MAZINGIRA DUNI KIZINGITI CHA ELIMU YA CHEKECHEA NCHINI
UKOSEFU wa Miundombinu ya kutosha katika shule za awali na msingi, njaa na umbali wa kutoka shuleni hadi katika makazi ya watu, vimetajwa kuchangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa shule hizo katika maeneo mengi nchini.
baadhi ya walimu katika shule hizo wamesema ukosefu wa miundombinu ya kutosha, mrundikano wa wanafunzi wengi katika darasa moja na kukosekana kwa chakula cha mchana ni miongoni mwa sababu zinazozidi kudidimiza kushuka kwa kiwango cha elimu katika maeneo yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanafunzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma wameitaka serikali kuwajengea mabweni ili walale shuleni kwani wanyama wakali na mazingira duni ya familia zao yanawafanya kukata tamaa na kuendelea na masomo.
Wameeleza kuwa endapo serikali itaweke mfumo wa kila shule inayojengwa kuwa na bweni, itasaidia elimu inayotolewa katika shule hizo kuwa na kiwango cha juu kuliko ilivyo hivi sasa.
Elimu ya awali
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi wanaosoma katika shule za binafsi za jijini Dar es Salaam, wamesema wanafunzi wanaosoma shule za awali (chekechea) zenye gharama kubwa wamekuwa na uelewa mkubwa ikilinganishwa na wanafunzi wanaosoma katika shule za awali za kawaida hali inayowasababishia walimu wa shule za msingi kupata wakati mgumu kuwaweka sawa kielimu.
“Kweli hizi shule zina gharama tofauti tofauti, nyingine zinagharama kubwa na nyingine ndogo, lakini kimsingi kitu chochote kinachokuwa bora na gharama yake inakuwa ni kubwa, kwahiyo kikubwa kinachotakiwa sisi wazazi ni kujipanga vizuri kwa ajili ya kuwawekea watoto wetu misingi mizuri wanapokwenda katika shule nyingine ili wakafanye vizuri zaidi” alieleza mmoja wa wazazi hao.
Zainab Emanuel, mkazi wa Makabe jijini Dar es Salaam ameitaka serikali kuweka utaratibu maalum wa kuangalia kuwa shule zote zinakuwa na mpango mmoja kwa kutoa elimu kwa viwango visivyotofautiana ili kuwa na mfumo wa elimu uliolingana.
Hata hivyo, wakazi wa jiji hilo wameitaka serikali kufuatilia kwa karibu utaratibu unaotumiwa na walimu wa shule za awali wa kufundisha wanafunzi kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wazazi wanaodai kuwa walimu hao wamekuwa wakitengeneza msingi mmbaya kwa watoto wa elimu ya awali.
“Serikali iweke miongozo mizuri hususani katika shule za awali maana hizi shule ndizo sehemu za kumjenga mwanafunzi katika maisha yake ya mbele, tusikimbilie kuwaacha wasome katika mazingira duni na baadae wakimaliza elimu ya darasa la saba ndio tunawahamisha kwenye shule za binafsi” Zainab alisema
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati kukiwa na taarifa kuwa ufinyu wa bajeti kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini na malipo kidogo kwa walimu wanaosahihisha mitihani ni mojawapo ya sababu za kushuka kwa viwango vya ufaulu nchini, imebainika kuwa kitendo cha kupuuzia elimu ya awali, ndicho kinachosababisha kushuka kwa kiwango cha elimu nchini, na kwamba hakuna njia ya mkato zaidi ya kuwekeza katika elimu ya awali.
CREDIT: FIKRA PEVU
Post a Comment