PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: JK APOKEA HOJA ZA UKAWA JUU YA MWENENDO WA BUNGE LA KATIBA
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  ...

Baada ya kilio cha muda mrefu cha makundi mbalimbali ya kijamii kumtaka Rais Jakaya Kikwete kukutana na vyama vya siasa ili kuokoa mchakato wa kutengeneza katiba mpya ambao kwa sasa upo njiapanda, hatimaye ameitikia wito huo na kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kupitia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) mjini Dodoma jana.
Mchakato huo uliofikia hatua ya Bunge Maalum upo njiapanda baada ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia kwa madai kuwa kinachojadiliwa ni tofauti na kilichomo katika Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Ukawa huundwa na wajumbe watokao katika vyama vikuu vya upinzani nchini vya Chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Baada ya Ukawa kususia Bunge hilo kumekuwa na hisia tofauti miongoni mwa jamii na makundi mbalimbali ya kijamii, huku baadhi wakimtaka Rais Kikwete kulisitisha na wengine wakiwasihi Ukawa kurejea bungeni kuungana na wenzao kutengeneza katiba mpya.
Msimamo wa Ukawa ulikuwa ni kukutana na Rais Kikwete ili kuzungumzia suala hilo na kwamba hawatarejea bungeni hadi hapo watakapohakikishiwa kuwa itakayojadiliwa katika Bunge hilo ni Rasimu iliyowasilishwa na Tume, ikiwa ni pamoja na kuzingatia maoni ya wananchi  yaliyotaka muundo wa muungano wa serikali tatu.
Rais Kikwete alikutana na viongozi wakuu wa vyama vya siasa katika ikulu ndogo mkoani Dodoma.
Awali, kabla ya kikao hicho, baadhi ya viongozi wa Ukawa, wakiwamo Mwenyekiti wa CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia,  Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa na Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF,  Magdalena Sakaya na viongozi wengine wa vyama vya siasa waliwasili mjini hapa kwa ndege ndogo ya kukodi saa 4:15 na baadaye kuungana na wenzao waliokuwa tayari mjini hapa na kufanya kikao kifupi kabla ya kuelekea Ikulu kukutana na Rais Kikwete.
Mbali na viongozi wa Ukawa, viongozi wengine wa vyama waliokuwapo ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema, Mwenyekiti wa UPDP, Fahami Dovutwa.
Baada ya kikao hicho, viongozi hao wa vyama walikutana na Rais Kikwete kwa takribani saa tatu,  kuanzia saa 6: 20 mchana na baada ya kikao hicho kumalizika,  viongozi hao wa vyama waliondoka ikulu na kufanya kikao chao cha faragha kwa muda wa saa moja.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chao, Mwenyekiti wa TCD, Cheyo, alisema mazungumzo yao na Rais Kikwete yalikuwa mazuri na kwamba wamezungumzia ajenda kuu mbili.
Alisema ajenda moja ilihusu mchakato wa katiba mpya na nyingine ilihusu uchaguzi mkuu ujao mwakani.
Hata hivyo, Cheyo, alikataa kuzungumzia kwa undani juu ya masuala hayo waliyozungumza na Rais.
Mwenyekiti huyo wa TCD alisema wamekubaliana na Rais Kikwete kukutana tena Septemba 8 mwaka huu mjini Dodoma ili kutoa nafasi kwa pande zote kutafakari waliyozungumza kabla ya kufikia makubaliano.
KAMATI TCD
Cheyo alisema baada ya kikao hicho na Rais, TCD imeunda kamati ndogo itakayoongozwa na Mbatia na itakuwa na kazi ya kupitia waliyozungumza na Rais na kutoa mapendekezo na baada ya hapo wajumbe wote wa TCD watakutana Septemba 5, mwaka huu ili kupokea taarifa ya kamati hiyo na kisha kutafuta msimamo wa pamoja watakaokwenda nao kwenye mazungumzo na Rais Kikwete.
Aliwataja baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni  Kinana na Prof. Lipumba.
Aprili 16, mwaka huu wajumbe wanaounda Ukawa ambao wengi ni kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia vikao vya Bunge hilo wakitaka msingi wa mapendekezo ya Rasimu ya Katiba usibadilishwe, wakipinga uamuzi wa CCM kutaka kuingiza mfumo wa serikali mbili badala ya tatu zilizopendekezwa katika Rasimu.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top