Baadhi ya wananfunzi wa Shule ya Msing Orbomba wakiwa wanajisomea majarida mbalimbali |
NA: Andrea Ngobole, Longido
Kati ya watoto kumi wa
shule ya Msingi Orbomba wilayani Longido Mkoani Arusha ni watoto sita tu ambao
hufika shule na kuhudhuria masomo, hii ni Zaidi ya asilimia arobaini ya watoto
wote wanaotakiwa kufika shule. Njaa imesababisha wanafunzi washindwe kuhudhuria
masomo.
Hali iliyopo katika
shule hii ndiyo picha halisi iliyopo katika
shule za msingi 43 zilizopo wilayani Longido. Vijiji vingi vya wilaya ya
Longido vinakabiliwa na ukame na hatimaye kuleta njaa kali katika familia kiasi
kwamba watoto wanashindwa kwenda shule.
Upatikanaji wa lishe bora na salama kwa matumizi
ya wanadamu ni moja ya huduma ya lazima kwa maisha na ustawi wa wanadamu. Kwa
mujibu wa Sera ya Lishe Bora ya mwaka 1992 inasema lishe ni mchakato wa chakula
mwilini na ni vyema kila mwanadamu kuzingatia makundi matano ya chakula
yanayomsaidia kuwa na afya bora ambayo ni nafaka, matunda, mbogamboga, nyama na
mafuta ili kuepukana na madhara ya utapiamlo.
Katika wilaya ya Longido wanavijiji wengi hawana
uwezo wa kupata mlo kamili kutokana na hali ngumu ya maisha waliyonayo iliyosababishwa
na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Familia nyingi za
vijiji vya, Kimokowa, Ranchi, Kitumbeine, Ortepesi, Orbomba, Ranchi, Orpukeli, Kitumbeine, Ildonyo,
Noondoto na Gilailumbwa
hazimudu kununua chakula cha kulisha familia zao kutokana na mifugo yao kufa kwasababu ya ukame uliyoikumba wilaya hiyo misimu minne mfululizo kuanzia mwaka 2020-2023
Norikidoti Kimamwe
(42) mkazi wa kijiji cha Kitumbeine anasema Ukame umepelekea kukosa mifugo na
hawapati chakula kwa ajili ya familia.
“Yaani kwa siku
tunakula mlo mmoja tu kwani bei ya chakula ni ghali sana hatuwezi kumudu
gharama zake debe la mahindi sokoni ni shilingi 24000 sasa kiasi hicho ni
kikubwa sana kwangu na familia yangu”. alisema
Jacob Kipamba (27) mkazi wa kijiji cha Ranchi anasema ukosefu wa
chakula ni mkubwa sana kijijini hapo kwa sababu wanategemea mifugo wauze ndiyo
wanunue chakula, ukame umepelekea ng’ombe kufa, alikuwa na ng’ombe 16 ambapo
walikufa 8 amebakiwa na ngombe 8 na mbuzi wanne.
“Mimi kwa kuwa nafanya kazi ya ulinzi katika ofisi ya kijiji
kidogo napata mshahahara unaowezesha kununulia familia chakula, ila kama
unavyojua ukubwa wa familia ukipata chakula mtoto wa kaka au dada huwezi
kumuona ana njaa ukaacha kumsaidia,” alisema
Familia hizi ni sehemu ya jamii kubwa ya wananchi wa wilaya ya
Longido waliokumbwa na baa la njaa baada ya mifugo yao kufa kwa ukame
uliosababishwa na mabadiliko ya tabianchi hali iliyosababisha mahudhurio hafifu
na utoro kwa wanafunzi wa shule za msingi.
Wazazi hawa wanadai watoto wao wanashindwa kwenda shuke kwa sababu wanakosa hata uji wa kuwapikia asubuhi na kwenda shule bila kutia kitu chochote tumboni na hivyo njaa inawapelekea kusikia kizunguzungu na kushindwa kuhudhuria shule kwa ajili ya masomo.
Pamoja na serikali kupeleka mahindi ya bei nafuu katika wilaya hii
wakazi hao wanashindwa kununua mahindi hayo yanayouzwa shilingi elfu themanini
kwa gunia moja la kilo mia moja kwani masharti ya serikali ni kuuza kwa gunia
na siyo kwa debe moja.
Bei ya mahindi Katika soko la Longido yanauzwa na wafanyabiashara
wa kawaida kwa shilingi 135,000 kwa gunia na bei ya debe moja la mahindi
linauzwa kati ya shilingi 24000/= mpaka 30,000/= ambapo kama serikali ingeuza
mahindi yake kwa debe moja wangeuza kwa shilingi 16,000/=
Mwalimu wa Shule ya Msingi
Orbomba ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa kuwa siyo msemaji wa shule na mkuu hakuwepo
anasema kijijini hapo kuna njaa sana hali ambayo inaathiri utendaji kazi wao
darasani kwani wanafunzi wamekuwa watoro hawaji shule kwa sababu ya njaa na pia
hata wanaokuja ikifika mchana wanatoroka kwani wanashindwa kuvumilia njaa.
“Kimsingi mahudhurio ya watoto shuleni hapa ni
madogo kutokana na njaa, walimu pia tunashindwa kuendelea na vipindi vya mchana
kwani usikivu na uelewa wa watoto unakuwa mdogo sana kwa sababu ya njaa,”
anasema
Anasema wameongea na wazazi wawe wanachanga shilingi
18,000 kwa muhula ili waanze utaratibu wa kuwapikia chakula hapo shuleni ila
bado mwitikio siyo wa kuridhisha kwani nao wanasema hawana pesa.
Shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 445 ambapo
mahudhurio ni wastani wa asilimia 60 na asilimia 40 hawahudhurii shule kabisa
kutokana na njaa.
Aidha baadhi ya watoto hao hulazimika kwenda mjini kuomba chakula kwa wasamaria wema ili waweze kupeleka nyumbani kwa ajili ya mlo wa familia.
Afisa Elimu msingi wilaya ya Longido, Deusdedit Bimbalirwa amekiri kumekuwepo na utoro katika shule za msingi kutokana na tatizo la njaa.
Bimbalirwa alisema kuna baadhi ya wanafunzi wameondoka na wazazi wao kwenda kutafuta malisho ya mifugo.
"Kawaida hizi jamii ukame unapokuwa mkali huwa wanahama na mifugo sasa na wanafunzi wanahama nao" alisema
Alisema pia kutokana na njaa wanafunzi wanapungua madarasani na kurudi majumbani.
Hata hivyo, alisema tayari Halmashauri ya Longido imeanza kulifanyiakazi tatizo hilo kwa kupeleka mashuleni na vijijini chakula cha msaada na bei nafuu.
"Tayari chakula cha msaada kimeanza kupelekwa mashuleni lakini pia chakula cha bei nafuu ili kukabiliana na hali hii" alisema
Kutokana na uhaba wa chakula unaokabili familia nyingi wilayani hapa, baadhi ya mashirika kadhaa yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza miradi katika wilaya hii ya Longido yameanza kusambaza chakula cha bure kwa kaya zilizokumbwa na njaa.
Kaimu Afisa Kilimo wa
wilaya ya Longido, Mariam Fivawo anasema ukame umesabisha uhaba wa chakula
katika maeneo mengi ya wilaya hiyo ambayo asilimia 95 ya wananchi wake ni
wafugaji.
Post a Comment