WAKULIMA WA MPUNGA SAME WAHOFIA KUFA KWA MRADI KUTOKANA NA USIMAMIZI MBOVU
HALMASHAURI ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, imeshutumiwa kushindwa kuongeza ufanisi wa matumizi bora ya kilimo cha umwagiliaji wa mpunga kwa kuboresha miundombinu katika skimu zilizopo wilayani humo, na kuwafanya wakulima kuingiwa na hofu ya kufa kwa mradi wa kilimo hicho uliopo katika Kata ya Ndungu kutokana na kuwepo kwa usimamizi mbovu uliopo sasa.
Wananchi wa Kata hiyo wamebainisha hayo na na kudai kwamba kumekuwepo na utata wa usimamizi wa mradi huo kwa muda mrefu unaosababishwa na uhaba wa wataalam kwenye skimu pamoja na miundombinu mibovu na kupelekea kujitenga kwa baadhi ya wakulima kutokana na baadhi yao kurubuniwa kuwa waendelea kutumia mbinu za zamani katika uzalishaji wa zao hilo licha ya mradi huo kusimamiwa na halmashauri wenye zaidi ya miaka 25.
Imeelezwa kuwa zipo skimu mbili za kisasa za umwagiliaji katika mkoa huo (Mradi wa Umwagiliaji wa Lower Moshi (1100ha) na Mradi wa Umwagiliaji Ndungu (680 ha), na kuwa licha ya wakulima hao kutoa taarifa kwa viongozi wa Kata na Halmashauri, viongozi wanasuasua kuunasua mradi huo katika hali iliyopo sasa na hivyo kuitaka Serikali ya Wilaya kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.
Diwani wa Kata hiyo, Khatibu Mrindoko na Diwani wa Viti maalum tarafa ya Ndungu, Veronica Mmbaga, wamesema kwamba mradi huo una hali isiyoridhisha na kwamba zinahitajika jitihada za halmashauri ili kuunusuru kilimo hicho.
“Kuna mbegu ya Kijapani iliyokuwa inatumika katika hiki kilimo ilikuwa haina mazao mazuri lakini hii mpya ya Supersaro ambayo inatumiwa na wakulima kwasasa iliyoanza kutumiwa tangu mwaka jana imeongeza uzalishaji na bei ya kilogram moja ya mchele ni 1200 kwa hapa kijijini kwahiyo wanahaki kulalamikia serikali kwa madhaifu yaliyopo japo kuwa wanapata maji ya kutosha katika kilimo”.
Kufuatia hofu hiyo Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira ya Halmashauri hiyo imeagiza kitengo cha ukaguzi wa ndani kukagua hesabu ya mashine ya kukoboa mpunga iliyopo katika skimu ya umwahiliaji ili kuona uendeshaji wake kutokana na utata wa fedha zinazopatikana katika mashine hiyo.
Taarifa za awali kutoka Ofisi ya Mkaguzi wa ndani katika halmashauri hiyo zimebainisha kuwa mradi huo hauna Meneja na mkoboaji mkuu na kwamba kukosekana kwa fomu ya ruhusa za watumishi wa mradi wanapokuwa nje ya eneo la kazi kumezorotesha utendaji kazi kwa kiasi kikubwa.
Imeelezwa kuwa mradi huo unadeni la umeme lenye kufikia zaidi ya milioni 7.5 ikilinganishwa na mapato ya milioni 6.3 yanayopatikana kulingana na uzalishaji wa kazi hiyo, huku nyaraka za fedha za uendeshaji ya ofisi zitokanazo na pumba zikikosekana na kugubikwa na utata wa hali ya juu.
Afisa Kilimo na Umwagiliaji wa wilaya hiyo, Majid Kajemela, amekiri kuwepo kwa matatizo hayo na kwamba halmashauri kwa kutambua changamoto hiyo imesimamia wakulima hao na kuwaunganisha kwa pamoja kuunda umoja ambao wanajukumu la kusimamia mashamba na kwamba kupitia umoja huo wanachangia kiasi cha milioni 80 kwa mwaka ambazo zinatumika kwa ajili ya ukarabati na matengenezo ya skimu.
“Kwa sasa tumeandaa wataalam wa kutosha wa ugani kutokana na hapo mwanzo kuwa na wataalam wawili kama ulivyosema lakini kwasasa wapo nane na uzalishaji wa zao hilo umeongezeka kwani kwa hekta wanapata tani 6.5 kwa ekari moja tofauti na hapo awali” alikaririwa Kajemela
Akizungumzia suala la utata wa fedha zinazodaiwa kupotea katika mazingira ya kutatanisha (zaidi ya milioni 7.5), amesema kwasasa wanahitaji kufanyia suala hilo uchunguzi wa wa kina huku akisema malalamiko ya kinu cha kukobolea mpunga kuharibika lipo katika ukarabati wa matengenezo madogo na kwamba pamoja na matengenezo hayo bado kinu mashine hiyo inaendelea kufanya kazi.
Wilaya ya Same inatajwa kuwa ni miongoni mwa wilaya tajiri mkoani humo kutokana na kuwa na madini mengi, ardhi yenye rutuba na yenye kustawisha mazao ya aina tofauti na yenye thamani kubwa na msitu wa Shengena wenye madini mengi na mazao ya miti, ambapo kilimo kikubwa kinacholimwa wilayani humo (maeneo mengi ni milimani) kimetajwa kuwa ni kilimo cha Tangawizi chenye uzalishaji wa asilimia (70%) ya Tangawizi inayozalishwa nchini na kilimo cha mpunga kinachoongoza kwa kushika nafasi ya pili baada ya Moshi Vijijini mkoani humo.
CREDIT: FIKRA PEVU
Post a Comment