PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: SOMA HOTUBA YA UFUNGAJI KAMPENI YA MHESHIMIWA LOWASA JANGWANI JIJINI DARESALAAM JIONI HII HAPA...
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
· Ndugu watanzania wenzangu. Imebaki siku moja tu kabla hatujapiga kura katika Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 mwezi huu. Tumshukuru M...
·
Ndugu watanzania wenzangu.
Imebaki siku moja tu kabla hatujapiga kura katika Uchaguzi Mkuu hapo tarehe 25 mwezi huu.

Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka na rehema zake kwa kutufikisha hapa hii leo tukiwa na afya njema. Katika kipindi hiki cha kampeni tumewapoteza, kwa masikitiko makubwa, ndugu zetu kadhaa ambao walikuwa wagombea Ubunge na udiwani na wengine waliyokuwa wakishiriki katika mchakato huu wa uchaguzi kwa namna mbalimbali.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani, Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, Mzee wetu Dk. Emmanuel Makaidi, mawaziri Mama Celina Kombani na Dk. Abdallah Kigoda, vijana wetu Mohamed Mtoi na Deo Filikunjombe, Mchungaji Christopher Mtikila na Estom Mallah ambao wote walikuwa wagombea ubunge. Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahala pema peponi. Amen.
Katika kipindi cha kampeni nimefika katika kila kona ya nchi yetu, ninatoa shukrani za dhati kwa mapokezi makubwa, mapenzi na ukarimu wa Watanzania kwangu, kwa msafara wangu na mgombea mwenza, Mheshimiwa Juma Haji Duni.
Aidha natoa shukrani zangu za pekee kwa wenyeviti wenza wa Ukawa, Freeman Mbowe, James Mbatia, Twaha Taslima na marehemu Dk. Emmanuel Makaidi kwa mchango wao mkubwa katika kuchochea mabadiliko na msaada wao kwangu wakati wa kampeni.
Pia namshukuru kwa dhati mzee wetu, Kingunge Ngombale Mwiru, Waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye, viongozi mbali mbali wa CHADEMA na UKAWA ambao kwa pamoja walijitoa kwa moyo wao wote kungoza harakati hizi za mabadiliko. Ahsanteni sana
Kwa namna ya pekee, pia nimshukuru mke wangu mpenzi, Regina Lowassa kwa upendo, msaada na mchango wake katika kuhamasisha Watanzania na hususan wanawake wakati wote wa kampeni. Ahsante sana Regina.
Ndugu Watanzania wenzangu
Katika ziara hizi, nimeshuhudia vuguvugu la mabadiliko, kiu na ari ya Watanzania kuyapokea mabadiliko hayo. Lakini pia nimejionea shida zinazowakabili wananchi hao.

