Mwezeshaji
wa mafunzo ya nembo na vifungashio, Emmanuel Bakashaya, akifundisha
akinamama wa Green Voices jinsi nembo na vifungashio vinavyopaswa
kuonekana.
Akinamama
wa Green Voices wakiwa katika ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) wakijifunza kutoka kwa Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula, Raymond
Wigenge, hivi karibuni.
Green
Voices katika majadiliano ya vikundi juu ya njia mbali mbali za
kutafuta rasilimali wakati wa mafunzo chini ya mwezeshaji Richard
Jackson.
Green
Voices wakiangalia bidhaa za ujasiriamali za Mama Rocky (mwenye mtandio
wa buluu) katika supermarket. Hii ni baada ya kumtembelea kiwandani
kwake katika ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Maendeleo ya Viwanda
Vidogo (SIDO) jijini Dar es Salaam.
Dkt.
Alicia Cedaba, Meneja wa Mradi wa Green Voices kutoka Hispania,
akifundisha akinamama wanaotekeleza mradi huo nchini Tanzania.
Akinamama wa Green Voices wakiwa katika mafunzo kwa vitendo katika makao makuu ya SIDO jijini Dar es Salaam.
Green
Voices baada ya kuhitimu mafunzo. Walioketi kutoka kushoto ni Mratibu
wa Green Voices nchini Tanzania, Secelela Balisidya, Mkurugenzi wa
taasisi ya IMED iliyotoa mafunzo, Dkt. Donath Olomi na Meneja wa Mradi
wa Green Voices kutoka Madrid, Hispania, Dkt. Alicia Cebada.
AKINAMAMA
wanaotekeleza mradi wa Green Voices nchini Tanzania sasa wanalenga
kuboresha bidhaa za kilimo wanazozalisha ili kuongeza tija ikiwa ni
katika azma yao ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Wakizungumza
baada ya semina ya wiki moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi
karibuni, akinamama hao walisema elimu waliyoipata imewapa mwanga wa
kuendeleza miradi yao na kuhakikisha wanaboresha bidhaa zao ili ziwezi
kuingia katika soko la ushindani.
Miradi
inayotekelezwa kupitia Green Voices Tanzania ni kilimo cha mihogo,
kilimo cha matunda, uyoga, ufugaji wa nyuki, ukaushaji wa mbogamboga na
utengenezaji wa majiko rafiki wa mazingira ambayo inatekelezwa katika
mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Kigoma, Mwanza na Kilimanjaro.
“Nilikuwa
nimekata tamaa nisijue nitauendelezaje mradi wangu, lakini kwa mafunzo
niliyoyapata kutoka kwa wataalam mbalimbali, hakika nimehamasika na
kuona kwamba ninaweza kusimama na kusonga mbele,” alisema Farida Makame
ambaye anasimamia mradi wa Majiko ya Umeme-Jua mkoani Kilimanjaro.
Farida
alisema amehamasishwa zaidi na mafunzo hayo, ambayo yamempatia mbinu
mpya zaidi za kuendeleza mradi huo kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Abiah Magembe anayesimamia mradi wa Usindikaji wa Muhogo na Mtama katika
Kijiji cha Kitanga, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, amesema mafunzo ya
jinsi ya kufungasha na kuweka nembo kwenye bidhaa yamempa mwanga mkubwa
na kwamba sasa yeye na wenzake watazalisha bidhaa zao kwa kujiamini na
kuziingiza kwenye soko la ndani na la kimataifa.
“Tunatengeneza
bidhaa nyingi zinazotokana na muhogo na zina viwango vizuri, lakini kwa
mafunzo tuliyoyapata, sasa tunaweza kuziboresha kwa kuhusisha taasisi
husika kama Shirika la Taifa la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na
Dawa (TFDA) ili tuingie kwenye ushindani wa kitaifa na kimataifa,”
alisema Bi. Magembe.
Bi.
Magembe alisema kwamba, bidhaa wanazozalisha kutokana na zao la muhogo
ni unga unaotumika kwa uji na ugali, vitafunwa kama keki, mikate,
skonzi, biskuiti, mandazi, sabuni ya unga pamoja na bidhaa nyingine
nyingi.
Mazao
mengine yanayopatikana katika muhogo ni mzizi wenyewe ambao unatafunwa
mbichi au ukiwa umepikwa au kukaangwa, kwenye futari, miti na majani
huweza kuzalisha bidhaa anuwai za viwandani kama vifaa vya nguo,
karatasi, mafuta, kilevi, dawa za binadamu na plastiki wakati ambapo
wanga (starch) hutumika kutengeneza dawa za madoa, gundi katika samani, rangi za awali za ukuta na sukari (sugar syrup).
