Dhana na Misingi ya Utafiti wa Kura ya Maoni na maana pana ya matokeo ya Twaweza
PAMETOKEA malumbano ambayo binafsi naweza kusema ni ‘yasiyo na tija’ kuhusu matokeo ya utafiti wa kura ya maoni uliotolewa na shirika la Twaweza hivi majuzi. Kwa kiasi kikubwa malumbano haya yamesababishwa na utamaduni wa wanasiasa wetu wa kutokuheshimu tafiti kwa kuwa wamezoea kufanya maamuzi kwa kuzingatia zaidi hisia badala ya mantiki na ushahidi wa mambo unaotokana na tafiti.
Aidha, malumbano haya yamesababishwa na ukweli kwamba tafiti zinazohusu kura za maoni siyo jambo lilizoeleka hapa kwetu. Tangu mfumo wa vyama vingi uanze, na kabla ya Twaweza, ni mashirika machache tu ambayo yamewahi kufanya tafiti kadhaa za kura za maoni, yakiwemo REDET ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Synovate. Katika nchi za magharibi na hata baadhi ya nchi za Afrika kama vile Kenya, Zambia, Afrika Kusini, Malawi na nchi nyingi za Afrika Magharibi, tafiti za kura za maoni ni jambo la kawaida na wanasiasa katika nchi hizo wameshazoea na wanajua namna ya kutumia matokeo ya tafiti hizi.
Katika makala haya nafafanua dhana na misingi ya tafiti za kura ya maoni na kutoa maoni yangu kuhusu maana ya baadhi ya vipengele vilivyojitokeza katika matokeo ya utafiti wa Twaweza.
Dhana ya utafiti wa kura ya maoni
Matokeo ya utafiti wa kura ya maoni kuhusu uchaguzi huwa ni kiashiria cha mambo yanavyoweza kuwa kama uchaguzi ungefanyika siku ambayo utafiti huo ulifanyika. Kwa hiyo, kimsingi, matokeo ya kura ya maoni siyo matokeo ya uchaguzi bali ni utabiri wa kisayansi kuhusu namna ambavyo wananchi wanatarajiwa kupiga kura. Ili utafiti wa kura ya maoni uweze kutabirika lazima tafiti hizo zifanyike mara kadhaa na pengine zifanywe na mashirika kadhaa tofauti. Wataalamu huweza kukokotoa wastani wa matokeo kutoka tafiti tofauti tofauti na kutumia wastani huo kutabiri nani anaweza kuibuka mshindi.
Msingi wa tafiti za kura ya maoni ni hojaji ya watu wachache waliochaguliwa kwa njia ya bahati nasibu. Hoja hii inaweza ikafanywa kwa njia ya ana kwa ana kati ya mtafiti na anayehojiwa, kwa njia ya aneyehojiwa kutumiwa dodoso kwa nia ya posta au kwa kupigiwa simu. Katika nchi ambazo teknolojia imesambaa na ambapo karibu kila raia ana uwezo wa kupata mtandao wa intaneti, kura ya maoni pia huweza kufanyika kwa kutumia njia ya mtandao kama vile kupitia barua pepe au kujaza dodoso moja kwa moja kwenye tovuti. Kila moja ya hizi njia ina faida na hasara zake, na hakuna hata njia moja ambayo ni murua kwa asilimia mia moja.
Katika utafiti wa kura ya maoni kinachozingatiwa sio idadi ya watu waliohojiwa lakini namna ambayo wahojiwa walipatikana. Ili matokeo ya utafiti yaweze kuakisi hali halisi lazima wahojiwa wapatikane kwa njia ya bahati nasibu (random sampling). Katika nchi nyingi tafiti nyingi za kura ya maoni huwa na idadi ya watu kati ya 1000 hadi 5000. Marekani, kwa mfano, ambayo ina idadi ya watu wasiopungua milioni 300, tafiti nyingi za kura ya maoni zimekuwa zikitumia idadi ya watu wasiozidi 2000 na mara nyingi tafiti hizo zimetoa matokeo yanayoakisi hali halisi katika uchaguzi mkuu. Kwa hiyo hoja kwamba utafiti wa Twaweza, uliokuwa na idadi ya watu zaidi ya 1000, ulitumia idadi ndogo ya watu na hivyo haukuakisi hali halisi ya wananchi walio wengi sio hoja ya maana katika muktadha wa kitafiti kwa kuwa watu walioshiriki walichaguliwa kwa njia ya bahati nasibu.
Hoja nyingine ambayo imepigiwa kelele sana ni matumizi ya simu hasa pale ambapo wahojiwa waligawiwa simu za mkononi. Nieleze tu hapa kwamba hili si jambo la ajabu. Lengo la kuwagawiwa wahojiwa simu ni kuepuka uwezekano wa baadhi ya wahojiwa waliochaguliwa kushiriki kushindwa kufikiwa kwa sababu ya kutokuwa na simu. Huu ni utaratibu wa kawaida duniani kote. Naelewa watu wanaohoji jambo hili na kuhisi kwamba hiyo inaweza ikawa hongo kwa sababu utamaduni wa rushwa umezagaa mno katika nchi yetu kiasi kwamba kila kitu sasa tunakitilia shaka.