Nimesikia na nyakati nyingine kujionea kilio chao cha kunyanyaswa na kunyimwa haki zao na watendaji wa serikali na baadhi ya vyombo vya dola.
Nimekisikia kilio chao cha umaskini, afya na elimu duni. Nimekisikia kilio kikubwa cha vijana kukosa ajira na matarajio ya kesho bora.
Nimesikia rai za Watanzania na ndoto zao za kupata maendeleo, maji safi, makazi bora na barabara madhubuti.
Nimesikia malalamiko ya wakulima na wafugaji kukosa maji na ardhi. Nimesikia kilio cha madaktari, wauguzi, walimu, askari na watumishi wa taasisi za umma kuhusu mazingira magumu ya kazi, kodi za juu na maslahi duni.
Nimesikia kilio cha wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu ugumu wa mazingira ya kufanyia shughuli zao, kodi kandamizi na kukosa mitaji.
Nimesikia kilio cha wanawake kuhusu haki zao na ushiriki wao mdogo katika shughuli za kiuchumi. Nimesikia kilio cha wazee na wastaafu wasio na bima ya afya, wanaolipwa pensheni isiyokidhi mahitaji yao na ugumu wa maisha yao uzeeni.
Nimesikia kilio cha Watanzania dhidi ya rushwa iliyokithiri na utawala dhaifu ulioshindwa kuondoa umaskini au kutetea haki za raia.
Jibu langu ni fupi. Nimeona, nimesikia, nimeelewa na nitatenda.
Uchaguzi wa mwisho wa wiki hii ndiyo utakaotupa Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais mpya wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Ni uchaguzi muhimu na wa kihistoria kwetu sote.
Nawaomba nyote mliyojiandikisha mjitokeze kwa wingi kutimiza haki na wajibu wenu wa Kikatiba. Sehemu muhimu ya mabadiliko tunayodhamiria kuyaleta ni kujitokeza kupiga kura.
Ipo dhana potofu inayojengwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kwamba wafuasi na wanachama wa vyama vyetu vinavyo unganishwa na UKAWA wataleta fujo wakati wa kupiga kura. Ni maneno ya kipuuzi.
Hata hivyo nawaomba nyote muwe wastaarabu, muheshimu sheria zilizopo. Tukusanyike na kupiga kura kwa amani na utulivu.
Katika kampeni zetu nchini kote hadi hivi sasa tumedhihirisha kwamba vyama vyetu vya upinzani na wanachama wake hatuvunji, hatujavunja na hatutavunja sheria.
Hatuna sababu ya kufanya hivyo. Nia na dhamira yetu ni kushinda Uchaguzi huu na kuing’oa CCM madarakani.
Dhana na fikra zingine potofu zinazojengwa na uongozi wa CCM kwa nia ya kuwaogopesha Watanzania ni kwamba eti Watanzania wakichagua upinzani nchi itaingia kwenye machafuko. Wapuuzwe wenye fikra hizi wameshasahau hata historia ya hivi karibuni ya nchi tunazopakana nazo.
Wote ni mashahidi kwamba chama cha UNIP cha Zambia kilipoondolewa madarakani kwa kura za ndugu zetu wa Zambia, hapakutokea fujo zozote Zambia. Ukweli ni kwamba Mzee wetu mpendwa Mzee Keneth Kaunda aliyekuwa anaongoza chama tawala wakati huo yuko Zambia na anaendelea kufurahia maisha yake wakati Wazambia wakipiga hatua katika maendeleo ya Taifa lao.
Chama cha Malawi Congress Party pia kiling’olewa madarakani kwa kura za ndugu zetu wa Malawi. Malawi kwa miaka yote imeendelea kuwa tulivu.
Chama cha KANU Kenya pia kiliondolewa madarakani mwaka 2002. Ukweli ni kwamba matatizo yaliyojitokeza Kenya miaka mitano baadaye hayakutokana na kuondolewa kwa KANU. Yalikuwa ni madai yaliyotokana na taarifa za kuwepo kwa udanganyifu katika matokeo ya uchaguzi mkuu. La kujifunza hapa ni kwamba udanganyifu uliwaletea wenzetu wa Kenya matatizo. Ni lazima watanzania tuepuke udanganyifu wa aina hiyo.
Wako hata wanaotuogopesha sisi Watanzania kwa kutulinganisha na Walibya. Hawa wapuuzwe na waonewe tu huruma kwa kuwa wamesahau misingi na uimara wa nguzo za Taifa letu ambazo uongozi wa Baba wa Taifa Mwal. Julius Kambarage Nyerere aliotujengea. Kwanza hawajui hata kwa nini Libya wanapigana. Ukweli ni kwamba machafuko yao hayakutokana na uchaguzi. Yalisababishwa na watawala kung’ang”ania madaraka na kugawana rasilimali za taifa kwa misingi ya familia zao.
Kama ilivyotokea Zambia, Malawi na Kenya, Watanzania wamedhamiria kuleta mabadiliko kidemokrasia na kuiondoa CCM madarakani kwa kura zao.
Ndugu zangu,
CCM imekuwa madarakani kwa miaka mingi mno – zaidi ya nusu karne. Haina jipya; imechoka na haina pumzi ya kuongoza Taifa letu tena. CCM imebaki kuonyesha jeuri na kubeza tu. Imeishiwa nguvu ya hoja.

Watanzania wamechoshwa na ahadi hewa za CCM za miaka nenda, miaka rudi. Tusiruhusu CCM kuendelea kurubuni na kuhadaa wananchi.
Watanzania sasa wanataka MABADILIKO; mabadiliko ya kweli na ya uhakika.
Tarehe 25 mwezi huu tuhakikishe tunaing’oa CCM madarakani na kuanza safari mpya ya kuleta mabadiliko.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top