Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akikagua Jengo la Mahakama ya
Mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania
leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu
wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkuu wa Taasisi hiyo Jaji
Dkt. Gerald Ndika.
Waziri
wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro akikagua Jengo la Mahakama ya
Mafunzo katika Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania
leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu
wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkufunzi wa Taasisi hiyo
Bw. Goodluck Chuwa.
Mkuu
wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania Jaji Dkt.
Gerald Ndika (kulia) akiongea na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.
Asha-Rose Migiro nje ya Jengo la Mahakama ya Mafunzo katika Taasisi hiyo
leo (Ijumaa, oktoba 24, 2014) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu
wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na kulia ni Mkufunzi wa Taasisi hiyo
Bw. Goodluck Chuwa. (Picha na Martha Komba, Wizara ya Katiba na Sheria).
Serikali
inakamilisha taratibu za kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria
unaolenga kurekebisha Sheria ya Bodi ya Mikopo ili kuwawezesha wanafunzi
wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (LST) kupata
mikopo kwa ajili ya mafunzo yao.
Waziri
wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Asha-Rose Migiro amewaambia wanafunzi wa
taasisi hiyo jijini Dar es Salaam leo (Ijumaa, Oktoba 24, 2014) kuwa
lengo la Serikali kukamilisha mchakato huo katika kipindi cha mwaka
mmoja kuanzia sasa.
"Nafahamu
kuna changamoto ya baadhi yenu kukosa mikopo, nimeambiwa na Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya
Uendeshaji wa Taasisi hii Bw. George Masaju kuwa taratibu za kurekebisha
Sheria ya Bodi ya Mikopo umeanza ili wanafunzi wa taasisi wapate
mikopo,” amesema Dkt. Migiro.
Waziri Migiro, ambaye aliongozana na Naibu wake Mhe. Angellah Jasmine Kairuki na Bw. Masaju, amezungumza na wanafunzi wa Taasisi hiyo iliyopo nyuma ya Jengo la Mawasiliano (Mawasiliano Towers) jijini Dar es Salaam.
Katika
ziara yake ambayo ni ya kwanza tangu ateuliwe na Mhe. Rais kuiongoza
Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri Migiro alikagua ujenzi wa majengo ya
kudumu ya taasisi hiyo pamoja na kukutana na watumishi na wanafunzi ili
kubadilishana mawazo.
Ujenzi wa majengo hayo ya kisasa ya kudumu, ulianza Mwezi Novemba, 2010 na kukamilika Agosti, 2012 na umegharimu zaidi
ya Tshs 16.1/- Bilioni na umefanywa na Serikali kupitia Programu ya
Maboresho ya Sekta ya Sheria (LSRP) iliyokuwa inatekelezwa chini ya
Wizara ya Katiba na Sheria.
Ujenzi huo umejumuisha Mahakama ya Mafunzo, Maktaba, Madarasa, Jengo la Utawala, Ukumbi wa shughuli mbalimbali na nyumba za watumishi.
Katika mazungumzo yake na wanafunzi hao, Dkt. Migiro pia aliwakumbusha wanafunzi hao kujiandaa kutoa huduma bora kwa jamii pale wanapohitimu kwa kuzingatia kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kuendesha mafunzo hayo.
“Mkumbuke
ule wito wa Mwalimu Nyerere kuwa nyie ni kama yule mtu aliyetumwa na
kijiji chenye njaa kwenda kutafuta chakula ili arudi kuwasaida
wanakijiji wenzake,” alisema Waziri Migiro na kufafanua kuwa kuna
wananchi wengi wanaohitaji huduma za kisheria nchini ambao wanawasubiri.
Akizungumza katika
ziara hiyo, Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Jaji Gerald Ndika alimweleza
Waziri Migiro kuwa tangu kuanza rasmi kwa mafunzo katika Taasisi hiyo
mwezi Machi mwaka 2008 hadi Julai mwaka huu, jumla ya wanafunzi 4,755
wamedahiliwa katika makundi tofauti na kati yao, wanafunzi 1,715
wamefaulu mafunzo na kupata cheti cha Stashahada ya Uzamili katika
Utalaam wa Sheria (Post-Graduate Diploma in Legal Practice).
“Tunafurahi
kuwa katika wanafunzi wetu 1,715 waliofaulu tangu kuanzishwa kwa
Taasisi hii, wahitimu 1,540 wameorodheshwa kuwa Mawakili wa Kujitegemea
baada ya kukamilisha taratbu na waliobaki wanaendelea kukamilisha
taratibu,” alisema Jaji Dkt. Ndika.
Pamoja
na mafanikio hayo, Mkuu huyo wa Taasisi amesema kumekuwa na malalamiko
kuhusu ufaulu mdogo hususan katika hatua ya kwanza (first sitting) na
kufafanua kuwa Bodi ya Uendeshaji chini ya Uenyekiti wa Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeunda Kamati Maalum ili kufanya utafiti
kwa lengo la kubaini kiini cha matokeo hayo.
“Bodi
imeunda Kamati Maalum inayoongozwa na Prof. Bonaventure Rutinwa na
inajumuisha wadau wengine kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Mahakama ya Tanzania, Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na tunatarajia
taarifa yake itakuwa tayari ifikapo mwanzoni mwa mwezi ujao wa Novemba,
2014” amefafanua Mkuu huyo wa Taasisi.
Akiongea
katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Uendeshaji na Naibu
Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. George Masaju amesema lengo la
kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni kuwanoa wahitimu wa shahada ya kwanza ya
sheria ili kukabiliana na changamoto za sasa hususan katika taaluma ya
sheria.
“Hapa
wanafundishwa vitu vingi ikiwemo namna ya kujadiliana katika mikataba na
mengineyo mengi ambayo kwa sasa ni changamoto,” amesema Bw. Masaju
ambaye aliongozana na Wajumbe wa Bodi wakiwemo Mawakili Bw. Charles
Rwechungura na Bi. Aisha Bade.
Post a Comment