Nini maana ya matokeo ya Twaweza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015?
Kama nilivyoeleza awali matokeo yoyote ya utafiti wa kura ya maoni ni kiashiria tu na wala sio hitimisho au matokeo kamili ya uchaguzi. Matokeo ya namna hii yanapaswa kuwasaidia wagombea mbalimbali katika kujipanga kushinda chaguzi zijazo. Kwa wale ambao wanaonekana kukubalika zaidi wanapaswa kutumia matokeo hayo kuendelea kujiimarisha zaidi. Na kwa wale ambao wanaonekana kutokufanya vizuri matokeo haya yanapaswa kuwasaidia kujipanga upya na hata kubadili mbinu na mikakati yao.
Kwa hiyo hakuna sababu yeyote ya wagombea ambao wanaonekana kusuasua kuanza kuchanganyikiwa na kuanza kurusha maneno ya kilevi barabarani kwa sababu safari bado ndefu sana ikizingatiwa kuwa maoni ya wananchi hubadilika mara kwa mara kutokana na hali ya kisiasa inavyobadilika. Tafiti zinaonyesha kwamba takribani asilimia 30 ya wapiga kura hubadili mawazo yao dakika chache kabla ya kupiga kura na ndio maana kampeni za mwisho ni muhimu sana. Katika mfano wa hivi karibuni kabisa uchambuzi wa matokeo ya kura maoni iliyopigwa Scotland unaonyesha kuwa wapiga kura wengi walibadili mawazo siku ya mwisho kufuatia hotuba ya Waziri Mkuu wa zamani Gordon Brown. Ndio maana narudia tena kwamba matokeo ya Twaweza hayapaswi kuwapa homa wagombea na vyama vyao bali yanapaswa kuwa kengele ya kuwaamsha kujipanga vyema.
Matokeo ya Twaweza yanatupa picha kadhaa kuhusu mtazamo wa wananchi tunapoelekea katika uchaguzi mkuu ujao. Mosi, wananchi walio wengi hawaridhishwi na mwenendo wa taasisi za siasa za sasa pamoja na wanasiasa wanaotarajiwa kugombea. Hili linathibitishwa na vipengele vitatu vya matokeo hayo. Kipengele cha kwanza ni idadi kubwa ya watu ambao hawajaamua chama au mgombea wa kumchagua ambayo ni asilimia 33 ya watu wote waliohojiwa. Pili, hakuna hata mgombea moja ambaye alichaguliwa na watu zaidi asilimia 15. Hii inaonyesha wananchi walio wengi bado hawana chaguo la chama wala mgombea.
Tatu, wananchi wachache sana kati ya waliohojiwa walionyesha kuridhika na utendaji wa viongozi waliopo sasa pamoja na vyama vyao. Kati ya wananchi wote waliohojiwa, asilimia 15 tu ndio walisema wanaridhishwa na utendaji wa CCM na asilimia 18 to ndio walisema wanaridhishwa na utendaji wa vyama vya upinzani. Hii inamaanisha kuwa wananchi walio wengi hawana imani na vyama vya siasa vilivyopo. Hii inatoa fursa kwa vyama hivi kujipanga upya na kujitathimini na kukubali ukweli kwamba mambo wanayoyafanya kwa sasa hayagusi moja kwa moja maisha ya wananchi na ndio maana wananchi hao hawajajipambanua navyo. Hii pia ni fursa kwa vyama vipya vinavyochipuka katika kujaribu kuziba pengo lililo wazi kabisa katika ulingo wa siasa hapa nchini. Matokeo haya pia yanatoa picha kwamba inawezekana nchi yetu ina ombwe kubwa la uongozi na pengine tunahitaji kizaizi kipya cha wanasiasa. Pengine pia tunahitaji kuwasukuma watu ambao tunajua wanaweza kuwa viongozi wazuri lakini hawataki kuwa viongozi. Naamini watu hawa wapo katika nchi yetu na wanashindwa kujitokeza kutokana na mazingira ya kisiasa kuchafuka mno.
Hitimisho
Nasisitiza kwamba matokeo ya utafiti wa kura ya maoni katika siasa ni utabiri wa kisayansi unaobashiri mambo yanavyoweza kuwa katika uchaguzi mkuu ujao. Kwa hiyo, haya sio matokeo ya uchaguzi kiasi cha kufanya watu wengine waandae sherehe za kushangilia na wengine waanze kuchanganyikiwa kana kwamba ndio kweli wameshashindwa katika uchaguzi. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kuwa katika nchi nyingi matokeo ya utafiti wa kura ya maoni umeakisi hali halisi katika uchaguzi. Ni mara chache mno pale ambapo matokeo ya utafiti wa kura ya maoni yametofautiana na hali halisi baada ya kura kupigwa. Kwa hiyo wanasiasa ambao wanadharau matokeo ya utafiti wa Twaweza wanafanya hivyo kujiridhisha kisaikolojia lakini ni kwa hasara yao wenyewe.
CREDIT: FIKRA PEVU
Post a Comment