Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa. ( Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Na Mwandishi wetu
JUMUIYA ya Kimataifa imetakiwa kuwajibika kuhakikisha kwamba wanaweza kuwepo na amani na usalama kwa kuwa hilo ndilo tatizo kubwa duniani.
Hayo alisema Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard membe katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Hafla hiyo imefanyika viwanja vya Mnazi Mmoja mapema zaidi kuliko tarehe iliyopaswa ya Oktoba 24 kutokana na Tanzania kuwa katika mchakato wa uchaguzi.
Waziri Membe alisema kwamba dunia kwa sasa ipo katika changamoto kubwa ya usalama kutokana na mizozo inayoendelea katika nchi kadhaa duniani.
Alisema kumekuwepo na wimbi kubwa la mapigano ndani ya nchi mbalimbali katika nchi mashariki ya kati, Ulaya na hata Afrika, kukua kwa ugaidi na siasa za kibaguzi.
“ Sote tunafahamu shida iliyopo katika nchi kama Syria, Iraq, Somalia, Libya, Afghanistan, Yemen na jamhuri ya Afrika Kati” alisema waziri Membe na kuongeza kuwa matukio ya vita ya mara kwa mara, misimamo mikali na ugaidi vimekuwa vikisababisha vifo vingi na mateso kwa jamii.
Kutokana na hali ilivyo kwa sasa dunia haiko katika hali ya amani na hivyo juhudi zaidi zinatakiwa kufanyika ili kurejesha amani ambayo ni kiungo muhimu katika maendeleo.
Pamoja na kuzungumzia haja ya amani kutokana na dunia sasa hivi kufikia kiwango cha juu cha wakimbizi ndani na nje ya nchi zao, Waziri Membe alihimiza mabadiliko katika uendeshaji wa Umoja huo ili kuleta uwiano wa uwajibikaji kimataifa.
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akisalimiana na baadhi ya wakuu wa Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa nchini huku akiwa ameambatana na pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Liberata Mulamula (kushoto).
Mwaka 2005 idadi ya wakimbizi duniani ilikuwa milioni 38 lakini miaka kumi baadae takwimu zinaonesha kwamba kuna wakimbizi milioni 60 ikimaananisha kwamba katika kila watu 122 duniani, mmoja ni mkimbizi.Tanzania ina wakimbizi 169, 874.
Aidha alisema kwamba bara la Afrika linastahili kuwa na kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama ili maamuzi kuhusu Afrika yawe na mamlaka ya Afrika yenyewe.
Katika hotuba yake pia alizungumzia mafanikio ya Umoja wa Mataifa ikiwamo utengenezaji wa malengo mapya 17 ya maendeleo endelevu na pia ufanisi katika utekelezaji wa mashirika ya Umoja wa Mataifa yakifanyakazi kama kitu kimoja.
Alisifu mafanikio makubwa yaliyotokana na uongozi wa Mratibu wa Umoja wa Mataifa nchini Alvaro Rodriguez tangu alipofika nchini miezi 13 iliyopita.
Alisema utendaji wake unaozingatia ngazi za chini hadi juu na vijijini hadi mjini umeleta mafanikio makubwa kutokana na kuwa sehemu kamili ya utekelezaji wa mambo mbalimbali ya maendeleo na kupiga vita umaskini.
Pia alishukuru mchango wa Umoja wa Mataifa katika kufanikisha elimu ya uchaguzi hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi ambao utafanyika siku 12 zijazo.
Umoja wa Mataifa na wadau wake wametoa jumla ya dola za Marekani milioni 22.5 kwa ajili ya shughuli za uchaguzi mkuu nchini na kuimarisha demokrasia na utawala bora.
Naye Rais mstaafu Benjamin Mkapa akizungumza katika hafla hiyo alitaka dunia kutambua kwamba madhumuni ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa bado yapo palepale na kutaka nchi wanachama kutoa michango yao kuendelea kupambana na changamoto mpya za dunia katika masuala anuia ikiwamo vita, umaskini, chakula na mabadiliko ya tabia nchini.
Mkuu wa ushauri wa ufundi wa Mfuko wa Umoja wa mataifa wa Ukuzaji Mitaji (UNCDF), Peter Malika akisalimiana na Waziri Membe mara tu baada ya kuwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar.
Mataifa 51 yalikutana mjini San Francisco, Marekani baada ya vita kuu ya pili ya dunia na kuanzisha Umoja wa Mataifa. Wakati wa uanzishaji wa Umoja huo mataifa manne tu ya Afrika yalikuwepo nayo ni Liberia, Ethiopia, Misri na Afrika Kusini.
