Mwandishi wetu, Babati
Hatimaye Halmashauri ya wilaya ya Babati mkoa wa Manyara, imeingilia kati mgogoro katika Jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori Burunge(JUHIBU) na kuirejesha bodi ya wadhamini ambayo ilikuwa imefukuzwa huku ikimsimamisha kazi mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Hamis Juma.
Sambamba na kurejesha bodi hiyo, halmashauri hiyo, imemrejesha kazini, Katibu wa Jumuiya hiyo, Benson Mwaise ambaye alikuwa ameondolewa kazini pia na baraza la uongozi la jumuiya hiyo(AA).
Bodi ya wadhamini na Katibu huyo, waliondolewa Novemba 18 mwaka huu, kutokana na mgogoro wa uwekezaji katika kitalu cha Uwindaji katika hifadhi hiyo, ambapo Bodi ya wadhamini na Katibu wa jumuiya hiyo, walikuwa wamepinga mkakati wa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Hamis Juma kuvunja mkataba na kampuni ya EBN iliyowekeza katika kitalu hicho tangu mwaka 2013.
Uamuzi wa kuirejesha bodi ya wadhamini, umetolewa na Mkurugenzi wa wilaya ya Babati,Anna Mbogo baada ya kubainisha kuvunjwa kwa sheria za WMA lakini pia kutokana na malalamiko ya wenyeviti wa vijiji na Bodi ya wadhamini kupinga maamuzi ya AA na kuomba serikali kuingilia kati mgogoro huo.
Katika barua ya mkurugenzi huyo kwenda kwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini yenye kumbu kumbu namba DED/BBT/L.3/1/38 , imeitaka bodi hiyo,kurejea kazini kuendelea na majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za WMA.
"kikao cha kuivunja bodi kilifanyika pasipo kushirikisha mamlaka za wilaya yaani ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya wala baraza la ushauri wa maliasili wilaya ambazo ni mamlaka zinazowajibika kisheria kutoa ushauri kwa JUHIBU ''alisomeka barua hiyo
Mkurugenzi wa halmashauri ameeleza kuwa, maamuzi yaliyofanywa na baraza la AA yalikuwa ni ya maslahi binafsi ya mwenyekiti wa juhibu Hamis Juma na amejiridhisha pasipo shaka kwamba baraza la AA halina mamlaka kisheria kuvunja bodi ya wadhamini iliyosajiliwa kisheria mwaka 2004 kwa usajili namba 2905 kwa sheria ya bodi ya wadhamini ya mwaka 1956.
Mkurugenzi huyo ameagiza kurejeshwa kazini, Katibu wa Jumuiya hiyo,Benson Mwaise ambaye pia alikuwa amesimamishwa kazi na AA kutokana na maslahi binafsi ya Mwenyekiti huyo wa Jumuiya.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Juma amesimamishwa kuendelea na shughuli zozote katika jumuiya hiyo, ili kupisha uchunguzi na tuhuma mbali mbali ambazo zinamkabili ikiwepo matumizi mabaya ya fedha.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mmoja wa wajumbe wa bodi ya JUHIBU , Lembice Makoa alithibitisha kupokea barua na kurejea kazini na kupongeza uamuzi wa serikali kutatua mgogoro huo.
"tunashukuru ofisi ya Mkurugenzi na serikali kwa ujumla kwa kuingilia kati na kutatua mgogoro huu kwa kulinda maslahi mapana ya uhifadhi na utalii nchini lakini pia maendeleo ya jumuiya yetu "alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti wa vijiji 10 ambavyo ambavyo vinaunda JUHIBU,Mwenyekiti wa kijiji cha Vilimavitatu Abubakari Msuya alisema wanapongeza halmashauri na Babati na Serikali kurejesha bodi na kumsimamisha kazi Mwenyekiti wa jumuiya.
"Sisi kama viongozi tulilalamika kwa viongozi wa juu,kupinga mwenendo wa AA hasa Mwenyekiti baada ya kubaini anamaslahi binafsi katika mgogoro na hata katika vikao alikuwa hatoi nafasi sisi kama wawakilishi wa wananchi kuzungumza"alisema
Hata hivyo,Mwenyekiti wa jumuiya hiyo,Hamis Juma hakuwa tayari kuelezea mgogoro huo baada ya kukata simu baada ya kuulizwa kuhusiana na kusimamishwa kazi.
Post a Comment