Na Ferdinand Shayo,Arusha.
Asilimia 50%
ya wahitimu kutoka vyuo vikuu hawakidhi mahitaji ya soko la Ajira katika nchi
za Jumuiya ya Afrika Mashariki hali inayopelekea Wahitimu wengi kutoajiriwa
katika sekta binafsi na zile za serikali.
Kwa mujibu
wa utafiti uliofanywa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA) pamoja na Baraza la Biashara la Afrika
Mashariki (EABC ) mwaka 2013 hadi mwaka 2014 uliohusisha Waajiri kutoka mashirika binafsi na
yale ya serikali ,Waajiri wengi
walilalamikia juu ya Wahitimu wanaozalishwa na vyuo kutokidhi haja ya soko la
ajira.
Katibu Mkuu
wa Baraza la Vyuo vikuu vya Afrika Mashariki,Profesa Mayunga Nkunya alisema
kuwa changamoto zilizooainishwa katika utafiti huo na waajiri ni pamoja na wahitimu kutoweza
kutumia maarifa waliyoyapa kuleta tija katika maeneo ya kazi,kuwa na elimu ya
nadharia kuliko ya vitendo pamoja na kukosa ujasiri wawapo kazini.
Profesa Mayunga
aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa Habari juu ya Kongamano kubwa
la kuwakutanisha waajiri,Wafanyabiashara na Wanafunzi wa Vyuo litakalofanyika
nchini Uganda Octoba mwaka huu lengo ni kujadili mambo muhimu ambayo yanaweza kusaidia
kuboresha elimu ya vyuo iweze kukidhi matakwa ya soko la ajira.
Mayunga
alisema kuwa badala ya waajiri kulaumu wanayo nafasi ya kushiriki katika kutoa
mawazo ambayo yatasaidia katika kuwaandaa wahitimu waweze kuleta matokeo
yanayotarajiwa katika jamii.
“Waajiri
wengi hulalamikia mitaala yetu kuwa haiendani na hali halisi ya soko mingine
imeangalia mahitaji ya miaka ya nyuma na si sasa hiyo ni changamoto ambayo
inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu” Alisema Profesa Mayunga
Mkurugenzi
Mkuu wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) ,Lilian Awinja alisema
kuwa kutokana na ugunduzi wa mafuta na gesi unaoendelea katika ukanda wa Afrika
Mashariki vyuo vikuu vina jukumu la kuwaandaa wahitimu wawe na ujuzi
unaohitajika katika sekta hiyo badala ya kuchukua wataalamu kutoka nje.
Post a Comment