WATU saba wamefariki dunia na wengine kumi wamejeruhiwa katika ajali
ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka na kulipuka na kuwaka moto huko mkoani Kigoma.
Akiongea na mtandao huu ofisini kwake Mganga Mkuu wa hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni Dkt. Leonard Subi amesema kuwa jana majira ya saa 12 jioni walipokea miili ya marehemu 6 na majeruhi 11 ilipofika saa 6 usiku majeruhi mmoja alifariki duniana na kupelekea idadi ya vifo kuwa saba.
Aliwataja waliofariki katika ajali hiyo ni Ashura Mussa, Kadogo Yusuph, Kabwe Iddy, Mwamvua Juma na Peter Sungura,maremu wawili miili yao bado haijatambulika sababu ya kuungua vibaya.
Dkt. Subi aliwataja pia majeruhi wa ajali hiyo kuwa ni Andrew Peter, Amos Thomas, Mutta Hamis, Shabaan Fadhil, Hassan Kasa, Esau Elias, Asha Kassim na Riziki Jaah.
"Majeruhi wote wamelazwa wodi namba saba na hali zao siyo nzuri wanaendelea na matibabu, mtoto aitwaye Riziki Jaah mwenye umri wa miezi nane ndiye aliyenusurika katika ajali hiyo hajaumia popote mama yake alimtupa dirishani baada ya moto kuwaka ila mama yake alifariki kwa kuungua kwenye ajali hiyo"alisema Dkt. Subi.
Naye Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Kigoma, Ferdnand Mtui amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ya gari aina ya Toyota Hiace lenye namba T.700 ADK lililokuwa likitoka Kigoma mjini kwenda katika kijiji cha Subankala kata ya Ilagala Wilayani Uvinza kilichopo mwambao mwa ziwa Tanganyika.
Kamanda Mtui alisema kuwa ajali hiyo ilitokea katika kijiji cha Mwakizega na chanzo cha ajali hiyo ni dereva kuwakwepa watembea kwa miguu kisha kugonga gema iliyopelekea gari kupinduka na kuwaka moto.
Post a Comment