TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tokea yalipofanyika Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, tumekuwa
tukiadhimisha tukio hilo kubwa katika historia ya Zanzibar kila mwaka
inapofika siku hiyo.
Tukio hilo kubwa ndilo lililopelekea kutangazwa kwa Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume.
Chama Cha Wananchi (CUF) kimekuwa kikishiriki kikamilifu katika
maadhimisho ya siku hiyo kila mwaka kwa kutambua kwamba Mapinduzi ya
tarehe 12 Januari, 1964 ni Mapinduzi ya Wazanzibari wote.
Malengo makuu ya Mapinduzi hayo yameelezwa na kufafanuliwa vyema kupitia
Dikrii Nam. 6 ya mwaka 1964 iliyopitishwa na Baraza la Mapinduzi ambayo
yanatajwa kwamba ni kuleta usawa, umoja na maridhiano baina ya
Wazanzibari wote na kupiga vita aina zote za ubaguzi.
Tayari tumetangaziwa kwamba kuanzia tarehe 2 Januari, 2016 kutakuwa na
shughuli mbali mbali zenye lengo la kuadhimisha Mapinduzi yetu na
hatimaye, kama ilivyo ada na desturi, kufikia kilele tarehe 12 Januari,
2016 katika sherehe ambazo zitafanyika Uwanja wa Amaan, mjini Zanzibar.
CUF kama chama cha siasa kinawatakia kheri Wazanzibari wote katika kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi yao.
Hata hivyo, tunatambua kwamba sherehe za mara hii zinafanyika wakati
ambapo nchi yetu na watu wake wema wamo katika mtihani mkubwa kufuatia
kitendo cha mtu mmoja, Jecha Salim Jecha, kuamua kwa utashi wake na
waliomtuma kuiingiza nchi yetu katika msukosuko na taharuki kwa kudai
kwamba eti ameufuta uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na matokeo
yake.
Kwa kitendo hicho cha mtu mmoja ambaye amevunja Katiba, amevunja Sheria
ya Uchaguzi na amevunja hata maadili ya kazi yake, mara hii nchi yetu
itaadhimisha Mapinduzi huku Serikali ikiwa inaongozwa na viongozi ambao
hawana uhalali na ridhaa ya wananchi.
CUF tumesisitiza mara zote kwamba hatukubaliani na uamuzi huo wa mtu
mmoja kujinyakulia mamlaka ya wananchi wa Zanzibar yaliyowekwa
kikatiba.
Kwa msingi huo huo, tunapenda kutumia fursa hii kuwaeleza wananchi wa
Zanzibar kwamba viongozi wetu hawatoshiriki katika shughuli
walizopangiwa katika ratiba ya sherehe hizi kwa sababu zifuatazo:
1. Kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (Toleo la 2010), Ibara
ya 28, Ibara ya 42(2), Ibara ya 48(b), Ibara ya 90(1) na Ibara ya 92(1)
Serikali iliyokuwepo madarakani na Baraza la Wawakilishi lililokuwepo
katika kipindi cha miaka mitano iliyopita (2010 – 2015) vilimaliza muda
wake wa uongozi tarehe 2 Novemba, 2015 kwa upande wa Serikali na tarehe
12 Novemba, 2015 kwa upande wa Baraza la Wawakilishi. Kwa sasa, hatuna
viongozi wenye uhalali wa kikatiba kuweza kutekeleza majukumu ya
kiserikali. Kwa hivyo, kushiriki katika ratiba hizo kwa kutumia nafasi
ambazo hazina uhalali tena wa kikatiba ni kwenda kinyume na dhamira ya
waasisi wa Mapinduzi, jambo ambalo hatuko tayari kulifanya.
