Aliyekua mgombea Urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama
vinavyounda UKAWA Mh.Edward Lowassa amelalamikia baadhi ya watendaji wa
serikali kwa kuwaandama na kuwatisha wananchi na wafanyabiashara
waliokuwa wanaunga mkono vyama vya upinzani na amezitaka idara
zinazohusika kuchukua hatua ili kuepusha matatizo yasiyo ya lazima.
Akizungumza katika ibada maalum ya kukaribisha mwaka mpya
iliyofanyika katika kanisa la kilutheri wilayani Monduli Mh Lowassa
amesema amepokea malalamiko ya kuwepo kwa uonevu na vitisho kwa wadau
walioonekana kuunga mkono vyama vya upinzani licha ya kuwa ni haki yao
kikatiba.
Pia Mh Lowassa aliyekuwa mbunge wa jimbo la Monduli kwa
tiketi ya (CCM) kabla ya kuhamia Chadema na kuwa mgombea urais amesema
ataendelea kusaidiana na mbunge wa sasa Mh Julias Kalanga (Chadema)
kutatua kero za wananchi na kuhakikisha kuwa misingi aliyoijenga inakuwa
endelevu.
Kwa upande wao baadhi ya viongozi wa dini na wananchi
waliohudhuria ibada hiyo wamepongeza uvumilivu wa kisiasa ulioonyeshwa
na Mh Lowassa ambao umeendelea kuimarisha amani na utulivu nchini na
wamewaomba wanasiasa wengine kuiga mfano huo.
Post a Comment