PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: Polisi ‘Yawatumbua Majipu’ Trafiki, yabadili Mfumo...Sasa Faini Kulipwa Kwa Mashine za EFD
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Jeshi la Polisi limefanya mabadiliko kadhaa katika Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuwahamisha baadhi ya askar...


Jeshi la Polisi limefanya mabadiliko kadhaa katika Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kuwahamisha baadhi ya askari wake huku wengine wakishushwa vyeo au kuachishwa kazi kutokana na makosa mbalimbali makubwa yakiwa malalamiko ya kuwaonea wananchi, rushwa na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wa barabara.

Kamanda wa kikosi hicho, Mohamed Mpinga akizungumza wiki iliyopita alisema ili kupunguza rushwa na kuingiza mapato, kikosi hicho kimeanzisha mfumo mpya wa kulipa faini wa kutumia mashine za EFD, ambao awali, ulifanywa kwa majaribio na kuonyesha mafanikio licha ya kasoro kadhaa zilizojitokeza.

Dar es Salaam

Wakati hatua hizo zikichukuliwa, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imeshawabadilisha kazi wakaguzi saba na askari wa vyeo mbalimbali 157 wa Kikosi cha Usalama Barabarani ambao utendaji kazi wao umeonekana kukosa tija.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman Kova alisema hivi karibuni kuwa uamuzi wa kuwabadilisha askari hao kutoka kikosi hicho kwenda katika kazi za kawaida umetokana na ufuatiliaji wa muda mrefu wa tabia na mwenendo wao.

Pia, alisema askari ambao watabainika kujihusisha na makosa ya moja kwa moja ya jinai kama vile rushwa au ukiukwaji wa maadili ya polisi, watashtakiwa katika mahakama za kijeshi.

Alisema uchunguzi zaidi unaendelea kuhusu vikosi vingine vya Kanda Maalumu na Jeshi la Polisi kwa ujumla ili kubaini kama kuna askari, mkaguzi au ofisa anayefanya kazi chini ya kiwango kisichoridhisha na ambaye analalamikiwa.

 Mtwara

Mkoani Mtwara, jeshi hilo limewabadilisha kazi askari 25 wa usalama barabarani kuwa askari wa kawaida. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Henry Mwaibambe alisema hivi karibuni kwamba sababu kubwa ni kuboresha utendaji hasa baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kuna baadhi ya askari wamekuwa wakiomba rushwa na wengine kulipa visasi.

“Tangu tumefanya maboresho haya tuna wiki mbili tu. Baada ya kupata malalamiko tuliyafanyia kazi ndipo tukagundua kuwa kuna baadhi ya askari hawafai kufanya shughuli za usalama barabarani tukaona ni bora tuwaondoe katika kitengo na kuwa askari wa kawaida,” alisema Mwaibambe.

Alisema mabadiliko hayo si wa askari wa usalama barabarani pekee, bali pia yamewakumba wa kitengo cha upelelezi.

 Tanga

Mkoani Tanga, polisi imefanya uhamisho wa ndani wa askari wake wa vikosi mbalimbali kikiwamo cha usalama barabarani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Zubery Mwombeji alisema uhamisho huo ulifanyika katika siku za hivi karibuni.

“Ni kweli hatua zimechukuliwa, lakini sheria ya jeshi la polisi inanikataza kutaja majina ya askari tuliowahamisha kuwashusha vyeo hata adhabu yoyote, ila nikuhakikishie tu kwamba tumefanya uhamisho mkubwa.”

 Kilimanjaro

Askari 38 wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Kilimanjaro wameondolewa kwenye kikosi hicho katika kipindi cha miezi sita iliyopita na kupangiwa majukumu mengine baada ya kukosa tija na ufanisi.

 Morogoro

Mkoani Morogoro, jeshi hilo limewahamishia katika vikosi vingine, askari 60 wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutokana na makosa ya kinidhamu na kiutendaji.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo alisema si kila kitu kinachofanyika ndani ya Polisi kinatangazwa kwa jamii.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe alisema katika kuboresha uwajibikaji kwenye taasisi za Serikali, askari 60 wa usalama barabarani mkoani hapa waliondolewa na kuhamishiwa vitengo vingine.


Njombe

Kadhalika, mkoani Njombe jeshi hilo limewabadilisha vitengo maofisa wake 20 wa kikosi cha usalama barabarani kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Wilbrod Mutafungwa alisema hivi karibuni kuwa kazi ya kuhamisha askari itakuwa endelevu ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi na maadili yanayotakiwa.

Arusha ngangari

Wakati makamanda wa mikoa kadhaa wakizungumzia kuwahamisha askari hao kutokana na utendaji usiokuwa na tija, Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha, Harrison Mwakyoma alisema trafiki yeyote atakayevunja au kukiuka maadili ya kazi atafikishwa mahakama ya kijeshi kujibu tuhuma zote zitakazomkabili na siyo kuhamishwa.

“Sisi hatuhamishi ila tunaadhibu kijeshi na tunawafikisha kwenye mahakama za kijeshi kwa utovu wa maadili,” alisema Mwakyoma.

Imeandikwa na Bakari Kiango, Mary Sanyiwa, Burhani Yakub, Hamida Shariff, Rachel Chibwete na Zulfa Musa.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top