Wema Sepetu |
Mkitaka kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu naendelea na shughuli zangu kama kawaida. Mungu ni mwema sana, anaendelea kubariki kazi ya mikono yangu, namuomba yeye aendelee kunibariki zaidi na zaidi.
Dhumuni la kuwaandikia barua hii ni kutaka kuwakumbusha kwamba nyinyi kwa sasa ni watu wazima. Umri wenu unatosha kabisa kusema haufanani na yale matukio yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Mara kadhaa nimewahi kuwaambia, hata yale mashindano yenu ya kumwaga fedha ukumbini, nyakati hizi si zake.
Mambo ya kuibiana mabwana kama yalishatokea, itoshe sasa kusema ulikuwa ni ujana. Kwa kuwa ilitokea, hakuna namna zaidi ya kuyasahau na kuchapakazi. Soko lenu la filamu bado haliridhishi, lakini mnapaswa kukomaa ili angalau mtengeneze fedha kupitia kazi zenu na si kuhongwa.
Binafsi sikufurahishwa na tukio lenu la kukutana ukumbini na kuzinguana mbele ya kadamnasi lililoripotiwa wiki iliyopita na magazeti Pendwa. Lilikuwa tukio linaloonesha kwamba bado hamjakua kitu ambacho sitaki kukiamini.
Wema na Kajala |
Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, huu siyo wakati wa nyinyi kuoneshana ubabe wa fedha. Kwamba eti kwa kuwa mwenzako kaenda kutunza msanii jukwaani, na wewe lazima utunze nyingi zaidi ili uonekane wewe ni zaidi.
Ndugu zangu, bahati nzuri maisha yetu tunajuana. Kwa kiasi kikubwa natambua maisha ya wasanii wetu nchini hususan warembo. Wengi wenu hamtegemei sanaa kuendesha maisha yenu. Wengi mnategemea mapedeshee au ‘mabwana’ kutamba mjini.
Niwashauri hizo fedha mnazozipata ni bora mngewekeza kwenye sanaa yenu. Mkajizatiti vizuri ili ziweze kuzaliana. Mnapigana ili iweje? Mnatambiana mbele za watu inawasaidia nini. Wenzenu wanapigana siku hizi wanaingiza fedha.
Nyinyi kazi yenu si ubondia. Kazi yenu ni uigizaji. Igizeni kwelikweli na Watanzania wawaunge mkono kwa kununua kazi zenu. Sanaa yenu ina changamoto nyingi, mnawezaje kuzishughulikia ikiwa hamna umoja.
Mtawezaje kutatua changamoto hizo ikiwa hamna upendo kati yenu? Si rahisi kutatua changamoto hizo wakati mna chuki. Ili mfanikiwe, mnahitaji kushirikiana. Shirikianeni ili muweze kuisogeza sanaa mbele, acheni vita ya kipuuzi mnayoendelea kuifanya.
Mkizingatia hayo niliyowaambia, hakika tutaona mabadiliko kwenu na sanaa kwa ujumla. Nina imani nyinyi ni watu wazima na mtajipanga upya na mtaanza kuchapa kazi kama kauli mbiu ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli, ‘Hapa Kazi Tu’.
Ni mimi mtu wenu,
Erick Evarist.
Post a Comment