Takwimu
za kilimo cha muhogo duniani zinaonyesha kuwa, Afrika ni bara la tatu
duniani kwa kuzalisha zaidi muhogo ambapo huzalisha takriban tani
milioni 102.6 kila mwaka.
Tanzania
ni nchi ya nne kati ya wazalishaji wakubwa wa muhogo barani Afrika
baada ya Nigeria, Ghana na Congo DRC ambapo inaelezwa kwamba karibu
ekari 670,000 za ardhi ya kilimo zinatumika kuzalisha muhogo, zao
linalochangia karibu asilimia 15 za chakula kwa nchi nzima na karibu
kaya 1,213,958 huzalisha muhogo nchini.
Regina Kamuli ambaye anasimamia mradi wa Majiko Banifu wilayani
Mkuranga, alisema anashukuru wanakikundi wenzake wamejizatiti na sasa
wanapata fursa ya kushiriki katika maonyesho mbalimbali yakiwemo ya
kilimo kuonyesha majiko hayo ambayo ni rafiki wa mazingira.
“Hivi
sasa baada ya kikundi kusajiliwa akinamama wamenufaika na mikopo nafuu
kutoka Halmashauri ya Wilaya na kwa mafunzo haya tutaboresha majiko yetu
ili tuyanadi katika maeneo mengi nchini Tanzania kwa sababu yanatumia
kuni kidogo, hivyo kuokoa mazingira,” alisema Regina.
Magdalena Bukuku anaongoza kikundi cha akinamama wanaoshiriki Kilimo cha Uyoga huko
Bunju jijini Dar es Salaam, ambapo anasema mafunzo ya ufungashaji na
uwekaji wa nembo yamempa mwanga mkubwa ili kwenda kuboresha bidhaa zao
ziingie kwenye ushindani.
“Tunazalisha
uyoga kwa wingi kwa sasa na wateja wameongezeka, hata hivyo, ikiwa
tutafungasha vizuri na kupanua kilimo chetu tunaweza kulifikia hata soko
la kimataifa,” alisema.
Mariam
Bigambo na Monica Kagya wao wanashiriki ufugaji wa nyuki ambapo mbali
ya kuvuna asali, lakini wanasaidia kutunza mazingira na kuongeza tija
katika mazao ya kilimo kutokana na uchavushaji.
Wakati Mama Bigambo anaendesha Ufugaji wa Nyuki huko
Dakawa, Morogoro, Bi. Monica yeye na akinamama wenzake wana jukumu
kubwa la kutunza misitu ya Pugu na Kazimzumbwi wilayani Kisarawe
kutokana na Ufugaji wa Nyuki.
“Tunataka tujikite katika kufungasha vizuri asali na kuziwekea nembo ili tuingie kwenye ushindani,” walisema.
Suala
la ufungashaji na uwekaji wa nembo nalo limewagusa Esther Muffui, Dkt.
Sophia Mlote na Leocadia Vedasto ambao wanashiriki katika kilimo na
ukaushaji wa mboga na matunda.
“Tunajihusisha na Ukaushaji wa Mboga na Matunda kule
Morogoro, sasa tulikuwa tunashindwa kufungasha vizuri, naamini tumepata
mwanga wa namna ya kufungasha bidhaa zetu ili tupate tija zaidi,”
alisema Bi. Esther.
Leocadia yeye anashiriki mradi wa Kilimo na Usindikaji wa Viazi Lishe huko Ukerewe mkoani Mwanza wakati Dkt. Mlote anashiriki mradi wa Kilimo Hai cha Nyanya na Mbogamboga Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
Naye Evelyn
Kahembe ambaye anaendesha Kilimo cha Matunda huko Uvinza, Kigoma,
amesema mafunzo hayo yamemuongezea ujasiri wa kuendeleza mradi huo
akishirikiana na wanawake wengine huko Kigoma.
Kwa
upande wake, Mratibu wa Mradi wa Green Voices Tanzania, Bi. Secelela
Balisidya, alisema mafunzo waliyoyapata yametoa mwanga mkubwa kwa
washiriki na kuleta mtazamo wa kibiashara zaidi tofauti na hapo mwanzo.
“Suala
la ufungashaji wa bidhaa ni la muhimu na imekuwa vyema tumepata mafunzo
ya kina pamoja na kutembelea taasisi kama Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA) pamoja na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO),
tumejifunza mengi ambayo yamebadili mtazamo wetu,” alisema Secelela.
Post a Comment