Baadhi ya wajumbe wa Bunge
Maalumu la Katiba wamesema
wala rushwa pamoja na wahujumu
uchumi adhabu yao iwe ni
kunyongwa.
Wametaka Katiba mpya
inayoenda kuandikwa itamke hivyo
ili kufanya viongozi wa kisiasa
kuogopa kama ilivyo kwenye nchi
nyingine.
Sababu ya wajumbe hao
kupendekeza jambo hilo ni
kwamba uhujumu uchumi na
rushwa nchini limekuwa tatizo
kubwa kwa viongozi.
Kutokana na ukiukwaji huo wa
maadili, wamesema
umefika wakati wa kuweka bayana
suala hilo kwenye sheria mama.
Miongoni mwa waliochangia ni
Paul Makonda aliyesema suala
hilo likiwekwa bayana, litaokoa
fedha nyingi za walipa kodi
ambazo kwa sasa baadhi ya
viongozi wanazichota na kwenda
kuzihifadhi nje ya nchi.
Pia alipinga kuruhusu viongozi wa
nchi kufungua akaunti nje ya nchi.
“Kwa nini viongozi hao washindwe
kuhifadhi fedha zao ndani ya nchi,
wanafanya biashara gani hadi
wakafungue benki nje ya nchi?
“Tusiruhusu jambo hili na
napendekeza kwamba kiongozi
atakayebainika amekula rushwa
na kuhujumu uchumi huyo
anyongwe,” alisema Makonda.
Yusuf Singo pia alisema maadili
yanazidi kuporomoka kwa
viongozi, jambo linalorudisha nchi
nyuma. Alitaka Katiba isisitize
maadili kwa kada hiyo na ambao
watakiuka wanyongwe.
Alitoa mfano wa Japan kuwa
kiongozi wa kisiasa
anapochunguzwa kwa kujihusisha
na rushwa anatoa machozi kwa
sababu hajui hatima yake.
“Tunataka na sisi ifike wakati
kiongozi akianza kuchunguzwa
atoe machozi,” alisema.
Dk Mary Mwanjelwa katika
mchango wake alisema rushwa
imekuwa adui mkubwa wa
maendeleo ya Watanzania.
Alisema isipopingwa kuanzia
kwenye Katiba, nchi itakuwa
inajichora.
Alisema Bunge halitaeleweka
kama halitaweka jambo hilo
kwenye Katiba, kwa sababu
wananchi wengi wameteseka
ndani ya nchi yao kwa sababu ya
rushwa.
Alisema pia wapo viongozi wengi
wasio na maadili na ndiyo maana
wanajihusisha na vitendo vya
rushwa.
Kwa upande wake, Profesa Mark
Mwandosya alisema tatizo la
rushwa haliwezi kutenganishwa na
haki za binadamu kutokana na
kukosesha wananchi maendeleo.
Profesa Mwandosya alisema Katiba
lazima itambue adui wa haki za
wananchi ni rushwa.
Alipendekeza suala hilo
litambulike kikatiba na serikali
zote mbili zitunge sheria kali za
kupambana na rushwa
kuhakikisha wananchi wanapata
haki zao za msingi bila kutoa wala
kupokea rushwa.
Naye Gerison Lwenge alisema
Katiba itambue jambo hilo na
ikemee vikali kwa wanaotoa na
wale wanaopokea.
Alisema kwa ahli ilivyo,
wanaobanwa zaidi ni wale ambao
wanapokea na akapendekeza
sheria kali zitungwe kubana pia
wanaotoa.
Alishauri Kamisheni isimamie
suala hilo la rushwa badala ya
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru).
Kwa mujibu wa Lwenge,
Kamisheni ni chombo kikubwa
zaidi kuliko ilivyo kwa taasisi.
Alisema kazi yake itakuwa ni
kuzuia zaidi na si kutibu pekee.
Jesca Msambatavangu alisema
Takukuru wanafanya kazi vizuri na
walishindwa kupambana na
rushwa kwa vile hawana uhuru wa
kutosha.
Alisema kama Takukuru wakipewa
meno kupitia Katiba mpya,
watashughulika kwa uhuru zaidi
katika kupambana na tatizo la
rushwa nchini.
Post a Comment