Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga akizungumza na waandishi wa habari ofisi za Baraza zilizoko Mwenge jijini Dar es Salaam.
KAMATI
za maandalizi ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) iliyopo
chini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) imezindua rasmi tuzo hizo
ambazo zimeongezewa makundi mawili ya kushindania.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisi za Baraza zilizoko Mwenge Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, amesema makundi mapya ya kushindaniwa katika shindano la mwaka huu, ni habari za kodi na ukusanyaji mapato, na habari za manunuzi ya umma.
Amesema kwa maana hiyo, tuzo zitakazotolewa katika shindano safari hii zitakuwa 22.
Mukajanga
ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mandalizi ya Tuzo, ametaja
makundi mengine kuwa ni habari za uchumi na biashara; mazingira; afya;
michezo; ukimwi; utawala bora; michezo; jinsia; sayansi/teknolojia.
Makundi
mengine ni habari za afya ya mama na mtoto; uchunguzi; elimu; watu
wenye ulemavu; utalii na uhifadhi; katuni bora; kilimo; afya ya uzazi
kwa vijana; gesi; mafuta; na uchimbaji wa madini.
Amesema
makundi mawili mapya yamelenga kuhamasisha waandishi wa habari kuandika
habari zinazohusu umuhimu wa kulipa na kukusanya kodi na tuzo ya
masuala ya manunuzi ya umma kuwaongezea ari waandishi kupenda kufuatilia
namna serikali na asasi zake zinavyopata huduma mbalimbali.
“Haya
ni masuala yanayohimiza uwajibikaji katika sekta ya umma. Ni maeneo
ambayo waandishi wengi bado hawajayachangamkia katika kuyachunguza,
labda hawajui ni maeneo yanayoigharimu serikali fedha nyingi za
wananchi,” amesema Mukajanga.
Kuhusu
uwasilishaji kazi, waandishi wametakiwa kupeleka kazi zao kuanzia hiyo
jana Oktoba 16 mpaka Februari 15 mwakani. Kazi zote zipelekwe ofisi kuu
za MCT.
Mukajanga
amesema kilele cha shindano kitakuwa Aprili 29, 2016 watakapokabidhiwa
washindi tuzo zao zikiwemo vyeti, fedha taslimu vifaa vya kufanyia kazi
kwa waandishi wa habari.
Katika
hatua nyingine, Mukajanga amewataka waandishi wa habari kuwa makini
katika kazi zao hasa kipindi cha uchaguzi ambao kura itapigwa Oktoba 25
(Jumapili wiki ijayo).
Meneja
Udhibiti na Viwango MCT, Pili Mtambalike ambaye alihudhuria mkutano huo
wa waandishi wa habari, amesema vipengele vya kushindaniwa hubadilika
kila mwaka kutokana na kupata mawazo ya kuimarisha utoaji wa tuzo kwa
waandishi mahiri.
“Kumekuwa
na kudorora kwa baadhi ya vipengele hasa ‘habari za uchunguzi na
ufuatiliaji’ kutopata waandishi wengi. Miaka iliyopita baadhi ya
vipengele tulipokea kazi tano hata nne wakati nyingine zinakuja hata
1,000 na kuendelea. Waandishi leteni kazi za aina zote,” amesema
Mtambalike.
Post a Comment