Mkurugenzi
Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa taasisi ya Young Scientists Tanzania
(YST), Dk. Gosbert Kamugisha, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo
pichani) leo hii wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya siku tatu ya miradi
na ubunifu wa kisayansi uliofanywa na wanafunzi kutoka shule 120
nchini. Maonyesho hayo yatafikia kilele Ijumaa Agosti 7, 2015. (Picha
zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).
Mwanzilishi Mwenza wa YST, Joseph Clowry, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo hii.
Makamu
wa Rais wa kampuni ya kuchakata mafuta na gesi ya BG Tanzania, John
Ulanga, akizungumzia udhamini wao katika maonyesho hayo ya YST. Kampuni
hiyo imetoa kiasi cha Dola 200,000 kudhamini maonyesho ya mwaka huu.
Naibu
Balozi wa Ireland nchini, Brian Noran, akizungumzia maendeleo ya tafiti
za kisayansi kwa taifa lolote duniani. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji
na Mwanzilishi Mwenza wa YST, Dk. Gosbert Kamugisha.
Mkutano ukiwaunaendelea.
Wanahabari wakiwa kazini.
Wanahabari wakifuatilia kwa makini.
Mwalimu
Geofrey Ndunguru (kulia) na mwanafunzi Yussuph Mwenda kutoka Shule ya
Sekonari ya Wavulana Songea nao wanashiriki maonyesho hayo kuzungumzia
Uchambuzi wa Mtazamo wa Wanafunzi Wasioona kuhusiana na Sayansi.
Mwanafunzi
Gladness Mpelemba (kulia) wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari
Sumaye mjini Morogoro akielezea kuhusu utafiti wao wa 'Kutumia Njia za
Asili za Kupanga Uzazi Kupunguza Madhara kwa Wanawake'. Kushoto ni
mwenzake Glory Crispine.
Wanafunzi wakiendelea kuonyesha tafiti zao.
Mojawapo ya utafiti uliofanywa na wanafunzi Saada Abeid na Zaina Maliki wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara.
Majaji
wakiwa kazini leo hii ili kuwapata washindi watakaotunukiwa zawadi
mbalimbali hapo kesho ambapo Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Alhaj Ali
Hassan Mwinyi, ndiye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Na Daniel Mbega
MAONYESHO
ya Tano ya Sayansi kwa wanafunzi wa shule za sekondari nchini
yamfunguliwa rasmi jijini Dar es Salaam leo yakiwa yanaendeshwa na
kuratibiwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST).Maonyesho hayo
ambayo yanafanyika kwenye Ukumbi wa iamond Jubilee yanashirikisha jumla
ya wanafunzi 240na walimu 120 kutoka shule 120 nchini yanatarajiwa
kufikia kilele keshokutwa Ijumaa ingawa kesho Alhamisi zawadi mbalimbali
zitatolewa kwa washindi zikiwemo fedha taslimu, medali, vikombe, vifaa
vya maabara pamoja na maktaba.
Dk.
Gosbert Kamugisha, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza
wa YST, amesema mgeni rasmi atakayetoa zawadi kwa washindi hapo kesho
atakuwa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
“Maonyesho
haya ni kwa ajili ya kuonyesha ubunifu na utafiti wa kisayansi
uliofanywa na wanafunzi wa sekondari na katika kipindi cha siku tatu
kuanzia leo wanafunzi hao wataonyesha miradi mbalimbali katika maeneo
tofauti ya kisayansi kama kemikali, fizikia na sayansi ya hisabati,
sayansi ya kibaolojia na kiikolojia, sayansi ya kijamii na kitabia, na
teknolojia,” alisema Dk. Kamugisha.
Aliongeza
kwamba, kama njia ya kutambua kazi iliyofanywa na wanafunzi hao, ndiyo
maana wameandaa zawadi mbalimbali kuwamotisha ambapo mbali ya zawadi
zilizotajwa, pia wanafunzi sita wanaweza kupata udhamini (scholarship)
kwa ajili ya masomo ya chuo kikuu kwa fani mbalimbali za sayansi na
teknolojia, udhamini ambao hutolewa na taasisi binafsi ya Karimjee
Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam.
“Maonyesho
ya mwaka 2015 ya YST yanalenga kuonyesha vipaji na ubunifu wa wanafunzi
wa sekondari, lakini pia ushuhuda wa umahiri wa mbinu za ufundishaji
kwa walimu ambao ndio wanaowaongoza wanafunzi hao yakiwa ni matunda ya
mafunzo yanayotolewa na YST kwa walimu wa sayansi katika kipindi cha
miaka minne iliyopita,” aliongeza Dk. Kamugisha.
