PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: RASIMU YA KATIBA MPYA ILIYOPENDEKEZWA KUWASILISHWA BUNGENI SEPTEMBA 24 MWAKA HUU
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
Na Benedict Liwenga na Magreth Kinabo. RASIMU ya Katiba Mpya iliyopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba Sep...





Na Benedict Liwenga na Magreth Kinabo.

RASIMU ya Katiba Mpya iliyopendekezwa inatarajiwa kuwasilishwa katika Bunge Maalum la Katiba Septemba 24, mwaka huu.


Mabadiliko hayo yametangazwa leo jioni na Katibu wa Bunge Maalum la Katiba, Yahya Khamis Hamad wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.


Aidha Katibu huyo amesema uamuzi wa mabadiliko hayo, umetokana na kufanyika kikao baina ya Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi.


Hata hivyo Katibu huyo amesema kuwa kazi ya uandishi wa Rasimu hiyo imeshakamilika na kazi iliyobakia ni kuipitia kwa makini, hali iliyosababisha mabadiliko ya uwasilishaji wa Rasimu hiyo katika Bunge hilo, uliopangwa kufanyika hapo kesho Septemba 22, mwaka huu.


“Uwasilishwaji wa Rasimu ya Katiba inayopendekezwa sasa utafanywa siku ya Septemba 24, mwaka huu, ” alisema Katibu wa Bunge hilo.


“Kamati ya uongozi imeona kuwa ni busara na kupewa siku mbili kwa ajili ya kuipitia upya ile kazi ambayo wameifanya ili kufikia tarehe 24 kutoa kitu makini, napenda niwahakikishie wananchi kuwa kitu kizuri kinakuja.


Aliongeza kuwa Kamati ya Uongozi ya Bunge hilo, inatarajia kukabidhiwa Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa tarehe 23 Septemba, mwaka huu kutoka kwa Kamati ya Uandishi wa Bunge hilo.


Aidha, Katibu huyo ameeleza sababu ya uairishwaji wa uwasilishwaji wa Rasimu hiyo Bungeni hapo kutokana na ugumu, umakini na uzito wa kazi yenyewe.


“Tulikuwa tumepanga hapo tokea awali kufanya kikao na Kamati ya Uongozi asubuhi tukafanya mchana na hata jioni kila wakati Kamati ya Uandishi ikawa bado haijamaliza hiyo kazi na tulivyofanya kikao cha Kamati ya Uongozi hii jioni tukamuita Mwenyekiti wa Kamati ya uandishi akaonyesha kwamba hiyo kazi walikuwa wakiifanya usiku na mchana na hadi sasa wamesema wamemaliza kuandika.


“Lakini kutokana na namna walivyokuwa wakiifanya hiyo kazi kwa uharaka na ingawa walikuwa wakiifanya kwa umakini lakini wanahitaji muda wa kuanza kuipitia kwa makini zaidi kuanzia mwanzo mpaka mwisho hivyo wakaomba wapewe muda wa siku mbili ya kesho na keshokutwa ili kuweza kuipitia kazi hiyo kwa umakini,”alisema.


Katibu wa Bunge hilo, aliongeza kwamba mabadiliko hayo hayataweza kuathiri upigaji kura uliopangwa kufanyika Septemba 29 hadi 2 Oktoba mwaka huu.


“Tumeacha siku ya Septemba 29, mwaka huu ili iwe siku ya kuanza kupiga kura na tumalize 2 Oktoba, mwaka huu ili tuhakikishe kwamba Oktoba 4 , mwaka tumemaliza hili zoezi,” alisisitiza.


Aidha Katibu huyo alifafanua kuwa ratiba kuhusiana na masuala hayo ataitoa kesho.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top