Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa jana amefanya kampeni kwa mara ya kwanza katika jimbo la Monduli na kumnadi mgombea ubunge wa Chadema, Julius Kalanga huku akieleza kuwa atazungumza na mgombea ubunge wa CCM, Namelock Sokoine kuona kama atakubali kupanda basi la Chadema chini ya Ukawa.
Lowassa
aliwaeleza wananchi wa Mto wa Mbu katika uwanja wa Barafu kuwa
atakutana na Namelock leo ili waelewane kwa kuwa asingependa kuvunja
umoja wao wa muda mrefu.
“Nimekuwa
mbunge kwa miaka 20 hivyo natakiwa nimjue mbunge atakayefuata,
nitakubaliana na Namelock akikataa kupanda basi hili basi,” alisema Lowassa.
Lowassa alisema anataka Monduli ibaki ile ile yenye amani na utulivu na ambaye hataki kupanda kwenye basi la Lowassa atabaki.
Wakati
Lowassa akizungumzia suala la kujadiliana na Namelock, mgombea wa
Chadema, Julius Kalanga alikuwapo akisubiri kunadiwa na mgombea huyo
ambaye alitumia muda mwingi kumzungumzia Namelock badala yake (Kalanga).
Baadaye Lowassa alimnadi Kalanga akimwombea kura kwa wananchi na kumpa nafasi ya kunadi sera zake.
Kabla ya Lowassa kumzungumzia Namelock, waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alianza kuzungumzia suala hilo akisema, “Najua tunaye mtoto wetu tumemtunza Namelock lakini hatuwezi kumsaidia kwa kuwa amebaki kwenye gari bovu.”
Sumaye alimtaka Namelock kuachana na kadi ya kijani ili aweze kupata nafasi nzuri kwenye serikali ya Lowassa.
“Namelock
atoke huko aungane na Lowassa hatuna sababu ya kuwa na tatizo naye.
Nchi nzima inahitaji mabadiliko na Lowassa atashinda kwa asilimia 80,
nashangaa Namelock anafanya nini huko CCM,” alihoji Sumaye na kuongeza: “Namwomba aachane na CCM aungane na sisi katika safari hii kwa kuwa nina uhakika Namelock atampigia kura Lowassa.”
Mbali
na Lowassa kuzungumzia suala la ubunge, aliwaomba wananchi wa Monduli
kumtafutia kura popote pale nchini kwa kuwa anahitaji kura nyingi ili
aweze kushinda urais.
“Mpigie shangazi yako kule Tabora na mwingine yeyote ili tupate kura,”alisema Lowassa.
Pia,
aliwaambia wananchi hao kuwa maendeleo yatakuja nchini kwa
kushirikiana, hivyo waache kuwa na ugomvi kati ya wakulima na wafugaji.
Alisema amefika Mto wa Mbu kufanya kampeni ila atapanga siku ya kwenda kuwaaga rasmi ili waweze kula nyama pamoja.
Alisema pamoja na kwamba anaachia ubunge, ahadi zake alizozisema akiwa mbunge ikiwamo ya benki, atazitimiza.
Akizungumzia
wito wa Lowassa, Namelock alisema hawezi kuzungumzia wito huo na kwa
sasa anaendelea na kampeni za ubunge kupitia CCM.
“Sina
maoni kuhusu kauli ya Lowassa, kwani sijamsikia mimi na hajawahi
kuniambia, nimepewa taarifa hizi kwa simu, ninaendelea na kampeni, kesho
(leo) nitakuwa Mto wa Mbu na Selela,” alisema jana.
Hata
hivyo, Jumatano alipozungumza kwenye uzinduzi wa kampeni zake katika
Kijiji cha Nanja, Namelock alimmwagia sifa Lowassa akimtaja kuwa mwalimu
wake kisiasa na kuahidi kuendeleza mema yote aliyoyaasisi na
kuyasimamiwa.
“Uhusiano
kati ya Lowassa na familia ya Edward Moringe Sokoine umejengwa katika
misingi isiyoweza kutetereshwa na harakati za kisiasa.
“Nitajidanganya
kubeza kazi aliyofanya Lowassa kwa Monduli ikiwamo kuboresha huduma za
elimu, afya, miundombinu na nyingine nyingi. Nitayaendeleza yote,” alisema Namelok.
Namelock
pia aliwamwagia sifa wabunge wengine waliowahi kuongoza jimbo la
Monduli akiwemo baba yake, Edward Sokoine na Lepilal ole Moloimet.
Alisema
Lowassa ndiye alimtambulisha kwa wazee wa mila na wana Monduli kuwa
anafaa kurithi kiti chake cha ubunge, hivyo ana imani atashinda na
hatamwangusha kwa kuwavusha salama wana Monduli.
Post a Comment