Mkuu
wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema
akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho miaka 50 ya
chuo hicho yanayoendelea jijini Dar es salaam.
Hatua
iliyochukuliwa na uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam
(CBE) kuendelea kuweka msisitizo katika usimamizi wa maadili kwa
wanafunzi imeanza kuzaa matunda kufuatia kuogezeka kwa ufaulu wa masomo
kwa wanafunzi wanaosoma chuoni hapo.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na mkuu wa Chuo cha Elimu ya
Biashara Dar es salaam (CBE) Prof. Emanuel Mjema wakati akitoa ufafanuzi
kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho yanayoendelea ya chuo hicho
kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake Januari, 1965.
Amesema
suala la usimamizi wa maadili kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia
chuoni hapo limepewa kipaumbele kikubwa na uongozi wake tofauti na miaka
iliyopita hali ilinayokifanya chuo hicho kuwa mfano wa kuigwa vyuo
pamoja na taasisi nyingine za elimu ya juu hapa nchini.
“Chuo
chetu sasa ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine hapa nchini kwa sababu
tumeweza kusimamia suala la maadili hasa uzingatiaji wa mavazi yenye
staha kwa wanafunzi hali iliyoongeza heshima kwa chuo chetu”.
Mbali
na suala la usimamizi wa mavazi kwa wanafunzi Prof amesema chuo hicho
kimeendelea kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi na jamii nzima
inayoingia na kutoka katika mazingira ya chuo hicho, kuimarisha ukaguzi
katika maeneo yote muhimu ya kuingilia wanafunzi na kuwatambua wanafunzi
wote kwa kutumia vitambulisho vyao.
Amefafanua
kuwa chuo hicho sasa kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka
50 tangu kuanzishwa kwake yakiwemo mabadiliko na maboresho makubwa
katika sekta ya elimu hasa ongezeko la udahili wa wanafunzi, ongezeko
la fani za masomo na kampasi za chuo hicho katika mikoa mingine nchini
ikiwemo Dodoma, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.
Prof.
Mjema amefafanua kuwa chuo cha CBE sasa kinatimiza miaka 50 kikiwa chuo
pekee Afrika ya Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi
za Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.
“Chuo
hiki pekee ndicho kinachotoa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya vipimo, ni
chuo kinachotegemewa sana katika ukanda huu wa nchi za Afrika Mashariki
na SADC” Amesisitiza.
Ameeleza
kuwa tangu kuanzishwa kwake Januari, 1965 na aliyekuwa Rais wa kwanza
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ,
chuo hicho kimepata mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi
wanaodahiliwa kila mwaka kutoka wanafunzi 25 mwaka 1965 hadi 14,000
mwaka 2014.
Mafanikio
mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi
kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD)
chuoni hapo pamoja na chuo kuanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo
vikuu vingine nje ya nchi kikiwemo Chuo Kikuu cha Eastern Finland katika
utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi
za SADC.
Ameongeza
kuwa katika kipindi cha miaka 50 ya chuo hicho idadi ya kampasi
imeongezeka kutoka 1 ya jijini Dar es salaam na kufikia 4 katika mikoa
ya Mbeya, Mwanza, Dodoma na upande wa Zanzibar huku idadi ya wahitimu wa
chuo hicho ikiongezeka kwa kipindi chote ikiwa zaidi ya wanafunzi Laki
moja.
Aidha,
katika kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu
inayotolewa kwa wanafunzi katika maadhimisho hayo,chuo kinaandaa matukio
mbalimbali ya ukusanyaji wa fedha kupitia chakula cha hisani,
matembezi, midahalo ya wasomi na mikutano wanafunzi wahitimu wa chuo
hicho Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Dar es salaam kwa ajili ya
ujenzi wa maabara, vyumba vya mihadhara ya wanafunzi na madarasa.
Pia
chuo hicho kinaandaa mafunzo ya ujasiriamali yatakayotolewa kwa jamii
ikiwa ni sehemu ya kurudisha huduma kwa jamii kwa kuwajengea uwezo
wajasiriamali, na kuwajengea uelewa wanafunzi ili waweze kuwa na
uchaguzi sahihi wa hatima yao ya baadaye pindi wanapohitimu mafunzo.
Post a Comment