PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: VIKOBA ARUSHA YAMILIKI BILIONI 7.5
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Na Ferdinand Shayo,Arusha. Vikundi vya Kuweka akiba na kukopa jijini Arusha maarufu kama VIKOBA wameweza kumiliki kiasi cha s...



Na Ferdinand Shayo,Arusha.

Vikundi vya Kuweka akiba na kukopa jijini Arusha maarufu kama VIKOBA wameweza kumiliki kiasi cha shilingi bilioni 5.7 ambazo ni mtaji unaowawezesha kuwakopesha Wanachama wake ili waweze kujiendeleza kiuchumi na kuondokana na umasikini.

Mwenyekiti wa VIKOBA  mkoa wa Arusha Evance Chipini amesema kuwa vikundi hivyo vinatoa mikopo rahisi ambayo inawasaidia watu kujiendeleza kibiashara ama kuanzisha miradi itakayowakomboa kiuchumi.

Evance Akizungumza katika Kongamano la miaka 10 ya VIKOBA mkoa wa Arusha tangu ilivyoanzishwa mwaka 2005  lililoshirikisha wanachama wote wa vikoba mkoani hapa pamoja na taasisi za fedha amesema kuwa kwa sasa wana vikundi 250 ambavyo vinakadiriwa kumiliki kiasi cha shilingi milioni 35 kila kimoja hadi kufikia jumla ya shilingi bilioni 5.7 hivyo ameiomba serikali ivitambue vikundi hivyo pamoja na kuvisajili ili viweze kutambulika na taasisi za fedha.

“Licha ya mafanikio haya changamoto kubwa tunayokutana nayo hapa ni kupigwa dana dana juu ya usajili wa vikundi vyetu serikalini  wanatuambia twende kwa BRELA ile hali sisi hatuna biashara ya pamoja inayotupa faida tunapaswa kusajiliwa chini ya Idara ya Maendeleo ya jamii,tunaiomba serikali itusaidie katika hili” Alisema Evance

Katibu  Tawala Msaidizi ,huduma za kiuchumi na uzalishaji mkoani Arusha Hargeney Reginald amewaasa wanachama wa VIKOBA kuhakikisha kuwa wanaelekeza mikopo katika vipaumbele walivyojiwekea na kuepuka matumizi mabaya ya fedha ili waweze kuboresha maisha yao na kurejesha mikopo hiyo.

Afisa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Arusha Blandina Nkini amesema kuwa kwa sasa kuna mkakati wa Wizara ya Maendeleo ya jamii kufanya kazi kwa pamoja na Vikundi hivyo vya Wajasiriamali ambavyo asilimia 78% ni kina mama na pia kuwawezesha kupata mikopo ya kuwawezesha Wanawake na Vijana asilimia 10% inayotengwa kila mwaka katika  Halmashauri.

Naye Afisa Utekelezaji Bima ya Afya  kutoka Mfuko wa Taifa wa  bima ya Afya  (NHIF) Desderius Buhiye amewaasa Wanavikoba wajiunge bima ya afya kwani afya njema ni mtaji wa kwanza unaowasaidia Wajasiriamli kufanya kazi kwa ufanisi  na hata wanapokopa inakua rahisi kurejesha.


About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top