Kwa maoni yake, si kwamba viongozi au wanachama wa
vyama vingine vinavyounda Ukawa hawana sifa za kuwania nafasi hiyo ya
juu katika siasa nchini, bali Dk Slaa ana sifa ya ziada; ana mvuto.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kafulila,
ambaye alikuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kuondoka na kujiunga na
NCCR-Mageuzi mwaka 2010, alisema Dk Slaa ana nafasi kubwa kuliko
viongozi wa vyama vingine vya siasa vinavyounda umoja huo ambavyo ni
Chadema, NCCR, NLD na CUF kwa sababu katibu huyo mkuu wa Chadema
anakubalika zaidi katika jamii kulinganisha na wengine.
Vyama hivyo vinne vilitia saini ya makubaliano ya
ushirikiano Oktoba 27, hasa ya kusimamisha mgombea mmoja katika chaguzi
zote, kuanzia wa Serikali za Mitaa mwaka huu na madiwani, wabunge na
rais mwaka 2015.
Hata hivyo, bado kamati maalumu inatafakari jinsi
ya kutekeleza makubaliano hayo ili kuzuia uwezekano wa mpango huo
kuvurugika kama ilivyowahi kutokea kwenye chaguzi zilizopita.
Miongoni mwa watu wanaopewa nafasi ya kuteuliwa
kugombea urais kwa tiketi ya Ukawa ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Dk Slaa.
“Kwa maoni yangu bado namwona Dk Slaa kuwa ni mtu
ambaye ana nafasi kubwa kuliko wenzake. Kwa vyovyote itakavyokuwa yeye
ndiye anawazidi wenzake kwa kukubalika,” alisema Kafulila (32)
alipotakiwa kutoa maoni yake kuhusu mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa na
kuongeza: “Siyo kama wengine hawawezi, hapana, ila si kila mwenye mvuto
anaweza kuongoza na wala si kila mwenye sifa anayeweza kuwa na mvuto.
Pia si kila anayekubalika anaweza na si kila anayeweza anakubalika. Ni
adimu kukuta mtu anaweza na anakubalika pia.”
Katika matokeo ya utafiti wa taasisi ya Twaweza,
Dk Slaa alishika nafasi ya tatu nyuma ya waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa na wa sasa, Mizengo Pinda akipewa asilimia 11 ya ushindi
kulinganisha na Pinda (asilimia 12) na Lowassa (asilimia 13).
Lipumba amegombea urais mara nne, akiwa ameshika
nafasi ya pili mwaka 2000 na 2005 kabla ya kushuka mwaka 2010 wakati Dk
Slaa alipopata asilimia 26 za kura katika uchaguzi ambao mgombea wa CCM,
Jakaya Kikwete aliposhuka kwa takriban asilimia 20 ya kura alizopata
mwaka 2005.
Mbowe aligombea urais mwaka 2005 na kushika nafasi
ya tatu wakati James Mbatia hajawahi kugombea urais na katika siku za
karibuni ameonekana kuelekeza nguvu kugombea ubunge wa Jimbo la Vunjo,
ambako kuna uwezekano mkubwa akapambana vikali na mwenyekiti wa TLP,
Augustine Mrema.
Alipoulizwa kama kuna uwezekano wa mgombea wa
umoja huo kuibuka na ushindi, Kafulila alisema: “Ni mapema mno kusema
Ukawa inaweza kushinda. Hiyo itategemea tunajipangaje, tukifanya makosa
tutashindwa vibaya. Makosa ya CCM na Ukawa yanategemeana kwenye kuamua
nani agombee.”
Akizungumzia vigogo wa CCM wanaotajwa kuutaka
urais kama wana uwezo wa kuchuana na Dk Slaa, Kafulila alisema mpaka
sasa hajaona hata mtu mmoja mwenye uwezo na sifa za kuwa rais wa
Tanzania.
Post a Comment