PRINCE MEDIA TZ PRINCE MEDIA TZ Author
Title: TEF NAO WAJA NA WARAKA WAO MZITO KWA SERIKALI
Author: PRINCE MEDIA TZ
Rating 5 of 5 Des:
  Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema tukio la kutekwa kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Comm...
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limesema tukio la kutekwa kwa mwandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda limeongeza hofu kwa waandishi wa habari nchini hasa wale wanaoripoti habari za uchunguzi

Pia, TEF imesema matukio ya kuzuiwa kwa mikutano ya siasa, kushambuliwa kwa mwanasiasa Tundu Lissu, mauaji ya Kibiti na kufungiwa kwa vyombo vya habari, hayana afya kwa Taifa
Gwanda alitoweka tangu Novemba 21 mwaka jana na mpaka sasa hajulikani alipo

Kaimu Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alisema jana kuwa jukwaa hilo limetafakari kwa kina na kujadili hali inayoibua sintofahamu na malalamiko kutoka katika makundi mbalimbali ndani ya jamii

“Kuminywa kwa uhuru wa maoni, athari yake ni kikwazo cha utendaji na ufanisi wa vyombo vyetu vya habari huku hofu ikiwafanya wananchi kusita kuzungumza na vyombo vya habari wanapohitajika kufanya hivyo,” alisema Balile

Alisema malalamiko mengi yaliyo katika jamii yanagusa kuminywa kwa uhuru wa kutoa maoni hasa kupitia vyombo vya habari, kuzorota kwa demokrasia nchini kwa ujumla wake na ukuaji wa uchumi usioakisi hali halisi ya watu

Alisema vyombo vya habari nchini vinafanya kazi katika mazingira magumu na ya woga kutokana na watendaji wake kuitwa na kuhojiwa na mamlaka kama Idara ya Habari –Maelezo kwa magazeti na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa vyombo vya kielekroniki

“Na wakati mwingine kupewa adhabu kubwa za kulipa faini au kufungiwa na baadhi ya adhabu nyingine kama kufungia magazeti zikitolewa kinyume cha Sheria ya Huduma ya Habari ya Mwaka 2016,” alisema Balile

Alipoulizwa kuhusu taarifa ya TEF, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alisema, hajaipata. Hata alipoelezwa maudhui ya taarifa hiyo aliomba atumiwe ili aisome na alipotumiwa hakupatikana tena kuizungumzia

Kuhusu mikutano ya vyama vya siasa Balile alisema, imezuiwa kinyume cha sheria huku vyama vya upinzani vikiathiriwa zaidi kwa kuwa watendaji wa chama tawala wanaendelea na shughuli za kisiasa kama kawaida

Kadhalika, Balile alieleza kuwa matukio ya mauaji ikiwamo ya Kibiti, ya Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Akwilina Akwiline, askari wanane Kibiti, mashambulizi ya risasi kwa Lissu, yamezidisha woga kwa wanahabari kwa kuwa hayajapata majibu ikiwamo wahusika kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. “Tunayo mifano ya nchi nyingi duniani, zilizoingia katika gharama kubwa kwa kudharau matukio madogo kama yanayotokea nchini mwetu hivi sasa,” alisema

Balile alisema TEF, kama wataalamu wa habari wanaotazama mambo kwa jicho la kiuchambuzi, wanashauri kuwapo kwa meza ya mazungumzo kitaifa kwa Serikali kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii ili kujadiliana kuhusu mustakabali wa amani na maridhiano ya kitaifa


Hata hivyo, Balile alisema TEF inapongeza na kutambua juhudi za Serikali za kusimamia misingi ya uwajibikaji, vita dhidi ya rushwa na ufisadi na usimamizi wa mapato ya Serikali na matumizi endelevu ya raslimali za umma.

About Author

Advertisement

Post a Comment

 
Top