Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Maj. Gen. Gaudence S. Milanzi (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Historia Asilia ya Berlin Ujerumani (Berlin Museum of Natural History), Prof. Johannes Vogel kuhusu masalia ya mjusi wa Tanzania yaliyofadhiwa katika makumbusho hiyo.
.....................................................
Ujerumani na Tanzania zimekubaliana kuendeleza tafiti za masalia ya mijusi katika eneo la Tendaguru mkoani Lindi.
Makubaliano
hayo yamefikiwa baada ya Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii,
Maj. Gen. Gaudence Milanzi kutembelea Makumbusho ya Historia Asilia ya
Berlin (Berlin Museum of Natural History) nchini Ujerumani
yanapohifadhiwa pia masalia ya mijusi waliopatikana eneo la Mlima
Tendaguru mkoani Lindi.
Maj.
Gen. Milanzi aliongoza msafara wa Tanzania ulioshiriki maonesho ya
Kimataifa ya utalii ya ITB Berlin 2018 yaliyohitimishwa jana nchini
Ujerumani. Maonesho hayo yaliyoanza tarehe 7 mwezi huu yalihusisha
taasisi 5 za Serikali na Makampuni binafsi 60 kutoka Tanzania.
Mkurugenzi
Mkuu wa Makumbusho hiyo, Prof. Johannes Vogel alimueleza Maj. Gen.
Milanzi kuwa shughuli kubwa inayofanywa na makumbusho hiyo ni utafiti
kwa ajili ya maendeleo ya sayansi, elimu na ufahamu wa mambo mbalimbali
kuhusu Dunia, viumbe pamoja na mazingira ili maarifa na ufahamu huo
usaidie binadamu kutawala maisha yake na mazingira yanayomzunguka.
Akizungumzia
fursa zilizopo za kushirikiana kutafiti maeneo yalikopatikana masalia
ya mijusi hao na viumbe wengine Prof. Johannes alisema, Makumbusho yake
ipo tayari kushirikiana na Wanasayansi wa Tanzania ili kujenga uwezo wa
kufanya utafiti na kupata matokeo yatakayochangia katika hazina ya
maarifa na sayansi ya viumbe na mazingira.
“Ili
kuwa na utafiti endelevu, ni vema kwa nchi ikawekeza kwa wataalamu wake
ili kuendeleza utafiti na maendeleo ya sayansi. Hivyo tupo tayari
kushirikiana ili kujenga uwezo kwa wasomi wa Tanzania kuweza hatimaye
kufanya utafiti na kuleta maendeleo kwa nchi yao” alisema.
Akizungumzia
kuhusu masalia ya mijusi waliopatikana Tendaguru na ambayo
yanahifadhiwa katika makumbusho hiyo, alisema badala ya kuwarudisha
nchini Tanzania, ni vema wakachukuliwa kuwa elimu, utafiti na maendeleo
ya sayansi yanayopatikana kutokana na kuwafanyia utafiti ni kwa
maendeleo na ustawi wa dunia nzima.
“Ichukuliwe
kuwa huu ni urithi wa dunia nzima na hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha
kuwa urithi huu hauachi ukapotea. Hivyo, ni vema tukaimarisha utafiti
katika eneo walikopatikana ili kupata masalia mengi zaidi na kuitangaza
Tanzania katika Nyanja za utafiti.
“Makumbusho
yangu ipo tayari kufanya ziara ya kuimarisha mazungumzo na mamlaka za
Tanzania mapema iwezekanavyo ili utafiti katika eneo la Tendaguru
uendelee kwa manufaa ya Tanzania na Dunia nzima”. alisema Prof.
Johannes.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu Milanzi aliahidi kuwapa ushirikiano ili
kuwezesha tafiti hizo kufanyika kwa ajili ya ustawi wa sayansi na uchumi
wa nchi zote mbili. Alimkaribisha Prof. Johannes na timu yake kuja
Tanzania mapema iwezekanavyo ili kujadili na kukamilisha makubaliano ya
kuendeleza tafiti hizo.
Awali,
Maj. Gen. Milanzi alipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na
Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Dk. Abdalla Possi. Miongoni mwa
mambo waliyozungumza ni pamoja na masalia hayo ya mjusi wa Tanzania
anayehifadhiwa katika moja ya makumbusho nchini humo.
Balozi
Possi alisema kuwa kwa maoni yake haoni kuwa wazo la kuhamisha masalia
hayo kurudishwa Tanzania kuwa litakuwa na tija kwa maendeleo ya utalii
na utafiti wa sayansi kwa nchi yetu.
Alitoa
baadhi ya sababu kuwa sio kweli kuwa masalia hayo ndiyo kivutio kikubwa
pekee kinachofanya wanasayansi na watalii wengi kutembelea makumbusho
hiyo na hivyo kuipa mapato makumbusho hiyo.
“Makumbusho
inapata ruzuku kutoka serikalini na kiingilio ni sehemu ndogo sana ya
mapato ya makumbusho hiyo. Fedha nyingi za kufanyia shughuli za
Makumbusho ya Berlin zinatokana na fedha zinazolipwa kwa ajili ya
kufanya utafiti na si viingilio katika makumbusho” alisema Dk. Possi.
Alisema
makumbusho hiyo ina mikusanyo mingi ya viumbe mbalimbali zaidi ya
milioni 30 ikiwemo ya mijusi kutoka nchi nyingine duniani. Mkusanyiko
huo kwa pamoja unatoa mvuto kwa watafiti na watalii kutembelea na
kufanya shughuli zao chini ya makumbusho hiyo.
Dk.
Possi alisema kuendelea kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo kuna
manufaa zaidi ya kuitangaza Tanzania kiutalii na utafiti wa kisayansi
kuliko masalia hayo yatakapoondolewa katika makumbusho hiyo na
kurejeshwa nchini Tanzania.
Alisema
kuwepo masalia hayo katika makumbusho hiyo ni kama Balozi wa utalii na
utafiti wa kisayansi anayeitangaza Tanzania sehemu mbalimbali duniani.
Akizungumzia
mchakato unaoendelea hivi sasa hapa nchini wa kuandaa Utambulisho mpya
wa Tanzania (National Branding), Balozi Possi alishauri kuwa ni vema
mabadiliko yatakayopelekea kuondokana na utambulisho unaotumika hivi
sasa ukaangaliwa kwa umakini kwa kuwa kuna hatari ya kupoteza msisitizo
uliopo katika vivutio maarufu vya utalii nchini na kutoa fursa kwa
washindani kutangaza utalii wao kupitia vivutio hivyo.
Alisema
endapo hakuna athari kwa kutumia utambulisho wa sasa ambao ni maarufu
(Tanzania the Land of Kilimanjaro, Serengeti and Zanzibar), ni vema
zikaangaliwa pia athari zitakazopatikana kwa kuachana na “brand”
inayotumika hivi sasa.
Alisema
kuwa baadhi ya vitu vinavyotumika kwenye utambulisho wa sasa tayari ni
“brand”. Alitoa mfano kuwa Mlima Kilimanjaro ni Brand maarufu na
inayojiuza, hali kadhalika kwa Serengeti na Zanzibar.
Post a Comment