Kibondo. Mbunge wa Jimbo la
Muhambwe mkoani Kigoma, Felix Mkosamali amefikishwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Kibondo akikabiliwa na shtaka la kumzuia karani mwandikishaji
kufanya kazi yake.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Peter Makala alidai
jana mahakamani hapo kuwa mbunge huyo alitenda kosa hilo juzi, baada ya
kufika Kituo cha Kitongoji cha Nduta, Kijiji cha Kumhasha, Kata ya
Murungu, wilayani Kibondo na kumzuia karani kuendelea kuandikisha wakazi
kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Makala alidai kuwa kitendo cha kumzuia karani huyo
kuendelea kufanya kazi yake ni kinyume na ukiukwaji wa Sheria ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Pia, alidai kuwa kitendo cha kuwazuia wakazi hao
kujiandikisha ni kuwanyima haki yao ya msingi, kwani baada ya kuzuiwa
waliendelea kudai kutaka kujiandikisha lakini mshtakiwa hakusikiliza
kilio chao.
Mshtakiwa alikana shtaka na Hakimu Erick Marley
alisema dhamana iko wazi kwa mdhamini kusaini bondi ya Sh4 milioni.
Mbunge huyo alitimiza masharti na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba
29.
Mkosamali alikamatwa juzi jioni baada ya kudaiwa
kumnyang’nya karani vitabu na madodoso na kuyapeleka ofisi ya Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo.
Post a Comment