PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: NDOA ZA UTOTONI ZINAVYOATHIRI USTAWI WA MTOTO WA KIKE WILAYANI LONGIDO
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Mtoto Mesoni Kashiro (15) mkazi wa kijiji cha Gilailumbwa, aliyejeruhiwa kwa kipigo na mumewe Namendea Lesiria kwa kosa la kumwaga dawa ya...

 

Mtoto Mesoni Kashiro (15) mkazi wa kijiji cha Gilailumbwa, aliyejeruhiwa kwa kipigo na mumewe Namendea Lesiria kwa kosa la kumwaga dawa ya mifugo alipofikishwa hospital na watetezi wa haki ya mtoto kwa ajili ya kupata matibabu


Na: Mwandishi wetu, Longido. 

Wakati wanaharakati wa kutetea haki za wanawake na watoto wakiwa katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia mwaka 2022 ambazo zitahitimishwa Desemba 10, ndoa za utotoni bado ni changamoto kubwa katika jamii za kifugaji nchini, ikiwamo wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha


Watoto wadogo wenye umri chini ya miaka 15 bado wanaolewa kwa kasi, hivyo kuathiri ndoto za maisha yao, ikiwemo kupata haki ya kusoma na wengi wakiishia kufanyiwa ukatili maishani mwao.

Lipo tukio la Septemba 22 mwaka huu, lililohusisha mtoto Mesoni Kashiro (15) mkazi wa kijiji cha Gilailumbwa, kujeruhiwa kwa kipigo na mumewe Namendea Lesiria kwa kosa la kumwaga dawa ya mifugo.

Tukio hilo lilivuta hisia za watetezi wa haki za watoto kutaka uchunguzi wa kukomeshwa ukatili huu, lakini kumbe tatizo ni kubwa zaidi na sio kwa Mesoni tu.


Pamoja na nchi kupiga kelele na kuzua mijadala ya hapa na pale kuhusu ndoa za utotoni na ukatili wanaofanyiwa watoto hao baada ya kuolewa, tatizo katika jamii za pembezoni bado ni kubwa na linahitaji juhudi za pamoja kuwanusuru.


Mkurugenzi wa shirika la kusaidia watoto na wanawake katika jamii za kifugaji la Mimutie Women Organization (MWO), Rose Njilo anasema ukatili dhidi ya watoto umekithiri katika jamii za kifugaji na ni jambo linalopaswa kushughulikiwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali.


“Hili ni tatizo kubwa, watoto wadogo wanalazimishwa kuolewa na kwa kuwa hawana uwezo wa kukataa, wanaozeshwa na kufanyiwa ukatili mkubwa na hawana watetezi,” anasema.


Anasema shirika lake karibu kila mwezi linapokea kesi za watoto kuolewa na wengine kukimbia makazi, kutokana kulazimishwa kuingia kwenye majukumu ya ndoa wakiwa na umri mdogo.


“Hii kesi ya Mesoni ni mfano tu wa matukio ya ukatili, lakini hadi sasa nina watoto saba walifanyiwa ukatili wa ndoa hizi za utotoni,” anasema


Msimamo wa Serikali

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima anasema jamii inapaswa kukomesha ukatili wa ndoa za utotoni kuanzia kwenye ngazi ya familia.

“Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa watakaobainika kuwafanyia ukatili watoto wadogo, ikiwepo kuwaoa wakiwa chini ya umri stahiki, kuwafanyia vitendo vya ubakaji na udhalilishaji,” anaonya Gwajima.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa shirika la kusaidia ustawi wa wanawake na watoto (WOCWELS), Mary Mushi anasema changamoto kubwa ya ndoa za utoto ni sheria ndio sababu ameamua kupeleka kesi mahakamani kutetea umri wa kuolewa uwe kuanzia miaka 18.

Anasema sheria ya ndoa ina mapungufu, kwani bado inatoa haki, mtoto mdogo kuolewa kwa ridhaa ya wazazi wake

Credit to Mwananchi gazette



About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top