Katibu wa Bunge wa zamani, Dk Thomas Kashililah amesema, Rais John Magufuli hakufanya kosa katika uteuzi wa Katibu wa Bunge.
Rais Magufuli jana Jumamosi alimteua Steven Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge, uteuzi ambao umeibua hoja kwamba sheria haikufuatwa.
Dk Kashililah akizungumza na mwananchi leo Jumapili, amesema kwa mujibu wa ibara ya 87(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano mamlaka ya uteuzi haikufanya kosa licha ya sheria ya Bunge kuelekeza utaratibu.
Amesema, “Mamlaka ya uteuzi iko sahihi… unajua sheria haiko juu ya Katiba na Katiba iko juu ya sheria, hivyo Rais akiamua anaweza kufanya hilo, sheria haiwezi kumzuia,” amesema Dk Kashililah akisisitiza ibara ya 87 iko wazi.
Ibara hiyo inasomeka: “Kutakuwa na Katibu wa Bunge ambaye atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye madaraka ya juu katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”
Dk Kashililah amesema: “Kama aliyeteuliwa angekuwa hayuko kwenye madaraka ya juu hapo sawa, lakini huyu aliyeteuliwa (Kagaigai) ni mtu senior kabisa serikalini na ana vigezo hivyo… kuna watu wanapotosha ukweli.”
Post a Comment