NA; YOHANA CHALLE.
ARUSHA
CHAMA cha mpira wavu
Tanzania (TAVA) kushirikiana na chama cha mpira wavu Afrika(CAVB) pamoja na
shirikisho la wavu Duniani( FIVB) wamefanikiwa kuzindua vituo vya
kufunzia vijana (wasichana) katika mchezo wa wavu nchini .
Mwenyekiti wa
kuendeleza mchezo wa wavu shuleni na vyuoni Amoni Safieli alieleza
kuwa mpaka sasa tayari wamefanikiwa kufungua vituo vitatu nchini ambavyo
ni pamoja na kituo kilichopo shule ya sekondari Tanga,Masasi
sekondari –Mtwara na kituo cha shule ya msingi Manyara Ranch(Manyara Ranch
primary school centre) kilichopo wilayani Monduli mkoani Arusha .
“Tunatarajia kuwa
na vituo vinne vya kufunzia vijana hususani watoto wa kike wa mchezo huu
nchini ambapo mpaka sasa Tayari tumefanikisha kufungua vituo vitatu na
kituo cha nne tutakifungua mkoani Dodoma mda wowote ili kuweza kukamilisha zoezi
hili tayari kabisa kwa mafunzo kwa vijana .”alieleza Safieli.
Safieli alieleza
kuwa lengo kuu ni kuhakikisha vipaji vya watoto vinaanzishwa wakiwa shuleni ili
kuweza kuwa na wachezaji ambao watakuwa tayari wamelelewa na waalimu na
wataalamu waliobobea katika mchezo huo.
“Kila kituo
tulichozindua tulifanikiwa kutoa vifaa vya mchezo huo ambavyo ni mipira
200 pamoja na vyavu 8 ambapo vilikuwa na thamani ya shilingi milioni 50 kwa
kila kituo tulichofika kuzindua mradi huu ambao umelenga zaidi kwa
wanawake ili kuhakikisha wanakuwa wawakilishi vyema katika mashindano
mbalimbali. ”aliongeza Safieli.
Naye Rais wa
chama cha mpira wavu Tanzania (TAVA) Agustino Agapa alisema mradi huu ni
kwa wasichana ambapo unajulikana kama ndoto za Afrika (African Dreams
Project ) utaweza kuhusisha vijana walio na umri kuanzia miaka 8-10 na miaka
10-14 ambao watatafuta nchi nzima na watapelekwa katika vituo hivyo
ambapo vigezo mbalimbali vitatumika ili kuweza kuwapata ikiwemo umri na
wawe urefu wa kuanzia sm 170 .
“Matarajio yetu kuwa
baada ya miaka 5 ijayo tuwe na wachezaji bora watakao weza
kuwakilisha nchi katika mashindano mbalimbali ili kuweza kupeperusha bendera ya
taifa letu vyema .”alisema.
Agapa alieleza
kuwa kila kituo kitaanza kufundisha wachezaji 25 ambao watafundishwa na
wataalamu pamoja na wakufunzi waliobobea katika mchezo wa wavu na ifikapo
mwishoni mwa mwezi wa huu wataalamu wa chama cha wavu Afrika na
Shirikisho la wavu Duniani watafika nchini kwa lengo la kuja kutembelea vituo
hivyo ili kuangalia mahitaji na jinsi ya kusaidia.
Post a Comment