Na Fredy Mgunda,Iringa.
MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuwajengea uwezo wataalamu wa ukaguzi wa dawa na vifaa tiba katika Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kwa lengo la kuboresha ufanisi wa kazi wawapo kazini ili kulinda afya za watumiaji wad awa na vifaa tiba.
Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo kaimu katibu tawala mkoa wa Iringa,Elias luvanda alisema kuwa ni kielelezo tosha kuwa wakaguzi ngazi ya Halmashauri mnathamini mchango wa TMDA katika kuwapa elimu kuhusu namna bora ya kutekeleza majukumu na kulinda Afya za wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa taifa letu la Tanzania.
Luvanda alisema kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya, yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi na Taasisi hiyo imeundwa chini ya sheria ya Dawa na Vifaa Tiba sura 219.
Alisema kuwa majukumu yanayofanywa na TMDA na yale yaliyokasimishwa kwenu, lengo lake ni lilelile la kulinda afya ya jamii kwa kuzuia athari zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
“Kwa kutambua jukumu zito la TMDA, Serikali iliona ni vema kukasimu baadhi ya madaraka na majukumu yao kwa Halmashauri kwa lengo la kusogeza karibu na wananchi huduma za udhibiti wa ubora na usalama wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi”alisema Luvanda
Luvanda aliwataka watendaji wote kufanya kazi kwa kutoa taarifa zilizo sahihi kwa wakati unatakiwa ili kurahisisha utendaji wa taasisi hiyo hivyo Mwongozo wa Kukasimu Madaraka na Majukumu umebainisha wazi kuwa taarifa za utendaji kazi za robo mwaka na taarifa za ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa zinazodhibitiwa katika soko zinatakiwa kuandaliwa na kutumwa TMDA kupitia viongozi wa ngazi ya Halmashauri.
“Ni mategemeo yangu kwamba mafunzo haya yatatoa maelekezo ya namna ya kuboresha utendaji kazi wenu, na kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara kuwa, wakaguzi wa Halmashauri wanatumia nguvu nyingi nyakati za kaguzi ambazo husababishwa na kutokutoa elimu kwa wateja (wafanyabiashara) Hivyo kukinzana na utaratibu wa ukaguzi wa TMDA ambao umejikita zaidi katika kuelimisha na kuwezesha” alisema Luvanda.
Alimalizia kwa kusema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itafanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo na makubaliano yatakayowekwa ili kuhakikisha wananchi wanahakikishiwa upatikanaji wa bidhaa bora na salama.
Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya kati Sonia Mkumbwa alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwaongezea ujuzi wakaguzi ili waweze kufanya kazi ya ukaguzi kwa kuzingatia sheria.
Mkubwa alisema kuwa wakaguzi watatekeleza kazi zao kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kama zilivyotolewa na TMDA kama vile Kufanya ukaguzi wa maeneo yanayohusika na utunzaji, uuzaji na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Kufanya ufuatiliaji na kutoa taarifa za ubora na usalama wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi katika soko.
Aliongeza kuwa wakaguzi watatakiwa kuchukua sampuli za bidhaa zinazodhibitiwa kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara pale inapohitajika na kufanya ufuatiliaji wa madhara/matukio yanayohisiwa kusababishwa na matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Mkumbwa alisema kuwa wakaguzi wanatakiwa kufanya uhakiki wa bidhaa zisizofaa kwa matumizi kabla ya uteketezaji kwa kujaza fomu ya uhakiki (Kiambatisho Na.7) baada ya mawasiliano na Ofisi ya Kanda ya TMDA na kusimamia zoezi la kuteketeza bidhaa ambazo hazifai kwa matumizi baada ya uhakiki na kisha kujaza fomu ya uteketezaji (Kiambatisho Na. 8) na kuiwasilisha ofisi ya Kanda ya TMDA kwa ajili ya kuandaa cheti cha uteketezaji.
Alimazia kwa kuwasema kuwa kila Halmashauri itaandaa na kuwasilisha taarifa za utendaji kazi kwenye Ofisi za TMDA za Kanda na kuwasilisha nakala kwa Katibu Tawala wa Mkoa ambazo ni taarifa ya utendaji ya robo mwaka na taarifa ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za udhibiti wa ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa katika soko.
Post a Comment