PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Mlinzi wa Mfalme wa Qatar Atiwa Mbaroni Moshi Kwa Tuhuma za Kusafirisha Fuvu la Twiga
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Jeshi la Polisi kupambana na ujangili, kimemtia mbaroni mlinzi wa mfalme wa Qatar, kwa tuhuma z...


Kikosi kazi maalumu kilichoundwa na Jeshi la Polisi kupambana na ujangili, kimemtia mbaroni mlinzi wa mfalme wa Qatar, kwa tuhuma za kusafirisha fuvu la twiga kwenda Uarabuni.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani jana alithibitisha kukamatwa kwa mlinzi huyo wa mfalme na kwamba utaratibu wa kumfikisha mahakamani ulikuwa ukifanyika.

“Ni kweli tuna mtu kama huyo tulimkamata pale (Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro) Kia, akapelekwa Arusha lakini amerudishwa Moshi na mchakato wa kumfikisha mahakamani hapa Moshi unaendelea,” alisema Ngonyani.

Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Idara ya Wanyamapori zimemtaja mlinzi huyo kuwa ni Jasim Mbarakke Alhkubaisi (43).

Mlinzi huyo amekamatwa wakati mtuhumiwa muhimu aliyepatikana na hatia ya kusafirisha wanyama hao wakiwamo twiga wanne kwenda jijini Doha, Qatar, Kamran Ahmed akiwa hajapatikana licha ya kushtakiwa na kuhukumiwa kifungo baada ya kupatikana na hatia.

Mlinzi huyo alikamatwa Kia, ambako Novemba 26, 2010 walipitishwa wanyamapori 152, wakiwamo twiga.

Taarifa zilizopatikana jana mjini Arusha na Kia, zilidokeza kuwa mlinzi huyo wa Mfalme wa Qatar alikamatwa na kikosi kazi hicho Desemba 18.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na fuvu la twiga, ambalo anatuhumiwa kuwa alitaka kulisafirisha kwenda Qatar kwa kutumia ndege ya Qatar Airways ya nchi hiyo.

“Hii issue (suala) ni nyeti. Kuna maofisa wa ubalozi wa Qatar walikuja hapa Arusha juzi na jana wakijaribu kufanya kila njia asishitakiwe lakini imeshindikana,” alidokeza afisa mmoja wa Uhamiaji.

Taarifa nyingine za uhakika zilisema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amelazwa katika hospitali moja jijini Arusha na polisi inaangalia uwezekano wa kulipeleka shtaka lake mahakamani ili asomewe shauri lake akiwa hospitalini.

Kukamatwa kwa mlinzi huyo, kumekuja wiki moja tangu Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, limtie mbaroni raia wa Vietnam, Hoang Nghia Trung (49), akiwa na kucha 261 na meno 60 ya simba.

Kamanda Ngonyani, alikaririwa akisema raia huyo wa Vietnam alikamatwa Desemba 14 saa 10 alasiri kwenye uwanja huo wa Kia.

Kwa mujibu wa Kamanda Ngonyani, mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya polisi wa uwanjani hapo kumtilia shaka na alipopekuliwa alikutwa na nyara hizo za Serikali.

Taarifa hizo zinadai kuwa wakati akikamatwa, kulitokea ubishani baada ya mlinzi huyo kujitetea kuwa alilichukua fuvu hilo kwa ajili ya utafiti, lakini akashindwa kufafanua ni utafiti gani.

Kwa mujibu wa vyanzo, mlinzi huyo alikuwa na hati mbili za kusafiria, moja ikiwa na hadhi ya kidiplomasia na nyingine ya kawaida lakini katika safari hiyo alitumia pasi ya kawaida.

Desemba 5, 2014, Kamran ambaye ni raia wa Pakistan, alihukumiwa kifungo cha miaka 60 jela baada ya kupatikana na makosa manne ya kusafirisha wanyamapori hao kwenda Arabuni bila kibali.

Mbali na kuhukumiwa kifungo hicho, pia Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa, Simon Kobero aliamuru kutaifishwa kwa mali zote za mtuhumiwa huyo zilizopo Tanzania.

Hata hivyo, hukumu hiyo ilitolewa bila ya mtuhumiwa kuwapo mahakamani kwa kuwa alitoroka nchini Februari 2014.

Twiga hao na wanyama wengine walitoroshwa kwenda Arabuni Novemba 26, 2010 kupitia Kia kwa kutumia ndege kubwa ya Jeshi la Qatar.

Wanyama waliotoroshwa kwenda Doha wenye thamani ya Dola 113,715 za Marekani (Sh170.5 milioni), walisafirishwa kwa kutumia maboksi marefu.  

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top