Amewataja
wadhamini wakubwa wa maonyesho ya mwaka huu kuwa ni kampuni ya BG
Tanzania inayojihusisha na masuala ya utafiti wa mafuta na gesi asilia
pamojana Shirika la Kimataifa la Misaada la Ireland (Irish Aid).
Akizungumzia
mafanikio ya maonyesho hayo, Dk. Kamugisha alisema mwitikio umekuwa
mkubwa zaidi tofauti na walipoanza maonyesho hayo mwaka 2011.
“Wakati
tulipoanza mwaka 2011 walishiriki wanafunzi nane tu, mwaka 2012 wakawa
300 kwani zilikuwepo shule 100, mwaka 2013 walishiriki wanafunzi 200,
mwaka 2014 pia walikuwepo wanafunzi 200 lakini mwaka huu wamekuwa 240
kwani hata shule zimeongezeka kutoka 100 hadi 120.
“Tulipokea
maombi ya shule 400 nchi nzima, lakini tukaamua kuzichagua hizi 120.
Tulizitembelea shule zote 400 mara tatu kwa mwaka, ndipo hatimaye
tukaziteua hizi zinazoshiriki ingawa tunaamini kwamba shule nyingi sasa
zimehamasika na watoto wanapenda sayansi,” alisema.
Akizungumza
katika mkutano huo na waandishi wa habari, Mwanzilishi Mwenza wa YST
Joseph Clowry, alisema kwamba kuna dalili za mafanikio tangu walipopata
wazo la kuanzisha taasisi hiyo mwaka 2009, kwani mwitikio umeonekana
kuwa mkubwa kadiri miaka inavyokwenda.
Alisema,
ili taifa lolote liendelee, ni vyema kuwekeza zaidi katika tafiti za
kisayansi kwa kuanzia kwenye ngazi za chini kabisa kama wao
wananvyofanya.
“Ireland
ilikuwa nyuma kimaendeleo kama zilivyokuwa nchi nyingi ulimwenguni,
lakini walipoamua kuwekeza kwenye sayansi hali imebailika hivi sasa
ambapo wapo wanasayansi mahiri kabisa na vijana nao wanapenda kujifunza
masomo ya sayansi,” alisema Clowry.
Kwa
upande wake, Makamu Rais wa BG Tanzania anayeshughulikia Sera na
Masuala ya Uhusiano, John Ulanga, alisema wameamua kujitolea kudhamini
YST kwa sababu wanatambua kwamba Tanzania inahitaji kuwa na wanasayansi
wengi hasa tunapozungumzia suala la mafuta na gesi ambayo yakitafitiwa
yakapatikana na kuchakatwa yanaweza kuinua uchumi wa taifa kwa kiwango
kikubwa.
“Tunahitaji
wanasayansi wa kutosha katika sekta hii adhimu ya mafuta na gesi,
tukiwa nao wazalendo itakuwa ni bora zaidi, hivyo ni lazima tuwadhamini
watu kama YST ambao wanajenga msingi imara katika kuwapata wataalamu wa
kesho,” alisema Ulanga.
Ulanga
alisema kwamba, kwa mwaka huu kampuni yake imetoa Dola 200,000
(takriban Shs. 450 milioni) kwa ajili ya udhamini wa maonyesho hayo na
akaahidi kwamba wataendelea kudhamini kwa kadiri ya mahitaji na hali
itakavyoruhusu.
Naye
Brian Noran, Naibu Balozi wa Ireland nchini, amesema ni jambo la busara
kwa serikali na jamii kuwekeza katika utafiti wa kisayansi kama kweli
taifa linataka maendeleo, lakini akaahidi kwamba serikali yake
itaendelea kusaidia kwani inatambua umuhimu wa kuwa na wanasayansi
wabunifu.
Aliwapongeza
YST kwa hatua waliyoifikia mwaka huu na kuwahamasisha waongeze bidii
zaidi ili kujenga taifa la wanasayansi kwa kuanzia ngazi ya chini.
“Sayansi
ndiyo inayoweza kuleta mabadiliko na maendeleo, hivyo ni muhimu
kuendelea kuwazalisha wanasayansi ambao watakuja kuwa wabunifu wazuri
hasa katika karne hii ya sayansi na teknolojia,” alisema Noran.
(IMEANDALIWA NA www.brotherdanny.com. Simu 0656-331974)
Post a Comment