Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
SERIKALI ya China imeipatia Tanzania msaada
wa Shilingi bilioni 29.4 kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu ya ufundi stadi,
utalii wa kijiolojia na kukarabati wa Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini
Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto
James, kwa niaba ya Serikali, na Kaimu Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Gou
Haodong.
Bw. Doto James alisema kuwa kiasi cha
Shilingi bilioni 22.4 cha msaada huo kitatumika kujenga Chuo cha Ufundi Stadi-VETA
wilayani Ngara mkoani Kagera, ambacho kitakapo kamilika kitadahili zaidi ya
wanafunzi 400.
“Fedha hizo zitatumika kujenga vyumba 19
vya madarasa, ujenzi wa karakana 9 za kutolea mafunzo ya elektroniki, ufundi
bomba, useremala, ufundi uashi na upakaji rangi” alisema Bw. James
Alieleza kuwa kiasi hicho pia kitatumika
kujenga majengo ya utawala, mabweni, nyumba za walimu na miundombinu mingine
itakayosaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwenye chuo
hicho.
“Tunaamini kwamba msaada huo utakuwa sehemu
ya kusaidia jitihada za Serikali za kujenga uwezo wa wataalamu wake watakaochangia
kukuza sekta ya uzalishaji na hatimaye kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira
kwa vijana nchini” alisema Bw. James
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Fedha na
Mipango Bw. Doto James alibainisha kuwa katika makubaliano ya msaada huo,
Jamhuri ya watu wa China, itatoa kiasi cha shilingi bilioni 6.7 kwa ajili ya kuukarabati
Uwanja wa Taifa wa Michezo wa Dar es Salaam.
“Katika makubaliano yetu ya msaada wa
kuendeleza Uwanja wa Taifa wenye uwezo wa kuingiza watu 60,000, China itatoa
msaada wa kiufundi na vifaa vya kisasa vya michezo na utaalamu katika usimamizi
na ukarabati wa uwanja” Alifafanua Bw. James
Bw. Doto James alisema kuwa kiasi kingine
cha shilingi milioni 300 kitatumika kwa
ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kuanzishwa kwa aina mpya ya utalii
ujulikanao kama utalii wa kijiolojia “Geopark Project” katika Hifadhi ya Taifa
Ngorongoro, mkoani Arusha.
Alisema lengo la utafiti huo ni kuhakikisha
kuwa Tanzania inanufaika na maajabu mbalimbali ya kitalii yaliyopo nchini
ambayo hayajatumika kikamilifu kuvutia watalii watakaoongeza pato la Taifa
“Tanzania ina kila sababu ya kujifunza
kutoka katika Hifadhi ya Kimataifa ya Jiolojia ya Jiaozuo ya Yuntaishan ya
China, iliyoanzishwa mwaka 2000 ambayo inaongeza asilimia 37.2 ya watalii kila
mwaka na huchangia asilimia 12 ya pato la Taifa la nchi hiyo” aliongeza Bw.
Doto James.
Aliishukuru China kwa ushirikiano wake wa
dhati na Tanzania tangu miaka ya 1960 na kwamba mpaka sasa nchi hiyo imeendelea
kuipiga jeki Serikali katika ujenzi wa miradi mbalimbali ukiwemo upanuzi wa
Chuo cha Polisi Moshi, Ujenzi wa Maktaba mpya katika Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki.
Kwa upande wake Kaimu Balozi wa China hapa
nchini, Mhe. Gou Haodong, amesema kuwa nchi yake inatarajia kwamba ujenzi wa
Chuo Cha Ufundi VETA huko Ngara mkoani Kagera utaanza haraka kama ilivyopangwa.
Kuhusu masauala ya utalii wa kijiolojia
katika Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, alisema Tanzania ina bahati ya kuwa na
vivutio vingi vya utalii lakini haijavutia idadi kubwa ya watalii kutoka China
kuja kuvitembelea.
“Zaidi ya watalii milioni moja kutoka China
wanatembelea nchi mbalimbali dunia lakini kati ya hao, Tanzania inapokea
watalii elfu 20 tu kila mwaka kutoka China, lakini kwa kuanzisha mradi huu, watalii
wengi kutoka China watavutiwa kuja nchini kufurahia utalii wa miamba, mandhari
nzuri, urithi wa dunia, na kutembelea hifadhi za Taifa” aliongeza Mhe. Haodong
Akizungumzia masuala ya uchumi, Balozi huyo
alisema kuwa hivi sasa China imekuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa
kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.77 na kukuza ajira nchini.
Ameitaja baadhi ya miradi mikubwa
iliyowekezwa kuwa ni pamoja na mradi wa miundombinu ya mtandao (Tanzania
ICT Broadband backbone), Bomba la gesi la kutoka Mtwara hadi Dar es
Salaam, mradi wa kuboresha miundombinu ya Bandari, barabara na madaraja.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu
wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo, ambaye alisema
kuwa msaada wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA mkoani Kagera kitaongeza watalaamu
watakaosaidia kuendeleza sekta ya viwanda nchini.
Post a Comment