PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: WAHUDUMU WA AFYA WENYE LUGHA CHAFU KWA WAGONJWA KUADHIBIWA
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Mkuu wa Wilaya ya Songea, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Joseph Mkirikiti, ametishia kupambana na watumishi wa afya katika...
 


Mkuu wa Wilaya ya Songea, ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Joseph Mkirikiti, ametishia kupambana na watumishi wa afya katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, watakaoripotiwa kutoa lugha chafu kwa wagonjwa wanaofika kutibiwa hospitalini hapo.

Awali wananchi wa Wilaya hiyo wamekaririwa  wakisema kumekuwepo na kero kubwa wanayokumbana nayo katika hospitali hiyo kwa baadhi ya wahudumu kutumia lugha chafu katika eneo la mapokezi, ukosefu wa dawa pamoja na madaktari kutokaa katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa kwa muda mrefu huku wakiendelea kuteseka.

Imeelezwa kuwa mbali na wananchi hao kutoa taarifa kwa baadhi ya viongozi husika pindi wanapokutana na kero za namna hiyo, bado tatizo hilo limeonekana kuwa gumzo baada ya kushindwa kutatuliwa na Ofisi ya Mganga Mfawidhi na kuwa baada ya kupiga kelele za muda mrefu juu ya suala hilo wamepewa namba za simu za mkononi kwa ajili ya kuripoti matukio hayo pindi wanapokutana na kadhia hiyo lakini bado suala hilo halijatatuliwa.

“Tumeanza kuchukua hatua na tunaripoti katika ngazi husika bila kuchelewa ili waweze kuwabana wauguzi wanaofanya hivi kwani sasa umefika wakati wa kuambiana ukweli, kama mtu anaona kuhudumia umma kunampotezea wakati basi akaanzishe Zahanati yake ambapo huko atakuwa huru kutumia lugha chafu kulingana na wateja wake”.

Wamesema madaktari wa hospitali hiyo hutumia muda mwingi kwenda kunywa chai na chakula cha mchana, kwa kutoka pamoja kwa makundi na hivyo kusababisha wagonjwa kusota kwa muda mrefu bila huduma.

Kwa upande wake, Mkirikiti, ameeleza kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa na serikali katika hospitali hiyo hayatakuwa na maana endapo kero hizo zitaendelea kudumu na kusababisha wananchi kupata huduma kwa mateso makubwa na kuwa mhudumu yeyote atakayepatikana na kosa la kutoa lugha chafu kwa wagonjwa atapambana na mkono wa sheria pasipokujua watoa taarifa.

Hata hivyo, amewataka wananchi hao kufika katika ofisi yake kwa ajili ya kufikisha matatizo yao ikiwemo tatizo hilo, ili kushirikiana kwa pamoja katika kuwezesha kuwakamata wahusika huku akiahidi kuwachukulia sheria wahudumu wote watakaobainika kutenda kosa hilo.

Kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kukimbia kupata matibabu katika hospitali za maeneo wanayoishi, kutokana na huduma mbovu zinazotolewa hospitalini pamoja na lugha chafu zinazotolewa na wahudumu wa hospitali hizo

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top