni ya SUMITOMO ya Japan asilimia 60.
Aidha
habari hiyo ilidai kuwa Serikali inachangia fedha za ndani kwa asilimia
12 na zilizobaki zikiwa na mkopo kutoka benki ya Japan na kwamba
gharama za mradi huo ziko juu ikilinganishwa miradi mingine akitolea
mfano Kampuni ya TALLAWARA Power Station ya nchini Australia anayodai
ilitaka kujenga mradi huo kwa dola za Marekani milioni 350.
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mawasiliano Serikali wa wizara hiyo, Badra Masoud alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu habari hiyo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dar es Salaam.
“Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Japan ya mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 292 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuzalisha
umeme wa Megawati 240 utakaojengwa na kampuni ya SUMITOMO kama
mkandarasi wa “EPC contractor” na sio kama mbia wa Serikali yaTanzania
kama ilivyodaiwa.
“Mradi huo unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia TANESCO na
hakuna mwekezaji mwingine katika mradi huo.Hivyo si kweli kwamba
Serikali ya Tanzania na kampuni ya SUMITOMO zinawekeza kwa ubia wa
asilimia 40 (kwa Serikali ya Tanzania) na asilimia 60 kwa SUMITOMO. Kwa
maana hiyo, hatutauziwa umeme utakaozalishwa na mradi huu kwani ni mali
yetu na hakuna gharama yoyote ya ziada kama alivyodai mwandishi wa
habari hiyo,” alisema Badra.
Aidha Badra alisema mwandishi huyo alidai kwamba mradi huo ulizinduliwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, wakati ni kwamba mradi huo haujazinduliwa bado na sasa upo katika maandalizi ya kuwekwa katika jiwe la msingi.
Akizungumzia
kuhusu gharama za mradi huo, alieleza kuwa unatekelezwa kwa dola za
Marekani milioni 344 sawa na Sh. bilioni 740 zikiwa ni mkopo wa masharti
nafuu wa asilimia 85 sawa na dola za Marekani 292 na
mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15 sawa na dola za Marekani
milioni 52 na sio asilimia 12 kama ilivyodaiwa na mwandishi huyo.
“Mwandishi
wa habari hii amejaribu kufananisha uwekezaji huu na uwekezaji wa
TALLAWARA Power Station ya Australia na kudai kwamba gharama yake
ingekuwa ndogo kuliko gharama ya mradi huu.
Taarifa
hii haina ukweli wowote kwa sababu gharama ya dola milioni 344
zinazotarajiwa kutumika mkatika mradi huu iko chini kuliko dola milioni
350anazodai mwandishi kwamba zingetumiwa na kampuni TALLAWARA.
“Aidha,
kampuni ya TALLAWARA haijawahi kuomba au kuonesha nia ya kuwekeza
katika mradi wowote wa kufua mradi wa umeme nchini. Pia ni muhimu
ifahamike kwamba makubaliano ya mkopo huu yalikuwa yanakwenda sambasamba
na utekelezaji wa mradi wenyewe (EPC with Financing).
Badra
aliongeza kwamba pamoja na kwamba gharama za uwekezaji wa mradi huo wa
kwanza wa aina ya “Combined Cycle” nchini zinawiana na gharama za miradi
mingine ya aina hiyo duniani, gharama za uwekezaji zinaweza kutofautiana kutegemeana na mazingira ya nchi na nchi, teknolojia iliyotumika na aina ya mitambo.
Hivyo sio suala la kulinganisha gharama ya mradi mmoja na mwingine.
Wizara hiyo imeshauri waandishi wa habari kufuata miiko na maadili ya uandishi wa habari kwa kuandika habari zenye ukweli na sahihi na zilizozingatia pande zote mbili kwa kuwa ipo na tayari kujibu maswali ya waandishi wakati wowote.
Post a Comment