Hata hivyo rais huyo mstaafu alisema ili Umoja wa Mataifa ufanikiwe ipo haja ya kubadili mifumo yake ili iweze kuwajibika kikamilifu kwa dunia na wala si kwa matakwa ya waasisi na matajiri.
Pamoja na mabadiliko hayo nchi nyingi zinazoendelea zinataka kuwa na haki ya upigaji kura katika vyombo kadha vya Umoja wa Mataifa ikiwamo shirika la Fedha na Benki ya Dunia.
Naye Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza katika hafla hiyo katika viwanja vya Mnazi Mmoja alisema kwamba Umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwezesha amani na maendeleo.
Pamoja na kushukuru kwa wananchi wa Tanzania kuwa pamoja na Umoja wa Mataifa katika sherehe hizo muhimu sana Dunia nzima, alisisitiza, ushirikiano kuendelea kuwapo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadau wa maendeleo, na mashirika ya Umoja wa Mataifa.
“Kwa kuadhimisha siku hii ya Umoja wa Mataifa kwa pamoja, tunaimarisha ushirikiano wetu, katika masuala ya msingi, ambayo nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wamekubaliana nayo. “ alisema.
Aidha alizungumzia mapatano ya mashirika ya Umoja wa Mataifa na Tanzania na utekelezaji wa mipango ya maendeleo inayoichangiwa na UN nchini Tanzania chini ya UNDAP na kusema imeleta mafanikio makubwa.
Katika wiki ya Umoja wa Mataifa, wafanyakazi na viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wananchi waliwafanya shughuli mbalimbali zikiwamo za upandaji miti, usafi na miradi ya nishati mbadala.
Gwaride maalum katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa likitoa heshima kwa mgeni rasmi Waziri Membe (hayupo pichani).
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akikagua gwaride maalum lililoandaliwa kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar.
Waziri Membe akitoa heshima kwa bendera ya Umoja wa Mataifa ikipandishwa kama ishara ya kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum akisoma dua kubariki sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Kiongozi wa madhehebu ya Kikristo akiongoza sala katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Meza kuu kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin William Mkapa pamoja na mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe wakishiriki sala maalum ya kuombea amani ya nchi na Umoja wa Mataifa.
Baadhi ya wafanyakazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa wakitoa heshima kwa wimbo wa taifa.
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akitoa hotuba katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin William Mkapa akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe (kulia) akimpongeza Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin William Mkapa kwa hotuba nzuri aliyoitoa.
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Bw. Alvaro Rodriguez akizungumza machache kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa kabla ya kumkabidhi tuzo maalum Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe (wa pili kushoto) iliyoshuhudiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Balozi Liberata Mulamula na Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Celestine Mushy (kushoto).
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akimkabidhi Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Mh. Bernard Membe tuzo ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa kwa kuzingatia mchango wake katika Maendeleo ya Milenia (MDGs) na Maendeleo Endelevu (SDGs) katika maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja huo jana katika viwanja vya Mnazi mmoja.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (katikati) akimpongeza Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe mara ya kukabidhiwa na Umoja wa Mataifa kwa kutambua mchango wake katika Maendeleo ya Milenia (MDGs) na Maendeleo Endelevu (SDGs) katika maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja huo jana katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar.
Mshehereshaji katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa ambaye pia Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Mindi Kasiga akifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
Meza kuu.
Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Wadau wa Maendeleo pamoja Viongozi wa Serikali wakiwa jukwaa kuu.
Wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mmoja wa viongozi wa madhehebu ya dini wakifuatilia jambo kwa umakini katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Pichani juu na chini ni sehemu ya wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja Mataifa walioshiriki katika kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Maulida Hassan na Eliet Magogo wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri katika viwanja vya Mnazi Mmoja.
Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje wakibadilishana mawazo wakati wa sherehe hizo.
Wanafunzi kutoka shule mbalimbali nao walishiriki.
Maafisa wa jeshi nao walishiriki.
Meza kuu katika picha ya pamoja na viongozi wa madhehebu ya dini.
Meza kuu katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini pamoja na wadau wa maendeleo.
Meza kuu katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule mbalimbali walioshiriki kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 70 ya Umoja wa Mataifa.
Meza kuu katika picha ya pamoja na wakuu wa mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania.
Meza kuu katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa.
Meza kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez katika picha ya pamoja na wanafunzi walioshika mabango ya malengo endelevu.
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Mh. Benjamin William Mkapa wakiondoka kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja.
Mgeni rasmi Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mh. Bernard Membe akiteta jambo na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum wakati akiondoka kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula.
Post a Comment