Malkia wa muziki wa R&B, Lady Jay Dee amedai kuwa maadui zake wamebuni njia mpya ya kumwangusha, baada ya zile za awali kutofanikiwa.
Katika waraka mrefu aliouandika katika mtandao wa
facebook, Lady Jay Dee alisema watu wasiopenda mafanikio yake wamekuwa
wakitumia mbinu mbalimbali kumwangusha, lakini hata hivyo wameshindwa.
Jay Dee analalamikia habari iliyoandikwa juu yake
kuwa amekuwa katika uhusiano mpya na kijana aliyemzidi umri, jambo
analosema halina ukweli.
Habari hiyo inahusishwa na kile kilichodaiwa kuwa
mwanamuziki huyo ameachana na mume wake, Gadner G Habash, ambaye ni
mtangazaji wa kituo cha redio Times FM.
Jide ameandika: “Hata kama nimeachana na mume
wangu, siyo sababu ya kunihusisha katika uhusiano na mwanamume mwingine
yeyote. Habari hii imenivunjia heshima. Nafikiri lengo la uzushi huu ni
kumfanya Lady Jaydee aonekane mtu asiyefaa.”
Habari hiyo ilipambwa na picha ambazo alizipiga mwenyewe kwa kutumia simu ya mume wake.
Aliongeza: “Ni vizuri kuzusha vitu ambavyo angalau
unavijua, hizi picha zilipigwa kwa simu ya Gadner ambaye mnasema
nimeachana naye, hamuoni kama mnawadanganya watu?”
Aliongeza kuwa huenda aliyeanzisha habari hizo ameona zile ambazo zilikuwa zikivuma wakati fulani, zimeshuka chati.
Alihoji: “Je, wimbo Jay Dee mgumba, Jay Dee tasa umeshuka chati ndiyo maana mmeamua kuleta mwingine?”
Hata hivyo, alisema lengo la wanaoanzisha uzushi
juu yake ni kumdhoofisha lakini anaamini jinsi alivyoshinda vita ya
kwanza, atashinda tena vita ya pili. “Hata kama ndoa yangu haiko sawa,
niacheni.
Lakini isiwe sababu ya kuendelea kunichafua kwa
maneno ya kizushi. Siyo lazima niandikwe, kwa sababu nilikuwapo kabla ya
kuandikwa sana... nitaendelea kuwapo bila kuandikwa.”
Post a Comment