Mwanasheria wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Gwakisa Mlawa, amedai mahakamani kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya shirika hilo haikujua chochote kuhusu mkataba ulioingiwa kati ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Tido Mhando na Channel 2 Group Corporation (BV1).
Mlawa alidai pia mshtakiwa anayekabiliwa na tuhuma za
matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh.
milioni 887.1, aliingia mkataba huo bila baraka za bodi ya zabuni ya
TBC.
Shahidi huyo wa pili alitoa ushahidi wake jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai,
shahidi huyo alidai kuwa hakuwahi kuufahamu mkataba huo hadi alipopokea
taarifa za kesi Juni, 2012 kutoka Channel 2 Group Corporation (BV1)
kwamba TBC imekiuka mkataba wa kuwekeza mitambo ya digitali.
"Mheshimiwa hakimu mkataba huo ulisainiwa kati ya Tido na
watu wawili wa Channel 2 Group Corporation (BV1). Pia kulikuwapo na
nyongeza ya mkataba uliotiwa saini kati ya Juni, Agosti na Novemba mwaka
2008... TBC tulimwandikia Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kuomba
ushauri naye aliagiza ateuliwe mwanasheria wa kimataifa ambaye ni mjuzi
katika masuala hayo," alidai shahidi na kuongeza kuwa:
"Iliteuliwa kampuni ya uwakili ya Freshfield Bruckhaus
Derringer us LLP ilikuja nchini TBC kufanya uchunguzi wa nyaraka na
kwamba ililipwa malipo ya awali zaidi ya Sh. milioni 800...katika
uchunguzi huo, ulibaini kuwa Tido alisababisha hasara ya fedha hiyo
iliyokuwa kampuni ya uwakili," alidai Mlawa.
Alipohojiwa na wakili wa utetezi, Ramadhan Maleta, kama
aliiona mikataba hiyo, shahidi alidai kuwa ilikuwa kama wameingia
makubaliano ya awali ya maandalizi ya mchakato wa kuelekea kwenye
digitali.
Katika kesi ya msingi, inadaiwa kuwa Juni 16, 2008, akiwa
Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido ambaye alikuwa Mkurugenzi
Mkuu wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saini
mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya
TBC na channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni, kitu
ambacho ni kinyume na Sheria ya Ununuzi na kuinufaisha BVl.
Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya
madaraka yake Juni 20, 2008 alipotia saini makubaliano kwa utangazaji wa
digitali duniani kati ya TBC na BVl.
Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba
2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini
mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya
usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa Novemba 16, 2008 akiwa
Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kutia saini mkataba wa
makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast
Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Post a Comment