2. Kiuataratibu, kilele cha sherehe huongozwa na Rais ambaye yupo
kikatiba. Kwa mara ya kwanza tokea tarehe 12 Januari 1964, sherehe za
miaka 52 zitaongozwa na Rais ambaye ameshamaliza muda wake wa uongozi
kikatiba na ambaye hana uhalali na ridhaa ya wananchi wa Zanzibar.
Kushiriki katika sherehe hizo ni kuhalalisha kipindi cha uongozi ambacho
hakipo tena kikatiba. Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wenziwe
ndani ya Chama waliokuweko Serikalini hadi tarehe 2 Novemba, 2015 hawako
tayari kuhalalisha uvunjaji wa Katiba ya Zanzibar ambayo ndiyo sheria
kuu ya nchi.
3. Viongozi wa CUF wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad wanaamini
katika msingi mkuu wa Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 chini ya
uongozi wa Baba wa Taifa la Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani
Karume, ambao ni kuleta utawala wenye ridhaa ya wananchi walio wengi.
Msingi huo umewekwa wazi na kutiliwa nguvu na Katiba ya Zanzibar ya 1984
(Toleo la 2010) kupitia Ibara ya 9(2)(a) ambapo inaelezwa kwamba,
“Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo
wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.”
Mamlaka hayo ya wananchi yalitekelezwa tarehe 25 Oktoba, 2015 kwa
kuwachagua viongozi watakaoongoza Serikali yao kwa miaka mitano ijayo.
Kitendo chochote cha kupindua mamlaka hayo ya wananchi ni kwenda
kinyume na misingi ya Mapinduzi na misingi iliyowekwa na Baba wa Taifa
la Zanzibar, Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume. CUF hatuko tayari
kushiriki katika kuisaliti misingi hiyo na kuisaliti dhamira ya Mzee
Karume.
4. Sherehe za kuadhimisha Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964 zina
lengo la kukumbuka malengo ya Mapinduzi hayo na dhamira ya waasisi wake
wakiongozwa na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika kusimamia
utawala wenye ridhaa ya wananchi walio wengi.
Kuzitumia sherehe za Mapinduzi kuhalalisha utawala usio na ridhaa ya
wananchi wa Zanzibar na ambao haupo kikatiba ni usaliti mkubwa wa
dhamira ya kuwepo kumbukumbu hiyo. CUF hatuko tayari kuwa sehemu ya
usaliti huo.
Kwa sababu hizo zilizoelezwa hapo juu, viongozi wa CUF hawatoshiriki
katika ratiba walizopangiwa mpaka pale chaguo la wananchi wa Zanzibar
walilolifanya tarehe 25 Oktoba, 2015 litakapoheshimiwa.
Tuweke wazi kwamba tulichoamua ni viongozi wetu kutoshiriki katika
ratiba zinazohusisha viongozi wa Serikali ambao wamemaliza muda wao wa
uongozi. Kwa hivyo, bado tunachukua nafasi hii kuwatakia wananchi wa
Zanzibar maadhimisho mema ya miaka 52 ya Mapinduzi na kuwataka
waendeleze umoja, mshikamano na amani katika nchi.
Mwisho kabisa, tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahala pema Peponi
muasisi wa Mapinduzi yetu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, na waasisi
wenzake wote na awasamehe makosa yao.
Tunawaomba Wazanzibari wote kila mmoja kwa dini yake wamuombe Mwenyezi
Mungu kuijaalia kheri na salama nchi yetu na kuyasimamisha yaliyo ya
haki. Tukiishika kamba ya Mwenyezi Mungu hatutoanguka.
Tunawatakia wote kheri ya mwaka mpya wa 2016 na tunaamini unakuja na
kheri kubwa kwa Zanzibar na watu wake. Ni mwaka ambao safari ya ujenzi
wa Zanzibar Mpya itaanza.
MAPINDUZI DAIMA!
HAKI SAWA KWA WOTE
MANSOOR YUSSUF HIMID
MSHAURI WA KATIBU MKUU – CUF
31 DESEMBA, 2015
Post a Comment