Jengo la Ofisi ya WMA BURUNGE |
BWAWA la MAJI lililochimbwa na kampuni ya EBN ili kuwawezesha wanyamapori kupata maji ya kunywa |
Mwandishi wetu, Babati
Baraza la Uongozi (AA) la Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge Wilaya ya Babati mkoa Manyara,limeifukuza Bodi ya wadhamini ya jumuiya hiyo baada ya kugomea kuvunja Mkataba na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya EBN ili kupisha kampuni nyingine.
Baraza hilo pia limemsimamisha kazi Katibu wa Jumuiya hiyo, Benson Mwaise ili kupisha uchunguzi kutokana na maamuzi ya Bodi ya Jumuiya hiyo na kusaini mkataba na kampuni ya EBN ambaye kwa kiasi kikubwa inafanya Utalii wa picha katika Kitalu hicho ambacho kinapakana na hifadhi ya Tarangire.
Wajumbe Bodi ya wadhamini wapinga kuondolewa
Hata hivyo Wajumbe wa Bodi ya wadhamini ya Jumuiya hiyo wamepinga maamuzi hayo na kueleza baraza hilo halina Mamlaka ya kisheria kuondoa Bodi kwani Bodi imesajiliwa kisheria.
Mmoja wa wajumbe wa bodi yenye wajumbe Saba ,Lembrice Makao akizungumza waandishi wa habari kwa niaba ya wajumbe wenzake amesema kilichofanyika ni vurugu za viongozi wachache wa baraza hilo ambao wanashinikiza kuvunja Mkataba na kampuni ya EBN na kuitaka kampuni nyingine ya Uwindaji wa kitalii
"Kwanza hawajuwi sheria siku Bodi ya wadhamini ikiondoka baraza nalo linavunjika kisheria,tunasubiri watuandikie barua zao tuwape maelekezo"amesema
Maamuzi kufukuza Bodi.
Maamuzi ya baraza hilo, yametolewa katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika jana Makao makuu ya jumuiya hiyo Burunge na kuongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo,Hamisi Juma ambaye amekuwa akitaka kampuni nyingine katika eneo hilo licha ya kushiriki katika kusaini mkataba wa awali na kampuni ya EBN Julai 14,2022.
Kikao hicho kimefanyika siku tatu baada ya kikao baina ya Bodi ya jumuiya hiyo kukutana na Maafisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii jijini Arusha,wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi na kushindwa kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na EBN.
Akizungumza katika mkutano wa baraza hilo,Hamis aliwaeleza wajumbe maamuzi ya kikao baina ya Maafisa wa Wizara juu ya kutaka kuendelea na mchakato wa kutangazwa kitalu hicho ili Kampuni nyingine zijitoke.
Juma alieleza Bodi ya wadhamini ilifanya makosa kusaini mkataba wa Julai 14 mwaka huu ili Kampuni hiyo ambayo tangu mwaka 2013 imewekeza katika Kitalu hicho.
Hata hivyo, Makao alisema mkataba na EBN ulisainiwa baada ya wizara ya Maliasili na Utalii kutoa baraka baada ya kufanya tathimini na ilishirikis Kamati ya ushauri ya Maliasili ya wilaya, maafisa kutoka taasisi za uhifadhi ikiwepo Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori.
"Wizara iliunda kamati ikiongozwa na Mwanasheria wa Wizara ndio walikuja kufanya tathimini walikaa siku nne huku Burunge na baadae walitoa barua kuridhishwa na mwekezaji na tuendelee na kusaini mkataba tunashangaa Leo hiyo hiyo Wizara inageuka na kuja kudai hatukufata taratibu "alihoji
Meneja Uhusiano wa EBN Charles Sylvester amesema mgogoro katika Kitalu unachochewa na watu wachache kwa maslahi yao ikiwepo kutaka kuwinda jirani na hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Alisema EBN ni kampuni ya kimataifa ya Utalii inayomilikiwa wawekezaji wakubwa wa Utalii wakiwepo kutoka Ufaransa, tangu mwaka 2013 wamewekeza zaidi ya billion 20 hoteli na kufanya Utalii wa picha na kuna wafanyakazi 240 ambao nao wanaathirika na mgogoro huu kinachofanyika ni kuvuruga Utalii nchini.
"Tunaomba serikali kufanya uchunguzi wa mgogoro kwani EBN ilifata taratibu zote kabla ya kusainiwa Mkataba lakini kinachofanyika Sasa ni hujuma kwa maslahi ya wachache"alisema
Mhifadhi mstaafu wa Hifadhi ya Taifa ya Tarangire ambaye aliomba kuhifadhiwa jina alisema hata kama ikifika wakati EBN ikaondoka Kitalu hicho hakina sifa ya kuwindwa wanyama kwani ni kidogo sana na ni kinyume cha sheria ya wanyamapori na muwindaji akiwinda atakuwa anaingia hifadhi ya Taifa ya Tarangire na hivyo kuharibu Utalii katika Hifadhi hiyo.
"Miaka ya nyuma kuna kampuni ilikuwa inawinda Hifadhi ya Tarangire ilikuwa shida sana na Watalii walikuwa wakilalamika maana kuna muda walikuwa hifadhini wanakutana na mnyama anavuja Damu na wengine kukimbia ovyo"alisema
Mhifadhi huyo alitaka kushirikishwa Watalaam wa taasisi ya utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI),maafisa wa TANAPA na una Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori (TAWA) kabla ya kutaka kurejeshwa Kitalu hicho katika uwindaji mkubwa wa Utalii.
Post a Comment