MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Dismas Macha, amekamatwa akiwa na nyaraka mbalimbali za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada kubainika ni daktari ‘feki’ katika Kitengo cha Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka MOI, Frank Matua, alisema kuwa Macha ni daktari feki wa siku nyingi ambaye aliwahi kufanya utapeli kama huo MNH.
Alisema hadi daktari huyo anakamatwa, aliwekewa mtego baada ya kudanganya kwamba ana dada yake aliyefariki nchini India akiwa kwenye matibabu, hivyo alikuwa na orodha ya Maprofesa kadhaa iliyoonyesha kumchangia na alikuwa akipita wodini ili kuchangisha fedha aweze kusafirisha mwili wa marehemu huyo.
Matua, alisema baada ya wafanyakazi wa MOI pamoja na wagonjwa kumbaini kuwa ni mwongo, ndipo walimposubiri hadi alipofika na alipoingia tu ndani walimfungia na kuanza kumhoji, ambako alikiri kufanya utapeli huo wa udaktari feki na alikiri kuwatapeli wagonjwa mbalimbali, hivyo walipiga polisi ambao walifika na kumchukua kwa mahojiano zaidi.
Alifafanua kuwa, wakati Macha anafanya utapeli MNH aliwahi kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria lakini baadaye alirudi tena na kuingia katika chuo kikuu cha afya na sayansi shirikishi Muhimbili (MUHAS), akijifanya kwamba yeye ni mwanafuzi lakini baada ya kugunduliwa alihamia MOI.
Kutokana ana tukio hilo, Matua alisema jukumu la MNH ni kuhakikisha usalama unazingatiwa kutokana kwa kuimarisha ulinzi uliopo katika hospitali hiyo, ingawa vitendo vingine kama hivyo na ujambazi si mara ya kwanza kutokea hospitalini hapo.
Alitoa wito kwa Watanzania, kuwa makini na matapeli hasa katika hospitali mbalimbali hapa nchini.
MWISHO
Post a Comment