MAPEMA Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura
alilalamika kubaniwa haki yake ya kukataa rufaa baada ya kupatikana na
hatia na kufungiwa maisha kujihusisha na soka.
Lakini leo ndiyo ile siku ambayo amekuwa akiisubiri kwa hamu kubwa na atakuwa na nafasi ya kusikilizwa.
Wambura
amepanga leo kutinga katika ofisi za shirikisho hilo akiwa amejiandaa
na yuko vizuri kwelikweli kujitetea kwenye Kamati ya Rufaa ya Maadili ya
TFF ambayo inakutana leo Jumamosi.
Hatua
hiyo imekuja baada ya Machi 15, mwaka huu, Kamati ya Maadili ya TFF
kutangaza kumfungia Wambura kutojihusisha na masuala ya soka maisha yake
yote baada ya kumkuta na makosa matatu.
Makosa
hayo ni kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kughushi barua ya
kuelekeza malipo ya Kampuni ya Jeck System Limited na kushusha hadhi ya
shirikisho hilo.
Baada
ya kutoka kwa hukumu hiyo, Wambura na wakili wake, Michael Muga,
walikata rufaa ambayo leo Jumamosi itajadiliwa na kutolewa uamuzi.
Wambura alisema amejipanga kikamilifu kwenda kujitetea kutokana na kutoridhika na jinsi ishu yake hiyo ilivyoendeshwa.
“Nina
kila sababu ya kujipanga kwenda kujitetea kwani naamini sikutendewa
haki kwa sababu hakuna ushahidi wa kile ambacho nimetuhumiwa nacho,”
alisema Wambura.
Naye
Wakili Muga alisema, mteja wake huyo yupo tayari kwenda kujitetea na
yeye ataendelea kuwa upande wake licha ya kuwepo kwa taarifa za kutakiwa
ajiondoe baada ya TFF kuwasilisha barua kwenye Chama cha Wanasheria
Tanzania (TLS) wakitaka asiendelee kumtetea.
“Mteja
wangu yupo tayari kwa kujitetea na mimi nitaendelea kuwa upande wake
kwa sababu TLS siyo kazi yao kumuambia wakili asimuwakilishe mteja na
haijawahi kutokea,” alisema Muga.
CREDIT: CHAMPIONI
Post a Comment