Afisa
wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Bibi Ellen Maduhu
akisoma hotuba katika Kamati ya Tatu ya Umoja wa Mataifa jijini New
York, Marekani.
Serikali
imetahadharisha kuwa endapo mchakato wa kuandaa Agenda ya Maendeleo
baada ya Mwaka 2015 unaoendelea hivi sasa katika Umoja wa Mataifa,
hautazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, dhamira ya kufikia
maendeleo endelevu itakuwa ni ndoto kwa kuwa katika kila idadi ya watu
watano duniani, mmoja wao ana ulemavu.
Kauli
hiyo ilitolewa na Bibi Ellen Maduhu, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania
katika Umoja wa Mataifa, alipokuwa anahutubia wajumbe wa Kamati ya Tatu
ya Umoja huo jijini New York, Marekani siku ya Jumatano tarehe 08 Oktoba
2014.
Bibi
Maduhu alieleza kuwa wakati utekelezaji wa Malengo ya Milenia unafikia
kikomo mwaka 2015, ni muhimu watu wenye ulemavu wakashirikishwa
kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Aidha, ni vema nchi zikawa na
utaratibu mzuri kuhakikisha kuwa kundi la watu wenye ulemavu linafaidika
na hatua za maendeleo zinazopigwa, kwa kuwa hiyo ni haki yao na ni
wajibu wakapatiwa.
Hotuba
hiyo ilifafanua mikakati mbalimbali inayochukuliwa na Serikali katika
kuboresha maeneo mbalimbali ya kijamii kwa faida ya wananchi wake.
Maeneo hayo ni pamoja na elimu, afya, ugatuzi wa madaraka na kuondoa
umasikini.
Kwa
upande wa elimu, alieleza kuwa Serikali inalipa kipaumbele eneo hilo,
kwa kuwa inaamini endapo litaimarishwa ipasavyo na kuwafikia watu wote
wakiwemo wanyonge itakuwa ni ukombozi kwa sababu itatoa dira ya kuondoa
umasikini.
Kwa
kuliona hilo, Serikali imechukuwa hatua mbalimbali za kuboresha sekta
ya elimu ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya shule ya msingi kwa wote.
Mchakato uliopo ni kuhakikisha kuwa elimu ya sekondari nayo itolewe kwa
wote. Aidha, Serikali inaimarisha elimu ya ufundi ili iweze kutoa ujuzi
kulingana na mahitaji ya sasa. Maboresho hayo pia yanagusa elimu ya juu
ambayo inapanuka kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.
Mbali
na maboresho hayo yanayofanywa katika sekta ya elimu, Bibi Maduhu
alikiri kuwa bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi na kutoa
wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na Serikali katika
kukabiliana nazo. Changamoto hizo ni pamoja na ubora wa elimu
inayotolewa; watoto kutomaliza elimu zao; upungufu wa walimu bora;
ukosefu wa vifaa vya kujifunzia kwa njia ya mtandao na vitabu.
Katika
sekta ya afya, Serikali imekuwa ikiendelea kuiboresha sekta hiyo kwa
kuhakikisha kuwa watu wote wanapata huduma ya afya ya msingi, licha ya
changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa rasilimali watu.
Bibi
Maduhu alihitimisha hotuba yake kwa kueleza kuwa, lengo la Serikali ni
kuhakikisha kuwa wananchi wote wanawezeshwa ili waondokane na umasikini,
hivyo Serikali imekuwa ikiandaa sera zinazotoa fursa kwa wananchi wote
kushiriki katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao. Sera hizo ni pamoja
na ugatuzi wa madaraka kwenda katika Serikali za mitaa ambako ndipo
wananchi wengi wanapatikana.
Post a Comment