Arusha. Nchi za Kenya na India
zimeipita kwa mbali Tanzania kwa kusafirisha na kuuza katika soko la
dunia, madini ya tanzanite ambayo yanapatikana hapa nchini pekee.
Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na
Madini, Mhandisi Paul Masanja aliwaambia waandishi wa habari jijini hapa
jana kwamba kwa mwaka jana, Tanzania haikufikia hata nusu ya Kenya kwa
mauzo ya madini hayo ya vito.
Kamishna Masanja alisema mwaka jana pekee, Kenya
ilisafirisha na kuuza nje ya nchi tanzanite yenye thamani ya zaidi ya
Dola 100 milioni za Marekani (Sh173 bilioni) dhidi ya Dola 38 milioni
(Sh45.5 bilioni) zilizouzwa na Tanzania.
“Katika kipindi hicho cha mwaka jana, India iliuza
tanzanite zenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 300 milioni (Sh509
bilioni) kiasi cha baadhi ya wanunuzi wakubwa, hasa kutoka Marekani
kujiuliza iwapo madini hayo yanachimbwa India,” alisema Masanja.
Bila kumtaja jina, Kamishna huyo alisema mmoja wa
wanunuzi wakubwa wa madini ya vito kutoka nchini Marekani aliwahi
kumuuliza iwapo kuna migodi ya tanzanite India kwa sababu akifika huko
hupata tanzanite bora na zenye ukubwa kuliko anayopata Tanzania.
Alisema zaidi ya asilimia 80 ya tanzanite
inayopatikana Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, Manyara huuzwa kwa njia za
panya nje ya nchi na kwamba Serikali imeanza kuchukua hatua.
“Serikali inakusudia kuunda kikosi kazi
kitakachojumuisha askari kutoka vyombo vyote vya ulinzi na usalama
kukabiliana na utoroshaji madini nje ya nchi.”
Alisema hivi karibuni, wizara itawasilisha muswada
bungeni kurekebisha Sheria ya Madini Namba 6 ili kumpa mamlaka Kamishna
wa Madini kutaifisha madini yote yanayokamatwa yakisafirishwa kinyume
cha sheria.
“Tunataka sheria ya madini ifanane na ile ya
misitu inayotaifisha mazao yote ya misitu yanayovunwa kinyume cha
sheria, tofauti na sasa ambapo tunalazimika kusubiri uamuzi wa Mahakama
kutaifisha madini iwapo watuhumiwa wanatiwa hatiani,” alisema.
Hadi sasa, Serikali imekamata na kutaifisha madini
yenye thamani ya zaidi ya Sh15 bilioni yaliyokamatwa yakitoroshwa nje
ya nchi baada ya watuhumiwa kutiwa hatiani na Mahakama.
“Tuna mpango wa kujenga kituo maalumu cha madini
kitakachojulikana kama Madini House kitakachokuwa na ofisi zote za
kununua na kuuza madini ya vito ili kudhibiti biashara holela,” alisema
Masanja.
Alisema katika kituo hicho kutakuwa na huduma za
kodi na malipo mbalimbali ya Serikali pamoja na usafiri wa helikopta za
kusafisha madini kwenda viwanja vya ndege ili kuepuka wizi na uvamizi
njian
Post a Comment